2013-08-30 15:30:17

Kardinali Joseph Mazombwe afariki dunia


Kanisa barani Afrika na kote duniani linaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia kuomboleza kifo cha aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Lusaka, Kardinali Medardo Joseph Mazombwe, aliyefariki dunia siku ya Alhamisi (29.08.2013) kwenye hospitali ya Chuo Kikuu cha Ukufunzi cha Lusaka.
Kardinali Mazombwe alizaliwa kunako tarehe 24 Septemba 1931 kwenye kitongoji cha Katete kilichoko Mashariki mwa Zambia. Alipewa daraja ya Upadri tarehe 4 Septemba 1960 na hatimaye kuteuliwa kuwa Askofu wa jimbo la Chipata mnamo tarehe 7 Februari 1971. Cardinali Mazombwe alihudumu kama Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Lusaka kuanzia mwaka 1996 hadi kustaafu kwake hapo mwaka 2006.
Tarehe 30 mwezi Novemba 2010 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa Kumi na sita kwenye kikao cha hadhara katika Basilika ya Mtakatifu Petro mjini Vatican, alimteua Askofu Joseph Mazombwe kuwa Kardinali wa kwanza mwenyeji wa Zambia.
Mama Kanisa atamkumbuka Kardinali Mazombwe kwa mchango wake mkubwa kupitia huduma mbalimbali ndani na nje ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba katika uhai wake, Kardinali Mazombwe amehudumu kwenye nafasi muhimu mbalimbali. Kwa vipindi vitatu vya miaka mitatu mitatu, Kardinali Joseph Mazombwe aliwahi kuchaguliwa kama rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, na pia kuhudumu kama Mwenyekiti wa Baraza la Mabaraza ya Maskofu Katoliki Afrika Mashariki na ya Kati (AMECEA) tangu 1979 hadi 1986.
Kwenya matayarisho ya kuadhimisha jubilee ya miaka 2000 ya ukristu, Kardinali Mazombwe, akiwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Lusaka alishiriki kikamilifu kwenye kampeni ya kuiomba jumuiya ya kimataifa kufutilia mbali deni la kimataifa la nchi yake ya Zambia. Zambia na mataifa mengi duniani yalijiunga na kampeni hiyo ya kimataifa kama tendo la kuuunga mkono mwito wa aliyekuwa Baba Mtakatifu Yohani Paulo II kwa jumuiya ya kimataifa kuonesha mshikamano na nchi nyingi zinazoendelea na zinazojitahidi kujitoa kwenye umaskini usio na kifani, lakini zinajipata zikiendelea kusongwa na uzito wa madeni kimataifa.
Kanisa la Zambia pia litamkumbuka Cardinal Mazombwe kwa mchango wake wa kichungaji na kujitoa bila ya kujibakiza na hasa katika kujenga Kanisa Kuu la Mtoto Yesu lililoko mjini Lusaka. Kardinal Mazombwe pia atakumbukwa kwa ujasiri na moyo wa matumaini hata katika kukabiliana na ugonjwa wa saratani ambao aliupokea kwa moyo wa imani kuu.
Mungu aiweke roho yake Kardinal M. Joseph Mazombwe mahali pema mbinguni.










All the contents on this site are copyrighted ©.