2013-08-28 11:32:41

Wa-Augostini waanza Mkutano wao Mkuu.


Jumatano hii, 28 Augost, Mama Kanisa akiadhimisha Siku Kuu ya Mtakatifu Augostine, Mwalimu wa kanisa, mwanzilishi na Baba wa Wa -Augoustini, wanashirika Wa-Augustini walianza mkutano wao Mkuu wa 184, hapa mjini Roma.

Mkutano unao fanyika kwa mujibu wa kanuni na taratibu za shirika, ukiongozwa na Makamu Mkuu wa shirika Padre Michael Di Gregorio.

Madhumuni makuu, ni kuona jinsi wanavyoweza kukuza umoja na mshikamano zaidi, kwa manufaa ya wanashirika wote. Mshikamano na umoja thabiti katika maisha ya shirika, unaoweza kuonekana kupitia shuhuda za maisha ya wanashirika, yenye kuangaziwa na mwanga wa maisha ya kiroho wa Mtakatifu Augostine, mahali popote walipo.

Na kwamba, Mababa wa Mkutano watachambua kwa kina, uwajibikaji wao katika kufanikisha manufaa ya wote, kama inavyotamkwa katika katiba ya shirika sura ya XX1.
Aidha Mkutano huu, utafanya uchaguzi wa Kiongozi wake , atakayechukua nafasi ya Padre Robert F. Prevost, anayemaliza muda wa kuwa mkuu wa shirika kwa mujibu na kanuni za shirika.

Historia ya shirika la Mtakatifu Augostine inasema Desemba 16 1243, Papa Innocent IV, alitoa tamko lake rasmi lililozitaka jumuiya ndogondogo katika mkoa wa Tuscany italia, kuungana na kuwa shirika moja la kidini kwa sheria na njia ya maisha ya Mtakatifu Augostine. Na hivyo Mwezi March 1244, Shirika lilifanya mkutano wake mkuu wa kwanza mjini Roma, chini ya maongozi ya Kardinali Richard Annibaldi, mkutano uliwezesha jumuiya hiyo kuanza kama shirika jipya la Mtakatifu Augostine.








All the contents on this site are copyrighted ©.