2013-08-27 10:37:02

Ujumbe kwa Siku ya Mazingira nchini Italia


Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake, bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe. RealAudioMP3
Ni sehemu ya Maandiko Matakatifu inayoonesha kwamba, binadamu ana uwezo wa kutunza au kuharibu mazingira. Haya ni mambo ambayo yako kwenye uamuzi wa binadamu mwenyewe kwani yanategemea jinsi ambavyo anatumia akili na hekima aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu.

Baraza la Maaskofu katoliki Italia katika Maadhimisho ya Siku ya Nane ya kutunza Mazingira inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Septemba, mwaka huu wanaongozwa na kauli mbiu inayosema kwamba, familia ina wajibu wa kuelimisha kuhusu utunzaji bora wa mazingira. Familia ni ni shule ya kwanza ya utunzaji wa mazingira na chemchemi ya hekima inayomwezesha mwanadamu kufanya maamuzi ya busara kuhusu hatima ya maisha yake.

Hivi ndivyo alivyofanya Bikira Maria aliyeitegemeza Familia Takatifu kwa mikono yake mitakatifu, kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu kwenye karakana yake ya Useremala hata akamfundisha Mtoto Yesu kupenda mazingira na kumtukuza Mungu anayewaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

Dhamana ya Familia katika kufundisha utunzaji wa mazingira nchini Italia inakwenda sanjari na Maadhimisho ya Juma la shughuli za Kijamii kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini Italia, litakaloanza kutimua vumbi hapo tarehe 12 hadi 15 Septemba, 2013 Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia. Maadhimisho haya yataongozwa na kauli mbiu “Familia tumaini na kesho ya Jamii ya Kiitalia. Ni maadhinisho yanayokwenda sanjari na Mwaka wa Imani na Kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Huu ni mwaliko kwa waamini kujisomea tena Nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ili kutambua na hatimaye, kumwilisha amana ya ujumbe huu ambao kamwe hauwezi kupitwa na wakati.

Waraka wa Gaudium et Spes, Yaani Kanisa katika ulimwengu mamboleo unakazia umuhimu wa Familia kwa kusema kwamba, Familia ni shule ya kujitajirisha kibinadamu; ni msingi wa jamii na mahali pa kusaidiana ili kufikia busara ya kibinadamu iliyo kamili zaidi, inayoangalia na kuzingatia haki msingi za binadamu na madai mengine ya maisha ya kijamii.

Katika hija ya maadhimisho ya matukio yote haya wanasema Maaskofu Katoliki wa Italia kwamba, wanaongozwa na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko anayeendelea kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kulinda na kutunza mazingira, kwani hii ni kazi ambayo kila binadamu amekabidhiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, utume unaopaswa kuendelezwa kwa kuwajibika zaidi, ili kuubadili ulimwengu uweze kuwa ni bustani inayopendeza zaidi na kuwa ni makazi ya wote. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya mazingira, binadamu na viumbe wengine; uhusiano huu kwa namna ya pekee kabisa unamgusa mwanadamu.

Mama Kanisa amekuwa akizungumzia kuhusu ekolojia ya binadamu na ekolojia ya mazingira. Wananchi wa Italia kama walivyo wananchi katika nchi nyingine duniani wanakabiliwa na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Athari hizi zinajionesha pia katika mazingira, lakini zaidi ni athari ambazo zimegusa utu na heshima ya binadamu. Huu ni utamaduni wa kutojali hali ambayo kwa sasa inaonekana kuwa ni jambo la kawaida kwa watu wengi.

Maisha na binadamu mwenyewe si tena tunu msingi ambazo zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na Jamii ili ziweze kulindwa, kutunzwa na kukuzwa. Hali hii ni mbaya zaidi kwa: watoto ambao hawajazaliwa, watu wenye ulemavu na wazee ambao kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba, hawana haki ya kuendelea kuishi. Utamaduni wa watu kutojali umepelekea uharibifu mkubwa wa chakula ambacho kingeweza kutumika kwa ajili ya kuwalisha watu wenye njaa. Inasikitisha kuona kwamba, kuna chakula cha kutosha duniani lakini bado kuna watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa sehemu mbali mbali za dunia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linabainisha kwamba, Familia ina uwezo na wajibu wa kurithisha elimu ya kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira, kwa kutambua mwelekeo wake wa shughuli za kichungaji kiekumene na kijamii. Linasema kuna haja Jamii kujenga na kudumisha utamaduni wa kulinda na kutunza mazingira, kwa kuwa na majitoleo thabiti; kwa kusaidiana na kurekebisha kasoro zinapojitokeza.

Familia itambue kwamba, ni zawadi safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, ina dhamana na utume ambao inapaswa kuutekeleza hapa duniani kwa kuendeleza uhusiano mwema na uhuru unaomwajibisha binadamu kuweza kupima vitu kwa hekima na busara. Ni mwaliko wa kuwa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu, hali inayojionesha katika sala na ile furaha ya kushirikishana kidugu katika kutunza nyumba pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya maji; kubana matumizi na kutunza mazingira. Mwanadamu anaishi katika bustani ambayo amepewa dhamana ya kuitunza na kuiendeleza.

Familia inapaswa kutambua kwamba, ipo kwa ajili ya kusaidiana kwa hali na mali sanjari na ujenzi wa mahusiano bora na yenye tija, huku wanafamilia wenyewe wakijitahidi kuheshimiana na kuthaminiana katika tofauti zao; ambazo kimsingi ni kwa ajili ya kukamilishana kadiri ya mpango wa Mungu. Familia ijifunze kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano ili kuondokana na mashindano yasiyokuwa na tija miongoni mwa wanaume na wanawake. Huu ni umoja unaojidhihirisha katika utofauti wake ili kushirikiana na wala si kudhaniana kuwa ni maadui. Moyo wa ushirikiano na mshikamano uwasukume kulinda na kutunza mazingira kwa kuongozwa na kanuni auni, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Familia ijifunze kurekebisha makosa yanayotendeka katika maisha na utume wake; jambo ambalo linahitaji kwamba kabisa: toba na wongofu wa ndani; msamaha na kila mwanafamilia kutambua kwamba ni zawadi kwa ajili ya jirani yake. Huu ndio mwelekeo unaopaswa kujenga ekolojia ya uhusiano wa kibinadamu na ekolojia ya mazingira. Wanafamilia wajifunze kurekebisha kinzani na misigano inayojitokeza, ili kujenga na kuimarisha udugu.

Watu washikamane kurekebisha madhara yanayotokana na maafa asilia; wasimame kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani, ili kwa pamoja kujenga Familia kubwa zaidi. Watu wajifunze kuguswa na shida pmoja na mahangaiko ya familia nyingine, ili kuwashirikisha upendo wa kigudu. Familia inaweza pia kutekeleza wajibu na dhamana yake barabara kwa kueshimu na kulinda ukuu na utakatifu wa Siku ya Bwana.

Hii ni Siku ya Mungu, Kristo, Kanisa na binadamu. Hapa Familia inajifunza kulinda na kutunza mazingira; inajifunza kusali na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia na vipaumbele vyao. Sadaka na majitoleo ya dhati yanaiwezesha familia kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wengine sanjari na ujenzi wa nyumba na familia zao.

Ujumbe huu umehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.