Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 22 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa
Ni Dominika nyingine tunakutana katika safari ya wokovu tukijaribu kusifu jina la
Bwana kwa njia ya tafakari ya Neno lake. Ni Dominika ya 22 ya mwaka C. Mama Kanisa
atupa chakula ndilo Neno la Bwana akisema Unyenyekevu ndiyo iwe dira ya maisha yetu
kwa ajili ya kujipatia zawadi yakushiriki maisha ya Kimungu na heri ya Watakatifuwa
mbinguni.
Mpendwa mwana wa Mungu Tukitaka kweli kuupata uzima wa milele ni
lazima kujijengea uadilifu na unyoofu wa moyo unaojitokeza katika unyenyekevu. Kunyenyekea
ni kutumaini yote katika Bwana aliye mkuu kuliko vitu vyote na kwamba katika yeye
kuna msamaha wa dhambi na hatimaye uzima wa milele. Baada ya kutekeleza jambo basi
mmoja lazima aingie katika kutenda kwa maana Mtakatifu Yakobo asema, imani bila matendo
ni bure. Ndiyo kusema kuhangaikia kundi la wasiojiweza, wasio na chakula, tuseme walio
ns shida mbalimbali katika maisha yao ambao kwa sababu hiyo mfumo jamii umewasukumiza
mbali.
Mpendwa msikilizaji katika Injili ya Dominika hii Bwana yuko katika
sherehe katika nyumba ya Mfarisayo mmoja ambaye amewaalika watu kadhaa kwa ajili ya
kusherehekea pamoja. Anatoa fundisho kuhusu unyenyekevu , fundisho hili linawalenga
watu wa aina mbili: mwenye sherehe na wale walioalikwa katika sherehe. Kwa mwenye
sherehe fundisho linagota bila kuchelewa akisema unapofanya sherehe ndugu yangu usiwaalike
wale ambao wanaweza pia kufanya kama ulivyofanya na hivi wakakualika! Bali waalikeni
wale ambao kwa namna yoyote hawataweza kufanya hivyo.
Jambo hili linagusa
mara moja maisha yetu, yaani mara kadhaa tumejenga urafiki na watu ambao kwa namna
fulani wanalipa kama wasemavyo vijana leo. Huu ni urafiki ambao umepimwa katika mantiki
ya kimahesabu, yaani nipe nikupe! Kwa namna hiyo tendo la kujitoa liko katika mmonyoko
kwa maana bila nipe hakuna msaada au tuseme upendo usiodai faida. Mfumo wa maisha
ya kikristu au maisha ya kawaida umeingiliwa na kirusi.
Wakati fulani kirusi
hiki huingia katika imani na hata kuweza kufikia kusema kuwa Mungu anatupa zawadi
mbalimbali kwa sababu tumefanya jambo fulani. Jambo hili lazima kulitazama kwa umakini,
Mungu si nipe nikupe bali ni upendo mkamilifu ambao hujitoa pasipo kutarajia malipo.
Mpendwa
msikilizaji sehemu ya pili ya fundisho la Bwana inaelekezwa kwa wale walioalikwa katika
sherehe. Bwana anaona kila mmoja anahangaika kujipatia nafasi ya mbele, kwa namna
yoyote katika mantiki ya kutaka kuonekana. Kila mmoja anaonesha ubinafsi wake katika
sherehe hiyo. Bwana anasema ni vema na vizuri kuchukua viti vya nyuma ili basi kama
unastahili utaalikwa kwa viti vya mbele.
Bwana hakemei kwa mtindo wa mauzi
bali anasema ni vema tukatambua kuwa wale wa kwanza watakuwa wa mwisho na wa mwisho
watakuwa wa kwanza. Wale wanaojishusha watakwezwa na vivyo hivyo kinyume chake. Kumbe
wajishushao wataweza kushiriki kile chakula cha ufalme wa mbinguni. Kwa hakika hiyo
sherehe yataka kuwakilisha sherehe ya uzima wa milele mbinguni.
Kwa ajili ya
kuingia katika chakula hicho yatudai unyenyekevu na hekima. Kama nitachagua viti vya
mbele maana yake tayari ninacho kila kitu katika utawala wangu na sihitaji tena msaada
wa mtu mwingine kwa hivi nitakuwa nimemaliza safari yangu hapahapa!
Nina
kila kitu katika maisha haya. Nikichagua njia ya kukaa nyuma maana yake basi mwenye
sherehe atanivuta na kunisogeza mahala pazuri kumbe kuna kupiga hatua zaidi. Haya
yanagusa yule mwalikwa. Kuhusu mwenye sherehe sharti ni moja kuwaalika wale wasiojiweza,
waliosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa ajili ya kujipatia tiketi ya kuweza kuingia
katika ufalme wa mbinguni.
Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa
kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.