Wakristo nchini Kenya wamehimizwa kuanza kupanda miti kwa matayarisho ya kuisheherekea
sikukuu ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi hapo tarehe 4 Oktoba 2013. Haya yamesemwa
hivi karibuni na Padre Hermann Borg.
Padre Borg aliashiria kuwa Mtakatifu
Francisko ni mfano bora kwa Wakristo popote duniani na akamsifu Baba Mtakatifu Francisko
kwa kumuenzi Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa kuchagua jina hili ambalo lina changamoto
nyingi katika: kusimama kidete kutetea misingi ya amani, utunzaji bora wa mazingira
na huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Padre
Borg amewahimiza watu binafsi na vikundi; jumuiya za akina mama, vijana pamoja na
wanafunzi kushirikiana kwa pamoja ili kupanda miti kwa wingi kwani ilikuwa ni fadhila
ya Mtakatifu Francisko kupenda, kuthamini na kuyatunza mazingira. Alizichangamotisha
jumuiya za watawa, shule, hospitali, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu kujiunga
kwenye zoezi hili makini ambalo linanuia kuzishirikisha Parokia zote kwenye majimbo
yote nchini Kenya kupanda miti kama njia ya kumuenzi Baba Mtakatifu Francisko kwa
vitendo!
Ili kuonyesha umoja na ushirikiano kwa ajili ya mafao ya wengi Padre
Borg anawaalika pia waamini wa dini zingine kushiriki kwenye zoezi hili la kupanda
miti ili kudumisha amani miongoni mwao, kwani ilikuwa sala kuu ya Mtakatifu Fransisko
kuona kila mwanadamu akiwa chombo cha amani.
Alisema ushirikiano wao utaimarisha
hata juhudi zao za pamoja kwa ajili ya kuiendeleza amani duniani kote, kwani dunia
ina uhitaji mkubwa wa umoja, amani, upendo na mshikamano na kwamba, Wakatoliki na
Wakenya wote kwa ujumla wao wanaweza kuwa chanzo cha amani hiyo kwa kuanzia na zoezi
la kupanda miti. Alinukuu mafanikio makubwa ya makundi yaliyokuwa ndoto ya mtu mmoja
au watu wachache na hatimaye, yakaweza kuwaunganisha watu wengi kutoka sehemu mbalimbali
za dunia.
Makundi haya, ambayo yangeweza kuigwa hata kwa zoezi la kumuenzi
Mtakatifu Fransisko wa Asisi hapo tarehe 4 Oktoba 2013 ni kama vile Green Belt Movement
ya hayati Prof. Wangari Maathai na mikutano mikuu miwili iliyofanyika nchini Kenya
mnamo 2007 ambayo ni ule wa Umoja wa Mataifa juu ya Mazingira na Jukwa la Masuala
ya Kijamii.