2013-08-27 10:52:22

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani nchini China!


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliutangaza na kuuzindua Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipochapisha Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki.

Lengo kuu la Mwaka huu ni kuwawezesha waamini kuifahamu kwa kina Imani wanayokiri; Imani inayoadhimishwa katika Sakramenti za Kanisa; hii ndiyo Imani inayopaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha adili yanayofumbata Amri Kumi za Mungu. Mwishoni, hii ni Imani ambayo inajidhihirisha kwa namna ya pekee katika maisha ya Sala inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, ili kujenga na kuimarisha uhusiano wa dhati na Mwenyezi Mungu.

Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Kardinali Zen Ze-kiun, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Hong Kong, China amekuwa akiendesha Katekesi za kina kama sehemu ya mchango wa ushuhuda wa imani yake kwa Kristo na Kanisa lake. Katekesi hizi kwa sasa zitasambazwa kwa njia ya DVD na CD kwa ajili ya matumizi ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini China.

Hizi ni Katekesi zilizokuwa zinahudhuriwa na umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema waliokuwa wanakiu ya kutaka kufahamu kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Amri za Mungu na Maisha ya Sala; mambo ambayo yamefafanuliwa kwa kina na mapana kwenye Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, utajiri na urithi mkubwa kutoka kwa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, Matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kama zilivyo Sheria za Kanisa. Katekesi hizi pia zimeanza kusambazwa kwa njia ya mitandao, ili kuwawezesha waamini walioko mbali zaidi kuweza kujitajirisha katika imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Zen Ze-kiun anasema, sehemu ya kwanza ya Katekesi hizi ambayo tayari inafanyiwa kazi ili kuwekwa kwenye DVD inagusia: Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Hii ni changamoto iliyoibuliwa na waamini waliotaka kufahamu kwa kina Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kwani hii ni sehemu ya majiundo endelevu.

Ni kweli waamini walipokuwa wanapokea Sakramenti mbali mbali za Kanisa walipewa mafundisho, lakini kuna haja ya kuanzisha mchakato wa majiundo endelevu, ili kuimarisha na kukomaza imani miongoni mwa waamini, tayari kuweza kuitolea ushuhuda katika maisha yao yak ila siku. Huu ndio umuhimu wa imani tendaji, changamoto inayotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Kardinali Zen Ze-kiun anasema Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican imekuwa ni fursa kubwa kwa waamini kujitajirisha kwa nyaraka mbali mbali zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Vyama vya kitume vimeendelea kutoa Katekesi maalum kuhusu utume na dhamana yao katika Kanisa na mwaliko wa kuendelea kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili. Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa hasa Ubatizo wakati wa Kipindi cha Pasaka, Kanisa linaendelea kukazia umuhimu wa majiundo makini kwa Wakatekumeni ili waweze kuifahamu imani watakayoiungama, adhimisha, ishi na kusali.

Mwaka wa Imani, kimekuwa ni kipindi cha kukuza na kuendeleza utume wa Biblia uliowahusisha Makleri, Watawa na Waamini walei ambao wamebobea katika Maandiko Matakatifu, yote haya yanalenga anasema Kardinali Zen Ze-kiun kuwaimarisha waamini katika hija ya maisha yao ya imani.

Alipokuwa mjini Vatican, alipata fursa ya kuzungumza na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kuhusu Katekesi za kina kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto alifurahishwa sana na jitihada hizi zinazolenga kuwaimarisha waamini katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili waweze kuwa tayari kuitolea ushuhuda.

Alipobahatika kuzungumza na Papa Francisko, alimwelezea pia mikakati ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani nchini China. Anasema, alikuwa anafahamiana kwa karibu na Kardinali Bergoglio kwani walikuwa ni wajumbe wa Tume ya Sinodi ya Ekaristi iliyokusanya matunda ya Sinodi hiyo na kwamba, walishiriki kwa pamoja kuandaa Sinodi zilizofuatia pamoja na kukutana mara kwa mara wakati wa mikutano elekezi ya Makardinali wakati wa “Conclave” iliyopita mjini Vatican.

Anasema Makardinali walipokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kumshukuru na kumuaga Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alibahatika kukaa karibu na Kardinali Berglio ambaye alimshirikisha maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini China. Kardinali Berglio alisikiliza kwa makini. Kardinali Zen Ze-kiun anasema, kwa hakika Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi anayetoa kipaumbele cha kwanza katika mikakati ya kichungaji na ana kipaji kikubwa cha kusikiliza kwa makini.








All the contents on this site are copyrighted ©.