2013-08-27 14:00:32

Jimbo Katoliki Mbeya lakabidhiwa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Wauguzi


Kama wasemavyo wahenga kuwa machozi ya mtu mzima hayaendi bure ndivyo ilivyotokea kwa Askofu Evaristus Marcus Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya kwa Serikali ya Mkoa wa Mbeya kuhusu ardhi ya Kijiji cha Lupata aliyoanza kuililia tangu mwaka 2009 kwa ajili ya kuwasaidia watanzania kwa kujenga Chuo cha Uuguzi na Uganga bila mafanikio, lakini kweli Mwenyezi Mungu hamtupi mja wake, hatimaye, kilio hicho kimesikika baada ya kukabidhiwa rasmi ardhi hiyo na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe.

Askofu amewahi kutoa kilio hicho kwa Serikali na kuhoji sababu ya kukwama kwa mchakato huo hata alidiriki kusema endapo ardhi hiyo ya Mungu imekuwa na mlolongo mkubwa kwa maneno yaliyozoeleka serikali kuwa ' mchakato' unaendelea basi itafika wakati Kanisa litahamishia ujenzi wa Chuo hicho cha Uuguzi na kupeleka maeneo mengine yenye kiu ya maendeleo endelevu.

Askofu Chengula alitoa kilio chake katika Jubilei ya 50 tangu kufunguliwa kwa Hospitali ya teule ya Wilaya ya Igogwe inayomilikiwa na Jimbo katoliki la Mbeya, ambapo mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa wilaya ya Rungwe Bwana Chrispin Meela. Alimhakikishia Askofu Chengula na kumwambia kwamba, atakipata kipande .

Akizungumza katika Jubilei hiyo Bwana Meela alisema baada ya kusikia mahubiri ya Askofu kutoa kilio chake kwa uchungu aliona ipo sababu ya kufanya haraka kufuatilia suala hilo na kulikamilisha na hivyo baada ya kupitia nyaraka za awali na kupata matokeo ya tume ya uchunguzi iliyoundwa na Katibu tawala wa Wilaya ya Rungwe aliamua kutoa ardhi kwa niaba ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ndiye mwenye ardhi kikatiba.

Alisema kazi yake kubwa kama Mkuu wa Wilaya ni kusimamia haki na sheria na kwamba katika suala la ardhi hiyo aliangalia taratibu zinasemaje na baadaye alichukuwa maamuzi baada ya kupima manufaa ya suala lenyewe kwa umma anayoiongoza.

"Nyaraka zilionesha kuna ubabaishaji mwingi kwa sababu taratibu zote za kutuma maombi zilifuatwa kuanzia ngazi ya Kijiji, nikaona Rungwe tuna upungufu wa wauguzi 128, nikaona Chuo kitakuwa mkombozi katika zahanati na vituo vya afya ambavyo vina upungufu mkubwa wa wataalamu kwa hiyo ninakukabidhi ramani hii Baba Askofu anzeni mara moja kujenga baada ya Desemba 22 watakapokuja watu wa upimaji na ahadi ya Watoto wa Kijiji hiki na Rungwe kwa ujumla kupewa kipaumbele usisahau,"alisema Mkuu wa Wilaya.

Hayawi hayawi yamekuwa ndivyo ulivyokamilika msemo huo hivi karibuni baada ya wakazi wa Kijiji cha Lukata Kata ya Kinyara,wilayani Rungwe kukabidhi rasmi ardhi yenye ukubwa wa ekari zaidi ya 5 kwa Askofu Chengula kwa ajili ya kujenga Chuo cha Wauguzi katika Hospitali Teule ya Igogwe inayomilikiwa na Jimbo Katoliki Mbeya

Tukio hilo limefanyika katika eneo lililopo jirani na Hospitali hiyo ambapo Katibu wa Hospitali Japhet Kalindu, Mganga Mkuu Dr. Oyeti Mwakosya na viongozi wa Chama na serikali wakiwemo machifu walihudhuria na kushuhudia makabidhiano hayo na kupita kuweka alama ya mipaka.

Ninakumbuka kauli ya Mkuu wa Wilaya wakati wa jubilei ya Hospitali hiyo alimwambia Askofu kuwa katika Wilaya yake anao mzigo mkubwa wa wanafunzi zaidi ya 4,000 kati ya 5,000 waliomaliza kidato cha nne mwaka jana ambao wapo wanazurula mitaani baada ya kuchaguliwa wanafunzi 800 kati yao kuendelea na kidato cha tano.

Awali Mganga Mkuu wa Hospitali ya Igogwe,Dkt.Mwakosya alisema chuo kinatarajia kuanza na wanafunzi 90 wa ngazi ya cheti kutokana na mipango ya serikali na wanatarajia kuendelea kutoa kozi za ngazi ya stashahada na shahada kwa wauguzi na kwamba ujenzi wa chuo ni faraja kwa Wilaya na Jimbo Katoliki la Mbeya.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa eneo hilo kwa niaba ya Askofu Chengula wa kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya ambaye ndiye mmiliki wa Hospitali ya Igogwe,Mganga mkuu Dkt. Mwakosya na Katibu wa afya,Kalindu waliwashukuru wananchi kwa kukubali kulitoa eneo hilo ambalo baada ya kuliomba lilizuwa mgogoro na hivyo kukwamisha mikakati ya ujenzi wa chuo cha uuguzi tangu mwaka ya 2009.

Hata hivyo baadhi ya viongozi,chifu mkuu na wananchi wa Kijiji cha Lukata wameelezea furaha yao huku Mratibu Elimu Kata ya Kinyala ambaye alikuwa anatuhumiwa kuwa miongoni mwa wananchi tisa wa Kijiji hicho waliokuwa wakipinga Hospitali ya Igogwe kugawiwa eneo hilo akitamka kuwa hana kinyongo na eneo hilo huku akiwatania wazee wa jadi wamlinde na hatari yeyote inayohusishwa na imani za kishirikina.








All the contents on this site are copyrighted ©.