2013-08-27 10:29:05

Cheche za Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jimbo kuu la Manila


Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila nchini Ufilippini anasema, Jimbo lake kwa sasa linajiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Kongamano la Kijimbo kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Kumbu kumbu kumbu ya Miaka 10 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili aliposchapisha kwa mara ya kwanza Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Huu ni muhtasari wa Imani, Sakramenti za Kanisa, Amri za Mungu na Maisha ya Sala.

Kardinali Tagle moja ya Makardinali wenye umri mdogo sana, ikilinganishwa na Makardinali wengine anasema kwamba, inasikitisha kuona kuwa, nchini Ufilippini ambako imani ya Kikristo ilikuwa imeota mizizi katika sakafu ya maisha ya waamini lakini leo hii, wamekengeuka na wanaanza kushikwa na ubaridi wa maisha ya kiroho.

Hii ndiyo hali ambayo inajitokeza kwa kasi kubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu hana tena nafasi katika maisha na vipaumbele vya watu. Hali hii imeenea sana kwa nchi za Ulaya na Amerika, lakini pole pole ubaridi wa maisha ya imani na maadili unaanza kupenya sehemu mbali mbali za dunia.

Idadi ya Wakristo nchini Ufilippini ilikuwa ni kubwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita, lakini kwa sasa hali inazidi kudidimia mwaka hadi mwaka, kwani idadi ya Wakatekumeni wanaobatizwa na Wakristo wanaofunga ndoa Kanisani inazidi kuongezeka kwa kasi ya kushangaza. Kwa miaka kadhaa sasa kuna baadhi ya wakristo hawauoni tena mlango wa Kanisa hasa katika Ibada za Jumapili na Siku kuu zilizo amriwa.

Baadhi yao wameamua kujiunga na Madhehebu mengine ya Kikristo wakitumainia kupata muujiza wao! Hizi ndizo changamoto ambazo Kanisa Katoliki nchini Ufilippini inakumbana nazo na sasa limeamua kuanza kuchemsha dawa inayofumbatwa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Dunia inaendelea kubadilika kwa kasi, lakini Neno la Mungu linabaki pale pale, ni jukumu la Kanisa kuendelea kuinjilisha ili hatimaye, Neno la Mungu liweze kuota mizizi katika maisha na vipaumbele vya waamini kwa kutoa majibu muafaka kwa changamoto mamboleo.

Kardinali Tagle anasema, kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 18 Oktoba, 2013 Jimbo kuu la Manila litaadhimisha Mwaka wa Imani, kama sehemu ya mchakato unaopania kuwahamasisha waamini kuonja tena ndani mwao ile furaha ya imani, ambayo wanapaswa kuikiri, kuiadhimisha, kuimwilisha katika maisha adili na kuisali. Kongamano hili linatarajiwa kupata wawakilishi kutoka katika nchi kadhaa za Asia. Huu ndio utakaokuwa mchango wa Kanisa Katoliki nchini Ufilippini katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, utakaohitimishwa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme.








All the contents on this site are copyrighted ©.