2013-08-27 10:44:07

Changamoto katika mawasiliano ya Jamii!


Mama Kanisa anahitaji kuibua mbinu, mikakati na sera mpya zaidi katika ulimwengu wa mawasiliano ya jamii ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa mawasiliano. Kanisa halina budi kutambua dhamana na nafasi yake katika Jamii husika, hii ndiyo changamoto iliyopo kwa sasa.

Ni maneno ya Monsinyo Paul Tighe, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii anapotafakari dhamana na utume wa Kanisa katika ulimwengu wa mitandao ya kijamii yenye fursa na changamoto zake. Mawasiliano hayana budi kuangaliwa katika mapana yake kiulimwengu, lakini ikumbukwe kwamba, yanagusa pia undani wa maisha ya watu mahalia.

Kanisa linapaswa kuibua mmbinu mkakati ambao utayasaidia Makanisa mahalia kuwepo kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya waamini na watu wao mahalia pamoja na kuendelea kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa la kiulimwengu. Dhana hii inahitaji majitoleo na ugunduzi utakaoiwezesha Injili kujikita katika mitandao ya kijamii, ili waamini na watu wenye mapenzi mema, waweze kushirikishana mang’amuzi ya kweli za Kiinjili.

Monsinyo Paul Tighe anasema, hizi kati ya mada zitakazojadiliwa na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Kijamii katika mkutano wake wa Mwaka unaotarajiwa kuanza hapo tarehe 19 hadi tarehe 21 Septemba 2013 hapa mjini Roma. Kanisa linaendelea kujifunza matumizi ya mitandao mipya ya kijamii kama ilivyojitokeza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani mjini Rio de Janeiro, Brazil. Njia hizi mpya pengine ni mpya kwa wale wanaoanza kuzitumia, lakini kwa vijana wa kizazi kipya, mitandao hii imekuwa ni sawa na maji kwa glasi.

Ni mitandao inayowashirikisha na kuwagusa watu wengi kwa pamoja, kiasi kwamba, hata wale wanaoishi pembezoni mwa Jamii wanaweza kupokea ujumbe huu pasi na mashaka. Ujumbe unaotolewa na Mama Kanisa katika mazingira kama haya hauna budi kuandaliwa kikamilifu ili kupata matunda yanayokusudiwa. Ni ujumbe unaotoka moja kwa moja kwa viongozi wa Kanisa ambao wakati mwingine inakuwa ni vigumu kupokelewa na wahusika katika maeneo yao, kwani hauwagusi moja kwa moja.

Monsinyo Paul Tighe anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ana lugha rahisi inayowagusa watu kwa haraka zaidi; ni kiongozi anayetumia vitendo kama ushuhuda wa kile anachozungumza. Maneno na matendo ni chanda na pete katika kuwasilisha ujumbe unaokusudiwa na hapa Baba Mtakatifu Francisko ameonesha umahiri mkubwa. Katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, Baraza la Kipapa la Mawasiliano lilitumia mbinu mbali mbali ili kuhakikisha kwamba, vijana wengi zaidi wanapata ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Mtandao wa Vatican unaendelea kuboreshwa zaidi kwani kwa sasa watumiaji wa mtandao huu wanaweza kupata: Gazeti la L’Osservatore Romano, Kusikiliza Radio Vatican na kuona picha zinazorushwa na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV pamoja na kujisomea nyaraka na makala mbali mbali kuhusu maisha na utume wa Kanisa. Sasa hivi nyaraka hizi zinawafikia watu wengi zaidi kwa njia ya mitandao ya kijamii na simu za viganjani.

Maelfu ya vijana wameweza kupata ujumbe wa Baba Mtakatifu wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa njia ya mitandao ya Kijamii na hasa zaidi kwa njia ya simu za kisasa. Huu ni ushirikiano wa dhati uliooneshwa na makampuni ya simu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Vijana wameshirikishana picha na ujumbe kwa njia ya simu na mitandao mingine ya kijamii kama vile twitter.

Monsinyo Paul Tighe anasema, wafuasi wa Baba Mtakatifu Francisko katika mtandao wake wa twitter wamefikia millioni nane, na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya viongozi mashuhuri duniani ambaye ujumbe wake unatafutwa ili kuwashirikisha wengine.

Huu ndio umuhimu wa kuwahusisha waamini kuwa ni wasambazaji wa ujumbe wa Baba Mtakatifu, lakini zaidi Injili ya Kristo kwa wajuani wao, ili kujenga jukwaa la majadiliano na ufahamu wa kina, ili kueneza Imani na kweli za Kiinjili kwa watu wenye kiu na njaa ya Neno la Mungu. Kwa njia hii, Kanisa linaweza kuonesha uwepo wake katika maisha ya watu kwa njia ya mitandao ya kijamii.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 yamekuwa ni kati ya matukio yaliyofuatiliwa na watu wengi zake kwa mwaka huu kadiri ya takwimu zilizotolewa na watumiaji mbali mbali wa mitandao.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake kwa Siku ya Upashanaji Habari Duniani kwa Mwaka 2013 aliwataka waamini kujishughulisha kikamilifu katika mchakato wa kuwamegea wengine: Imani na kweli za Kiinjili kwa njia ya uwepo wao kwenye mitandao ya Kijamii, ili kujadiliana na kushirikishana utamu na uzuri wa Injili.

Baraza la Kipapa la Mawasiliano, litatumia mkutano mkuu kujadili mafanikio na mapungufu yaliyojitokeza katika mawasiliano ili kujiwekea mbinu mkakati wa maboresho kwa siku zijazo. Ni fursa ya kuangalia changamoto na kiu inayooneshwa na watumiaji wa mitandao ya kijamii. Ni nafasi ya kusikiliza yale yaliyojadiliwa ili kugundua kwa namna ya pekee: matumaini, furaha na machungu yanayomsibu binadamu katika ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Hii inaonesha kwamba, kimsingi Kanisa linasikiliza na linapania kujenga jukwaa la majadiliano ili kutoa ushuhuda wa Kiinjili, ndivyo anavyohitimisha tafakari yake Monsinyo Paul Tighe, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii.
Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaaya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.