Somo la Injili : Mt 23:13-22. Tafakari
ya Jumatatu, tarehe 26 Agosti, 2013
Leo Bwana wetu Yesu Kristo anachagiza
uongozi wo wote katika jamii. Tabia ya uongozi mzuri wa watu ni kujiwekea utaratibu
wa kujipima utendaji wake. Kujiwekea nidhamu ngumu ya kujikosoa na kupokea kwa radhi
vipindi au wakati wa kukosolewa. Gwiji la falsafa ya Wagiriki aliyeishi miaka 500
kabla ya Kristo - Socrates aliwahi kusema, maisha yasiyotafakariwa au yasiyo na kujichunguza,
hayafai kuyaishi (unexamined life is unworthy living). Na kipimo sahihi cha kujipima
ni watu wetu, familia zetu, na wateja wetu.
Katika ofisi za serikali au
makampuni kuna mtindo wa kuweka masanduka ya maoni (suggestion boxes). Yesu naye alitumia
"suggestion box" alipokuwa na mitume wake Kaisarea Filipi (Mt 16:13-17), "..watu wanasema
mimi ni nani?" Tusipoweka utaratibu wa kupimwa, tutapimishwa na watu wetu kwa lazima.
Ingawa waswahili husema mtu mzima hagombwi - siku moja mtu mzima atatukanwa na anaowangoza
kama Yesu alivyofanya leo kwa Waandishi (Mt 23:16) "..ole wenu viongozi vipofu.."
Bwana
wetu Yesu Kristu anataka kutuambia nini leo :
1. Uongozi wo wote ule ni dhamana
tuliyoichukua kutoka kwa Mungu na kwa watu tunaowaongoza. Daima waongozwa wanahitaji
na wana matarajio ya kupata nafuu, hauweni, uzima tele (Yoh 10:10), huruma na msamaha.
kutoka kwa uongozi wanataka kuonja kutetewa na kujaliwa. Yule anayeongozwa hujiweka
chini kwa anayemuongoza kama kondoo au mtoto. Na ndio maana Mungu kwa kinywa cha nabii
Ezekieli anasema, "mimi mwenyewe nitawachunga kondoo zangu.."(Ezek. 34:11-16). Jicho
la kiongozi ni kujipima kama kweli unavyoongoza watu wako wanaonja unafuu katika maisha
yao.
Baba au mama katika familia yako jipime mwisho wa wiki au mwezi - je watoto
wangu wanajisikiaje wakiwa nami? Je, sipeleki ila sura ya ujemedari wangu wa jeshi
(kama baba ni askari) kwa watoto wangu na mke wangu nyumbani? Hata kama wewe ni Brigedia
jeshini - unaporudi nyumbani vya sura ya ubaba kwa na watoto wako. Watoto waseme toka
moyoni "baba yetu.."na sio brigedia fulani.
2. Viongozi wakae na watu wao na
wawasilize. Viongozi waonje shida zao, matatizo yao, hofu zao. Kiongozi mzuri ni msikivu
wa daima, azijua sauti za kondoo wake. "..Kondoo husikia sauti yake, naye huwaita
kondoo wake kila mmoja kwa jina lake.." (Yoh 10:3). Daima maamuzi mengi tunafanya
kimakosa kwa kujisikiliza sisi wenyewe. Tunakuwa na mtindo wa "top bottom approach"
katika Uongozi wetu. Tukumbuke daima tunaozeka nyumba ya nyasi, daima wale walio chini
huona matundu mengi hivyo umsaidia mwezekaji nyumba kuifanya kazi yake vizuri.
Kwa
kuwa kila mmoja wetu ni kiongozi kwa nafasi yake, tujiombee Jumatatu hii Roho wa Mungu
atuumbe upya ili ndani ya familia zetu, jumuiya, parokia na kazi zetu tupate viongozi
wa mfano wa Kristu mwenyewe.
Mtumishi wenu – Padre Benno Michael Kikudo Jimbo
kuu la Dar es Salaam.