2013-08-26 09:45:25

Ujumbe kwa Siku ya Utalii kwa Mwaka 2013


Jumuiya ya Kimataifa hapo tarehe 27 Septemba 2013 itaadhimisha Siku ya Utalii Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Utalii na Maji: Utunzaji wa mafao yetu kwa siku za usoni”. Mada hii inakwenda sanjari na mikakati ya Umoja wa Mataifa uliotangaza Mwaka wa ushirikiano kimataifa katika sekta ya maji. RealAudioMP3

Itakumbukwa kwamba, Umoja wa Mataifa ulitangaza Mwaka 2005 hadi Mwaka 2015 kuwa ni Kipindi cha Maji ni Uhai, kwa kutambua umuhimu wa maji katika mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu, hasa katika mchakato wa kupambana na umaskini na baa la njaa duniani. Maji ni muhimu sana katika ustawi na maisha ya binadamu na ni msingi wa mafanikio ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015.

Baraza la Kipapa na shughuli za kichungaji kwa ajili ya Wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani kwa Mwaka 2013 linasema kwamba, Vatican inapenda kuchangia katika Maadhimisho haya kwa kushirikisha mang’amuzi na vipaumbele katika sekta ya Utalii na changamoto na fursa zake katika azma ya Uinjilishaji. Sekta ya Utalii ni kati ya sekta zinazokuwa kwa haraka na zinachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa kimataifa na kitaifa.

Maji ni muhimu sana katika Sekta ya Utalii, kama rasilimali na chanzo cha mapato. Ni rasilimali kwani inamvuto na mashiko kwa watu wengi, kwani kuna mamillioni ya watalii wanaopenda kufurahia maisha kwenye maji yaani kwenye fukwe za bahari, maporomoko asilia, visiwani, milimani kwenye barafu na sehemu ambazo zina mvuto kutokana na uwepo wa maji. Maji ni chanzo cha mapato katika maeneo mengi ya kitalii.

Sekta ya Utalii inaweza kuwa na mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya watu ikiwa kama vyanzo vya maji vitaheshimiwa na kutunzwa mikakati ya uchumi wa kijani na utunzaji bora wa mazingira. Jumuiya ya Kimataifa inaalikwa kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, inaendeleza Utalii endelevu na rafiki kwa mazingira, utalii ambao utachangia upatikanaji wa fursa za ajira, uchumi mahalia pamoja na kupunguza balaa la umaskini. Sekta ya Utalii ijikite katika utunzaji bora wa mazingira kwa kusaidia kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaofanywa na watalii wasiowajibika.

Maji ni muhimu sana kwa maendeleo na maisha ya binadamu. Lakini kuna idadi kubwa sana ya watu wanaoishi katika maeneo ambayo yana uhaba mkubwa sana wa maji. Inakadiriwa kwamba, ifikapo mwaka 2030, nusu ya idadi ya watu duniani itakuwa inaathirika kwa uhaba wa maji, kutokana na ukweli kwamba, uhitaji wa maji utakuwa umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 40%. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu Billioni moja ambao hawana maji safi na salama.

Changamoto hii inatarajiwa kuongezeka maradufu kwa siku za usoni kutokana na ugavi mbovu; upotevu na uchafuzi wa maji na vyanzo vyake, matumizi haramu ya maji au kutokuwa na vipimo sahihi vya vipaumbele vya matumizi ya maji, bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Wakati mwingine, Sekta ya Utalii imekuwa ikishindania matumizi ya maji na sekta nyingine katika uchumi, kiasi kwamba, wakati mwingine kuna matumizi mabaya ya maji wakati ambapo wananchi wanaozunguka katika maeneo ya kitalii wanataabika kwa kukosa huduma bora ya maji.

Baraza la Kipapa la Shughuli za Kichungaji kwa Wakimbizi na Watu wasiokuwa na makazi maalum katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani linaendelea kusema kwamba, utunzaji makini na endelevu wa maji ni changamoto katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kimazingira kwa kuzingatia kanuni maadili kwani maji ni kwa ajili ya mafao ya wengi, kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kulinda na kutunza maji na vyanzo vyake, kwani hii ni zawadi ya Uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu kuitunza na kuiendeleza.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, uharibifu wa mazingira unaweza kusababisha maafa makubwa kwa jamii ya watu. Ubinafsi, uroho wa utajiri wa haraka haraka ni kati ya mambo yanayopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira, badala ya kuwa ni kito cha thamani kinachopaswa kulindwa na kuendelezwa. Kwa mwelekeo kama huu, binadamu anakosa kipaji cha kushangaa, kutafakari na kusikiliza kazi ya Uumbaji.

Kanisa Katoliki katika Ibada zake mbali mbali zinashuhudia utukufu wa Mungu unaojionesha katika zawadi ya maji inayotumika katika Sakramenti ya Ubatizo. Maji yanaonesha pia wema wa Mungu katika kazi ya Uumbaji na Ukombozi, inayoendelezwa na Mama Kanisa katika nyakati hizi katika mchakato wa kumwondolea mwanadamu dhambi na uchafu wake wote kwa kujipatanisha na kuonja huruma na upendo wa Yesu Kristo kwa njia ya Sakramenti za Kanisa.

Kristo ni maji ya uzima yanayozima kiu ya mwanadamu, ni chanzo cha maji yenye uhai. Kutokana na umuhimu wa maji kwa maisha na maendeleo ya wengi, Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza wale wote wanaohusika na matumizi ya maji, kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana hii kwa uaminifu na uadilifu mkubwa, kwa kutambua kwamba, maji ni kwa ajili ya mafao ya wengi kwa sasa na kwa ajili ya kizazi kijacho.

Wanasiasa, wadau na wawekezaji katika sekta ya maji watambue changamoto zilizoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwa makini na masuala ya maji na wajizatiti kuweka sera na mikakati inayopania kuendeleza mafao ya wengi. Watu wajijengee mtindo mpya wa maisha kwa kuongozwa na nidhamu binafsi. Watalii wawajibike katika utunzaji bora wa maji na vyanzo vyake. Jamii ielimishwe kuhusu umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa matumizi sahihi ya maji; wajiepushe na uchafuzi wa maji na vyanzo vyake na waoneshe kwamba, wanathamini maji kama chemchemi ya uhai na maendeleo endelevu ya binadamu.

Utunzaji bora wa mazingira anasema Baba Mtakatifu Francisko ni mwanzo wa ujenzi wa utamaduni wa mshikamano na uwajibikaji wa pamoja. Jumuiya ya Kimataifa katika Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani ijumuike kwa pamoja kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kama alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Hivi ndivyo Baraza la Kipapa la Shughuli za Kichungaji kwa ajili ya Wakimbizi na Watu wasiokuwa na makazi linavyohitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Utalii Duniani kwa Mwaka 2013. Ujumbe ambao umetiwa mkwaju na kardinali Antonio Maria Vegliò na Askofu mkuu Joseph Kalathiparambil, Rais na katibu wa Baraza hili la Kipapa.

Ujumbe huu umehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.