2013-08-26 10:59:31

Mungu ameteua viumbe dhaifu na kuvifanya kuwa ni vyombo vya baraka yake!


Watumishi wa Mwenyezi Mungu na wote waliowekwa wakfu kwa namna ya pekee, hawapokei tunu hizi kwa mastahili yao wenyewe bali kwa upendo na huruma ya Mwenyezi Mungu.
Bwana huteua viumbe vilivyo dhaifu, anavijaza baraka na kuvifanya kuwa vyombo vya baraka yake. Hivi ndivyo anavyoita vijana na kuwafanya makuhani ili wawe baraka katika jamii wanamotumikia.
Haya yamesemwa na Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, katika adhimisho la Misa Takatifu katika kumbukumbu ya Mtakatifu Dominiko Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Sumve-Mwanza. Katika adhimisho hilo Askofu Ruwa’ichi alimpatia Daraja ya Upadre Shemasi Bernadin Mtula wa Parokia ya Sumve.
Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi anasema, Kristo anawashirikisha mapadri ukuhani, ufalme na unabii wake ili wawe mashahidi wake wakuu. kama vile Baba wa Imani Ibrahimu alivyoitwa na Mwenyezi Mungu kuhama nchi yake kuelekea anakoongozwa na Mungu na kufanywa kuwa chombo cha baraka, ndivyo makuhani wanavyoalikwa kuhama maisha ya kawaida na kuwa vyombo vya baraka kwa watu na vitu. Watu hawa wanapofanywa kuwa vyombo vya baraka katika Daraja Takatifu, basi wana wa Mungu wawe makini wasiwadharau, wasiwabeze, wala kuwalaani bali wawaheshimu na kwenda kuchota baraka kwao. Maana Bwana asema “atakayekulaani atalaaniwa na atakayekubariki atabarikiwa”. Maneno hayo kwa Ibrahim ni maneno yenye thamani ile ile kwa makuhani wa Bwana.
Nao makuhani wawe tayari kutoa maisha yao katika kueneza baraka ya Bwana kwa watu na vitu. Maana kama vile watu wanavyomsonga Kristo sababu ya njaa na kiu ya ukweli na haki, ndivyo leo Familia ya Mungu ina njaa na kiu ya mambo mengi na wanahitaji kuhudumiwa ndani ya Kristo. hata hivyo Askofu Mkuu Ruwa’ichi, ametoa angalisho kwa waamini wote kuwa makini juu ya kiu na njaa walizonazo.
Kwani wapo wenye kutambua vema wanatafutia wapi pa kupozea njaa na kiu yao, yaani kwa Kristo hata kama ni kwa kupapasa papasa. Wapo wanaotafuta au kupapasa yasiyostahili. Amewaalika waambatane na Kristo wakiongozwa na wachungaji wao katika kupapasa papasa mahali panapostahili.
Kristo anaingia ndani ya mtumbwi wa Petro na kumuamuru Petro kuendelea na uvuvi kwa namna ambayo Kristo mwenyewe anamuagiza naye anatii. Mtumbwi huu unawakilisha Kanisa zima, unawakilisha Familia ya wana wa Mungu na unawakilisha nafsi ya Petro na hivyo nafsi ya kila mwana wa Mungu. Kristo anaingia katika nafsi ya kila muumini, katika mpangilio wa maisha na vipaumbele vya kila mmoja ili atoe maelekezo sahihi ya kuboresha maisha na Imani.
Kristo anaingia katika nafsi, vipaumbele na mipangilio ya Padre, anamgeuza na kumfanya kuwa chombo chake cha baraka, anamfanya kuwa Alter Christi, Kristo mwingine. Naye Padre anaalikwa kujibu kwa uhuru, ukunjufu, uradhi na ukarimu. Kristo anamuagiza Padre atweke mpaka kilindini, yaani Padre azame katika Imani, uadilifu, Upendo, matumaini, katika vilindi vya mazingira anamotendea utume wake. Padre anaalikwa kuinjilisha mahusiano, mazingira ya mahali pa kuishi, mahali pa kazi, katika familia, taifa na ulimwengu.
kama Kristo anavyotoa maisha yake kwa ajili ya ulimwengu, ndivyo Padre mpya Bernadin Mtula anaalikwa kutoa maisha yake kwa ajili ya wale atakaowatumikia. Ndio maana yakugeuzwa na kufanywa Alter Christi, kristu mwingine. Padre Bernadin Mtula kaalikwa kuzingatia zama hizi za utandawazi katika utume wake. Atweke mpaka vilindini katika kufahamu vema na kuinjilisha jamii inayoelekea kuhadaiwa na utandawazi. Kahimizwa kuzama katika Neno la Mungu na Sakramenti Takatifu, akishikamana na Kristo na bila kukubali kuyumba, awe thabiti.
Hata leo Kanisa linahitaji watetezi na wafafanuzi wa Imani, anasema Askofu Mkuu Ruwa’ichi, hivyo pamoja na Mtakatifu Bernadin somo wake Padre mpya, amchukue pia Mtakatifu Dominiko awe mfano katika utume wake.
Padre Bernard Mtula alizaliwa 20/05/1981 katika kitongoji cha Sumve, wilaya ya kwimba jijini Mwanza, na wazazi Epimack Kamuli Kisusi na Fauster Kabula Manyasa akiwa mtoto wa saba kati ya watoto tisa. Alibatizwa 9/08/1981, parokiani Sumve. Malezi na majiundo ya Upadri alipatia katika Seminari kuu ya Kibosho kwa masomo ya Falsafa (2005-2008) na katika Seminari kuu ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala, Tabora kwa masomo ya Taalimungu (2005-2012). Alipewa Daraja ya Ushemasi 25/01/2013, siku kuu ya kuongoka kwa Mtume Paulo, katika seminari ndogo ya Mt. Maria, Nyegezi.
Radio Vatikani inamuombea kheri, mafanikio na baraka katika utume wa
Na. Pd. Celestin Nyanda
Jimbo kuu la Mwanza.








All the contents on this site are copyrighted ©.