2013-08-26 10:48:42

Changamkieni Uinjilishaji wa kina kwa furaha na unyofu wa moyo!


Pamoja na kwamba wanadamu hawana mazoea sana ya kuchangamkia na kufanikisha mambo ya wengine, Mapadri wachangamkie kwa furaha na unyoofu uinjilishaji kama vile Yohane Mbatizaji alivyomshabikia Kristo na kuwatambulisha wanafunzi wake kwa Kristo.
Hayo ameyasema Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Mwanza, mwishoni mwa Juma, katika adhimisho la Misa Takatifu katika Parokia ya Mtakatifu Kizito Kabila, Jimbo kuu la Mwanza, ambapo alitoa daraja takatifu la Upadre kwa Shemasi Peter Madata.
Padri Peter Madata ameonesha nia yake dhahiri na kwa uhuru ili kumtumikia Mungu katika ukuhani wa huduma. Askofu Mkuu Ruwa’ichi kamualika azingatie nia yake hiyo pamoja na masharti yanayoambatana na maisha ya Upadri. Masharti hayo ni pamoja na useja. Amemuonya kuwa makini na walimwengu wanaoshabikia kuwa useja ni uvunjifu wa haki za binadamu na uonevu, na badala yake atambue kuwa Useja ni kukumbatia Kanisa na kudhihirisha Ubaba wa Padri kwa wana Kanisa, amesema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Masharti hayo ni pamoja na maisha ya ufukara, kutokujilimbikizia mali, hivyo Padri mpya Peter Madata kaalikwa kuwa mtiifu na kuhudumia vema na kwa moyo wa ukarimu popote atakapotumwa hata mahali anapodhani kuwa hakuna mshiko wa kutosha wala mnuso wa kuridhisha. Akiwa mwaminifu na mwadilifu hatakuwa tajiri lakini pia hatapungukiwa chochote, hivyo ajitose zaidi katika kulijenga Kanisa la Kristo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi anawaalika mapadri wote kuvaa silaha za kimungu katika utume wao: ukweli wa kauli na ukweli wa nafsi uwakoleze mapadri na kuwaongoza; watende haki kwa kumpa kila mmoja anachostahili ikiwa ni pamoja na kuzingatia kuwahi katika maadhimisho; wawe na bidii ya utume kwa ukunjufu na ukomavu; Neno la uzima walitafakari, waliishi na kulifundisha na hivyo, wasijiridhishe na mambo ya kijiweni na udaku; wajikite katika sala ili Mungu abariki, aongoze, asindikize na kufanikisha mipango yao na kila wafanyacho.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi amemwalika Padri Peter Madata aambatane na Bikira Maria katika utume wake kwa kumtambua kuwa ni Mama yake na mama wa Kanisa. Kawaalika pia wanajimbo wote kuziombea parokia zote za Jimbo kuu la Mwanza zizidi kuzaa na kulea miito mitakatifu.

Na Padre Agapito Mhando.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.