Waamini wanafunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani!
Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Tunisia, Jumapili tarehe 25 Agosti 2013
inasali kwa ajili ya kuombea amani, umoja na mshikamano wa kitaifa kwa nchi za Kiarabu
ambazo kwa siku za hivi karibuni zimekumbwa na vita pamoja na machafuko ya kisiasa
na kijamii, kiasi cha kusababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa watu wasiokuwa
na hatia.
Askofu mkuu Ilario Antoniazzi wa Jimbo kuu la Tunis, nchini Tunisia
anasema kwamba, Kanisa linaendelea kufuatlia matukio ya ukosefu wa misingi ya haki,
amani na mshikamano huko Mashariki ya Kati, kwenye nchi za Kiafrika na Kiarabu. Waamini
wanapenda kutumia Jumapili kwa ajili ya kumpigia Mungu magoti ili kumlilia aweze kuwajalia
tena zawadi ya amani, utulivu na mshikamano wote wanaoendelea kuteseka kutokana na
vita.
Hii itakuwa ni siku ya kufunga na sala na kwamba, ni siku maalum iliyotengwa
kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwafariji wote wanaoteseka kutokana na vita. Ni matumaini
ya Kanisa Katoliki nchini Tunisia kwamba, kwa maombezi ya Bikira Maria Malkia wa amani,
Mwenyezi Mungu ataweza kuwasikiliza na kuwasaidia katika mchakato wa kutafuta amani
ya kudumu sehemu mbali mbali za dunia.