Ujumbe kwa Maadhimisho ya Siku ya 87 ya Kimissionari Duniani 2013
Baba Mtakatifu Francisko ameandika ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya 87 ya
Kimissionari Duniani, inayoadhimishwa tarehe 20 Oktoba 2013. Itakumbukwa kwamba,
kwa mara ya kwanza Siku hii iliadhimishwa kunako mwaka 1927 baada ya Papa Pio wa Kumi
na moja kuridhia ombi lililokuwa limetolewa na Taasisi ya Uenezaji wa Imani.
Ikaamriwa
kwamba, kila Mwaka, Jumapili ya Mwisho wa Mwezi Oktoba, itumike kwa ajili ya kuhamasisha
shughuli na mikakati ya kimissionari ndani ya Kanisa Katoliki, ili waamini waweze
kutambua na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa maisha na utume wa Kanisa kwa
kuchangia kwa hali na mali, kama kielelezo cha mshikamano wa kidugu na Makanisa mahalia
ambayo yalikuwa yanaanza kupokea Ujumbe wa Habari Njema.
Ni siku ambayo inatumika
kukusanya mchango kwa ajili ya kufadhili miradi na shughuli za kichungaji kwa ajili
ya kuwaendeleza: Makleri, Watawa na Makatekista, ambao kimsingi ni wadau wakuu wa
shughuli za Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Baba
Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya 87 ya Kimissionari
Duniani anasema, Maadhimisho haya yanafanyika wakati huu Mama Kanisa anapokaribia
kufunga Mwaka wa Imani, ambao umekuwa ni fursa makini kwa ajili ya kuimarisha urafiki
na Kristo katika hija ya maisha ya Kanisa kwa kutangaza kwa ari, nguvu na ujasiri
mkuu Injili ya Kristo.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu anapenda
kuangalisha mambo makuu manne: Imani ni zawadi yenye thamani kubwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu; Mwaka wa Imani, Vikwazo vya Uinjilishaji ndani ya Kanisa; Uinjilishaji kwa
njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii na mwishoni himizo kwa kila mwamini kuwa ni
mdau wa mchakato wa Uinjilishaji mpya.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Imani
ni zawadi yenye thamani kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwezesha mwamini kufungua
akili na moyo wake, ili kumfahamu na kumpenda Mwenyezi Mungu, ili kujenga uhusiano
wa dhati na hatimaye, kushiriki katika maisha ya Kimungu. Mwenyezi Mungu anawapenda
watu wake, lakini anahitaji jibu makini na ujasiri wa imani, unaomwezesha mwamini
kumwilisha pendo na kuonja huruma yake isiyokuwa na kifani.
Ni zawadi inayotolewa
kwa wote, mwaliko kwa kila mtu kujisikia kwamba, anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi
Mungu, kwani hii ndiyo furaha ya wokovu. Ni zawadi shirikishi inayowachangamotisha
waamini kuendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu, ili mataifa waweze kuwa ni wanafunzi
wa Yesu, kielelezo makini cha ukomavu wa Jumuiya ya Kikanisa.
Baba Mtakatifu
Francisko anasema, kila Jumuiya ina ukomavu kwani inakiri imani, inaadhimisha Liturujia
kwa furaha, inaishi fadhila ya upendo na kutangaza Neno la Mungu bila kuchoka hadi
pembezoni mwa Jamii, hususan kwa wale ambao bado hawajabahatika kumfahamu Kristo.
Uthabiti wa imani katika ngazi ya mtu binafsi na Kijumuiya unajionesha katika uwezo
wa kuieneza na kuwatangazia wengine; unamwilishwa katika mapendo, unashuhudiwa kwa
wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao.
Baba Mtakatifu Francisko katika
tafakari yake kuhusu Mwaka wa Imani anasema, Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa
Pili wa Vatican ni fursa makini kwa waamini kutambua kwa mara nyingine tena uwepo
wa Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo na utume wake kwa watu na mataifa. Umissionari
ni dhamana inayowaunganisha watu kutoka katika kila kabila, tamaduni na kila mwamini
mmoja mmoja, kwani mipaka ya imani inapenya katika tamaduni na mioyo ya watu.
Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican umebainisha kwa kina umuhimu wa kupanua mipaka ya imani kwa
kila mbatizwa na kwa kila Jumuiya ya Kikristo ili kila mtu aweze kutolea ushuhuda
wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Ni wajibu wa kila Jumuiya kutafsiri wajibu huu
kwa kuendelea kuwa ni wafuasi wa Kristo wakimshuhudia Kristo kwa watu wa mataifa kama
kiini na utambulisho wao wa Kikristo. Waamini wote wanatumwa na Kristo kufanya hija
pamoja na ndugu wengine, kwa kuungama na kushuhudia imani kwa Kristo na hivyo kuwa
kweli ni watangazaji wa Injili.
Baba Mtakatifu anaialika Familia ya Mungu kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa ari na moyo wa Kimissionari inayopaswa kujionesha kwa namna
ya pekee katika mikakati ya shughuli za kichungaji na malezi endelevu kwa kutambua
kwamba, wajibu huu unakamilika kwa njia ya ushuhuda kwa Kristo mbele ya Mataifa na
watu wote. Umissionari unagusa undani wa utume na maisha ya kila Mkristo.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema kwamba, wakati mwingine shughuli za Uinjilishaji zinapata
vikwazo kutoka ndani ya Kanisa lenyewe: waamini wanakosa ari, furaha, ujasiri na matumaini
ya kutangaza kwa wengi Ujumbe wa Injili ya Kristo pamoja na kusaidia kurahisisha mchakato
wa watu wanaotaka kukutana na Yesu katika ulimwengu mamboleo. Dhana hii inapingana
na matumizi ya nguvu kama njia ya kutangaza Injili ya Kristo, bali kutangaza kweli
za Kiinjili na wokovu wa Kristo katika ukweli na uwazi pamoja na kuheshimu mawazo
ya wengine.
Waamini wanachangamotishwa kuwa na ujasiri wa kuwashirikisha wengine
furaha ya kukutana na Yesu kwa heshima, huku wakitambua kwamba, wao ni vyombo vya
Injili. Yesu anaonesha njia na dhamana hii amewakabidhi wafuasi wake ili kuowaonesha
wengine dira na njia ya kufuata sanjari na kuendelea kutangaza Injili hadi miisho
ya dunia. Inasikitisha kuona kwamba, ukweli huu unachafuliwa kwa kukuza zaidi uhalifu
na kashfa.
Umefika wakati kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatolea ushuhuda
wa maisha adili ya Injili, kwa kuitangaza na kuishuhudia kwanza kabisa ndani ya Kanisa,
kwa kutambua kwamba, haiwezekani kutangaza Injili ya Kristo pasi na Kanisa na kwamba,
huu ni utume wa Familia nzima ya Mungu. Maadhimisho ya Liturujia, Neno la Mungu na
Sakramenti zote hata katika maisha ya binafsi ni mchakato unaolishirikisha Kanisa
zima kwa niaba ya Yesu mwenyewe. Hii ndiyo nguvu ya Kimissionari kwamba, Wamissionari
kamwe wasijisikie wapweke, kwani wao ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Yesu, yaani Kanisa
linaloongozwa na Roho Mtakatifu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba,
Waamini wanaishi katika ulimwengu wenye maendeleo makubwa ya vyombo vya mawasiliano
ya Jamii vinavyorahisisha mchakato wa watu kuweza kukutana, kufahamiana na kushirikishana
mang’amuzi; kuna mwingiliano mkubwa; watu wana fursa ya kushirikishana taaluma na
mang’amuzi yao ya kitamaduni; utalii ni jambo jingine linalowasukuma watu kutembelea
sehemu mbali mbali za dunia.
Licha ya maendeleo yote haya, wakati mwingine
inakuwa ni vigumu kwa waamini kuweza kufahamiana, hali inaonesha kwamba, kuna idadi
ya waamini wanaoendelea kupoteza imani yao; watu wasiojali au wanaovutika kwa urahisi
na dini za watu wengine; wengine wameasi kabisa kiasi kwamba, kuna haja ya Uinjilishaji
Mpya. Kuna idadi kubwa ya watu ambao bado hawajabahatika kusikia Habari Njema ya Wokovu.
Ulimwengu unaendelea kushuhudia athari za myumbo wa uchumi kimataifa unaojionesha
katika masuala ya fedha, uhakika na usalama wa chakula; mazingira, bila kusahau tunu
msingi za maisha.
Maisha ya watu wengi yanaendelea kukabiliana na kinzani,
hali inayosababisha ukosefu wa amani na usalama, changamoto ya kuendelea kutangaza
kwa ari na ujasiri mkubwa ujumbe wa matumaini, upatanisho, umoja, ukaribu na huruma
ya Mungu; wokovu pamoja na nguvu ya upendo wa Mungu kwa waja wake inayoweza kuvunjilia
mbali nguvu za giza na hatimaye, kumwongoza mwanadamu katika kutafuta mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya 87
ya Kimissionari Duniani kwa Mwaka 2013 anasema, mwanadamu anahitaji kutembea katika
mwanga unaopatikana kwa kukutana na Yesu Kristo, changamoto kwa waamini kushuhudia
mwanga huu kwa njia ya upendo na matumaini yanayobubujika kutoka katika imani.
Umissionari
wa Kanisa ni ushuhuda wa maisha yanayoangazia njia inayowajalia watu matumaini na
mapendo. Kanisa ni Jumuiya ya waamini wanaohamasishwa na nguvu ya Roho Mtakatifu ili
kuishi na kuonja ile ladha ya maisha ya kukutana na Yesu Kristo, ili hatimaye, kuwashirikisha
wengine mang’amuzi na furaha ya ndani ya Ujumbe wa Wokovu ulioletwa na Kristo. Roho
Mtakatifu analiongoza Kanisa katika safari hii.
Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza
waamini wote kuwa ni wadau wakuu wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu, lakini kwa
namna ya pekee: Wamissionari wa zawadi ya imani, watawa na waamini walei wanaojitosa
kimasomaso kwa ajili ya kutangaza Injili katika tamaduni na nchi tofauti. Anayashukuru
Makanisa mahalia kwa mchango wao katika azma ya Uinjilishaji mpya kwa kuonesha ari
na mwamko mpya wa Injili kwa Makanisa ya zamani. Ni utajiri mkubwa kwa kila Kanisa
na Jumuiya kutoa Wamissionari, watambue kwamba, si kwamba, wanapoteza bali wanafaidika
zaidi.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Maaskofu na Mashirika ya Kitawa
na Kazi za Kitume kuwa makini katika wito wa kimissionari kwa watu wa mataifa kwa
kusaidia Makanisa mahalia ambayo yana upungufu mkubwa wa Mapadre, ili kuimarisha utume
na maisha ya Jumuiya ya Kikristo. Jukumu hili pia lishughulikiwe na Mabaraza ya Maaskofu
Katoliki katika maeneo husika. Makanisa yaliyobahatika kuwa na utajiri mkubwa wa miito
ya Kipadre na Kitawa yawe tayari kusaidia Makanisa ambayo yanaonesha ukata wa wahudumu
wa Injili.
Wamissionari wajitahidi kuishi ile furaha ya kutoa huduma kwa Kanisa
mahalia wanapotangaza imani na kuleta mwamko na ari kubwa zaidi kwa Makanisa mahalia
kama njia ya kushirikisha imani kwa kuwawezesha wafuasi wa Kristo kutajirishana. Baba
Mtakatifu anapongeza shughuli na mikakati inayotekelezwa na Mashirika ya kimissionari
yanayohamasisha shughuli za kimissionari sehemu mbali mbali za dunia, kuendeleza dhamana
hii katika majiundo ya waamini na Jumuiya zao, kwa kutambua pia umuhimu wa majiundo
ya kimissionari kwa Familia ya Mungu. Jumuiya za Wakristo zioneshe moyo wa ukarimu
na upendo kwa kujitoa kwa hali na mali katika kusaidia mikakati ya Uinjilishaji.
Baba
Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya 87 ya Kimissionari Duniani
kwa kuwakumbuka waamini wanaokumbana na mateso na madhulumu ya kidini sehemu mbali
mbali za dunia, wasikate tamaa, bali Jumuiya ya Kimataifa ijitahidi kuhakikisha kwamba,
hata wao wanapata haki msingi na uhuru wa kuabudu. Hawa ni mashahidi na wafia dini
wa nyakati hizi, Mama Kanisa anatambua na kuthamini mchango wao. Baba Mtakatifu anawasihi
waendelee kuwa waaminifu kwa Kristo naye anawasindikiza kwa sala na sadaka yake, watambue
kwamba, Kristo ameushinda ulimwengu.
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani iwe ni fursa
ya kuimarisha urafiki na Kristo kwa kuwa na matumaini ya pendo kuu na endelevu kutoka
kwa Kristo. Baba Mtakatifu Francisko anawatakia kheri na baraka Wamissionari wote
wanaojitosa kwa ajili ya kutekeleza dhamana ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu
hadi miisho ya dunia, waonje furaha ya kutangaza Injili ya Kristo.
Ujumbe
huu umehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.