Monsinyo Joseph Kyeyune aliyekuwa na umri wa miaka 97 na alikuwa anajiandaa kuadhimisha
Miaka 67 ya Upadre, hivi karibuni alifariki dunia na kuzikwa kwenye Makaburi ya Kanisa
kuu la Lubaga, katika Ibada iliyoongozwa na Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga wa Jimbo
kuu la Kampala, Uganda.
Askofu mkuu Lwanga amemsifu Marehemu Monsinyo Kyeyune
kwa moyo wa sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa nchini
Uganda. Alikuwa ni kati ya viongozi mashuhuri wa Kanisa Afrika Mashariki kama vile:
Kardinali Emmanuel Wamala, Askofu Adrian Ddungu, Askofu Paul Kalanda pamoja na hayati
Kardinali Laurian Rugambwa.
Kilele cha maisha na utume wake wa Kipadre kilikuwa
ni katika Mwaka 1996 alipojiunga na Mwenyeheri Yohane Paulo II kusherehekea Jubilee
ya Miaka 50 ya Upadre kwa kuungana na Mapadre kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliokuwa
wamekusanyika mjini Vatican kwa tukio hili muhimu. Hawa ni Mapadre waliokuwa wamepadrishwa
kunako Mwaka 1946. Wengi wao katika Jubilee hii waliletwa wakiwa wamebebwa kwenye
viti maalum vya wagonjwa!