2013-08-24 09:59:46

Miaka 35 tangu Mzee Jomo Kenyatta alipofariki dunia!


Askofu msaidizi David Kamau wa Jimbo kuu la Nairobi, anawaalika waamini na wananchi wa Kenya katika ujumla wao kujenga mshikamano, umoja wa kitaifa, uzalendo na mafao ya wengi. Askofu msaidizi Kamau ameyasema hayo tarehe 22 Agosti 2013 wakati wa kumbu kumbu ya siku aliyofariki dunia Mzee Jomo Kenyatta, Rais wa kwanza wa Kenya, yapata miaka 35 iliyopita.

Enzi ya uhai wake, Mzee Jomo Kenyatta aliwajengea wananchi wote wa Kenya moyo wa uzalendo na uhuru, mambo ambayo yanapaswa kuendelezwa hata wakati huu kwa kujikita katika mchakato wa maendeleo ya Kenya. Kama binadamu Mzee Kenyatta alikuwa na mapungufu yake, lakini aliona ari na moyo wa kutaka kujenga na kuimarisha nchi ya Kenya kwa ajili ya mafao ya watu wake.

Ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoka kifua mbele kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kenya. "Yaliyopita si ndwele wagange ya sasa na yale yanayokuja"! Hayati Mzee Jomo Kenyatta kunako mwaka 1976 alipata fursa ya kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya na kuwataka kuimarisha maadili na utu wema kwa kukemea maovu ndani ya Jamii. Aliwaambia kwamba, ikiwa kama Jamii itakwenda mrama, viongozi wa kidini watawajibika!

Mzee Jomo Kenyatta alifariki dunia hapo tarehe 22 Agosti 1978 akiwa Mjini Mombasa.








All the contents on this site are copyrighted ©.