Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 21 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa
Ninakuleteeni kipindi tafakari Neno la Mungu masomo Dominika. Tayari tuko Dominika
ya 21 ya mwaka C. Mwaliko toka Neno la Mungu: Jitahidini uingie katika mlango mwembamba
ili upate kuokoka.
Katika Historia
na ndivyo ilivyo Bwana wetu Yesu Kristo ndiye mlango mwembamba. Ili kuweza kuingia
katika mlango huo mwembamba inatudai kujikaza na kuwa ushujaa wahali ya juu. Mlango
mwembamba ni Neno la Mungu, ni upendo wa kimungu ambao lazima humfikie yule ambaye
anaonekana hasitahili kufikiwa, ni Bwana ambaye anaenda Yerusalemu kwa ajili ya kupokea
kikombe cha mateso na hatimaye kifo.
Ni kwa jinsi hiyo basi wokovu ni jambo
la kuhangaikia. Kutokana na mahangaiko juu ya wokovu linakuja swali kwa Bwana likisema
“Hivi ni wachache wanaokoka? Bwana atatoa jibu kwa namna tofauti. Jambo la msingi
kwa Bwana si wangapi wanaokolewa bali ni kwa namna gani na kwa njia gani wanaokolewa!
Bwana
anatoa fundisho lake akitumia mfano wa watu ambao wako mlangoni wakitaka kuingia ndani
ya sherehe lakini hawawezi kuingia. Ilikuwa rahisi kwao kuingia mapema kwa kupitia
mlango mwembamba lakini hawakufanya hivyo na hivi kwa mlango mkubwa Bwana amekwishajiandaa
kufunga! Mlango mwembamba unawakilisha suala la kwamba si rahisi kupita umati bali
mtu mmojammoja.
Kumbe haitoshi kuwa mmojawapo wa wanajumuiya ya Wakristo lazima
kuwajibika. Mlango mwembamba ni chujio, kumbe anapita mmoja baada ya mwingine. Kumbe,
wokovu ni jambo linalomgusa mtu mmoja katika uhalisia wake na mtu huyo katika uhuru
kamili huchagua kuokoka. Ni kwa jinsi hiyo tunafikiria tena, kama mlango ni mwembamba
basi ni kwa ajili ya wale ambao wanaweza kujiingiza katika hali ya ukubwa wa mlango,
yaani kuwa katika vipimo halisi.
Si rahisi kuupanua huu mlango maanake umekwisha
kuwekwa vivyo hivyo. Vipimo vyenyewe ni kumfuasa Bwana kwa kuitikia mashauri ya Injili.
Mpendwa
msikilizaji kulikuwa na mwanafunzi mmoja analalamika kuwa chumba chake ni kidogo na
hivi anakosa hewa, ni katika hilo mwalimu alimwambia kadiri utakavyojitahidi kuwa
mdogo ndivyo ukubwa wa chumba utaongezeka. Fundisho la Bwana kuhusu uongozi lawezapia
kutujuvya vema juu ya hili. Anayetaka kuwa mkubwa lazima awe kama mdogo anayetumikia.
Katika Injili ya Mathayo 5:1-13 juu ya Heri Nane tunakutana na heri moja isemayo Heri
waliomaskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao. Hii yatufundisha kuwa katika
chumba cha sherehe wanaingia wale tu ambao umaskini wa roho umewafanya wawe wepesi!
Mpendwa
msikilizaji, umesikia watu waliokuwa nje ya mlango mkubwa wakisema: sisi tulikula
na kunywa pamoja nawe, hili tatizo ambalo latuonesha kuhangaikia mambo ya kula na
hivi kujenga miili ambayo inashindwa kupita katika mlango mwembamba na matokeo yake
lazima kusubiria mlango mkubwa ambao haiwezekani kupita kwa sababu umati ni mkubwa
na hivi inafika muda Bwana harusi anafunga.
Unene huu si wa kimwili bali ni
unene katika fikira za kidunia: rushwa, unyanganyi, uongozi mchafu na mambo kama hayo.
Haya yote yazuia mtu asifike katika mlango mwembamba.
Bwana katika sehemu ya
pili ya Injili anataja makundi ambayo yatakuwa yameketi chakulani pamoja na Bwana
yaani toka pande zote za dunia. Hawa ni wale katika maisha yao waliwekwa pembezoni,
walijitahidi kuishi maisha ya kiinjili na wakajitahidi polepole kuingia katika mlango
mwembamba. Ni wale ambao walishika sheria ya Bwana, wakitubu na kuomba msamaha daima.
Na sasa wanaonja matunda na furaha ya huruma ya Mungu ambayo waliitafuta katika maisha
yao.
Mpendwa msikilizaji kila mmoja wetu anaowajibu wa kujua wapi aliko katika
sehemu hizi mbili. Hakuna mwingine ambaye atakuja na kuweka maelezo marefu au mafupi
juu ya wapi uliko. Angalia maisha yako kuhusu sakramenti za Kristukama wazipokea vema,
angalia kanuni ya Imani na kisha angalia kama uko usikivu kwa mamlaka halali iliyowekwa
na Mwenyezi Mungu.
Angalia maisha yako katika uwanja wa fikra na maadili ukilinganisha
na heri Nane za Mlimani ambazo ni mwongozo wa maisha yako ya kila siku pamoja na amri
za Mungu. Kwa kifupi somo la pili latuambia wajibu wa kuishi daima katika imani kama
atakavyo Baba yetu wa mbinguni ni wajibu wa kila mmoja wetu hata kama kuna mateso.
Ni kwa namna hiyo twaweza kuingia katika mlango mwembamba.
Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.