Jengeni utamaduni wa Utalii unaowajibisha: kiroho, kiutu na kimaadili!
Kardinali Antonio Maria VegliĆ², Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji
kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi katika ujumbe wake kwa washiriki
wa mkutano wa shughuli za kichungaji nchini Argentina anawataka wakazie umuhimu wa
utalii unaowajibisha.
Anasema, watalii wanapaswa kufaidika na mikakati ya
kichungaji inayofanywa na Mama Kanisa katika kulinda na kudumisha misingi ya maisha
bora ya kiroho, kimaadili, kiutu na kimaendeleo. Sekta ya utalii inapaswa pia kujikita
katika mchakato wa kupambana na umaskini wa kipato na kihali, changamoto inayoendelea
kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Mkutano huu ambao umefunguliwa hapo tarehe 21 Agosti, na kuhitimishwa tarehe
23 Agosti, 2013 umepembua Waraka wa Mababa wa Aparecida kuhusu Utalii kama sehemu
ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu na maboresho ya utu na heshima ya binadamu.
Mababa wa Aparecida wanabainisha kwamba, katika mapambazuko ya Milleniab ya tatu ya
Ukristo, kuna nyanja mbali mbali za shughuli na mikakati ya kimissionari na kati ya
sekta hizi, utalii unapaswa kupewa msukumo wa pekee.
Kanisa pia linapaswa
kujielekeza katika Uinjilishaji wa kina katika michezo, Sinema na kwenye Maduka Makubwa.
Huku ndiko ambako kuna umati mkubwa wa watu unaojionesha katika uhalisia wa maisha
ya kawaida. Sekta ya Utalii ni uwanja mpya unaoweza kutumiwa na Mama Kanisa katika
Uinjilishaji Mpya, ili kukabiliana na changamoto za nyakati hizi katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ukarimu upewe msukumo wa pekee,
kwa kushirikiana na wadau mbali mbali katika miundo ya Kanisa.
Sekta ya Utalii
ni kati ya sekta ambazo zinaendelea kucharuka kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika
ukuaji wa uchumi na inaweza kuwa ni chanzo cha fursa za ajira kwa vijana wengi wanaoteseka
kutokana na hali ngumu ya maisha na ukosefu wa fursa za ajira, kiasi cha kuwafanya
waanze kuishi kwa "kubangaiza".
Ni mwaliko wa kukuza na kudumisha utalii wa
kijamii unaojenga na kuimarisha mshikamano wa upendo sanjari na kukataa mambo ambayo
ni kinyume cha utu na maadili mema. Huu ndio utalii wa ngono, unaopaswa kupatiwa ufumbuzi
kutoka katika chanzo chake. Waamini wajengewe uwezo kwa njia ya Mafundisho Jamii ya
Kanisa, ili kudumisha utalii unaowajibisha: kiutu na kimaadili, ili watu waweze kuheshimiana
na kuthaminiana na wala si kugeuzwa kuwa ni chombo cha kukidhi tamaa za watu. Utalii
uwe ni kikolezo cha maendeleo endelevu na utunzaji bora wa mazingira.
Wajumbe
wa shughuli za kichungaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, wamejadili pamoja
na mambo mengine kuhusu: utamaduni wa kazi; unyanyasaji na unyonyaji unaofanywa maeneo
ya sekta ya utalii; mikakati ya kuwawezesha wajasiriamali ili kujikwamua kiuchumi;
utalii kwa wote na mwono wa utalii katika jicho la kimissionari. Mkutano huu umekuwa
ni fursa kwa wajumbe kusikiliza shuhuda mbali mbali zilizotolewa na wadau wakuu katika
sekta ya utalii kutoka ndani na nje ya Argentina.