Jengeni utamaduni wa kutetea utu wa binadamu kwa kukazia upatanisho na mshikamano
wa kitaifa
Kuna mamillioni ya watu ambao wamepoteza maisha kutokana na dhuluma na nyanyaso zilizofanywa
na tawala za kidhalimu Barani Ulaya. Hawa ni wananchi waliokuwa wanatamani kuishi
katika mazingira ya haki, amani, utulivu na maendeleo, lakini wakakumbana na ukatili
ambao umeacha kurasa chungu katika maisha ya wananchi wengi Barani Ulaya.
Katika
mazingira kama haya, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kusimama kidete kulinda na
kutetea: maisha, utu na heshima ya binadamu sanjari na kukazia upatanisho na mshikamano
wa kitaifa na kimataifa.
Ni changamoto iliyotolewa na Askofu mkuu Julius Janusz,
Balozi wa Vatican nchini Slovenia katika Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya wahanga wa
tawala za kimabavu Barani Ulaya. Katika mahubiri yake anasema, Kanisa linaendelea
kuwahamasisha waamini na watu wenye mapenzi mema kwa njia ya Mafundisho Jamii, kusimama
kidete kulinda na kutetea: uhai, uhuru na demokrasia ya kweli; utu na heshima ya binadamu
pamoja na haki zake msingi.
Imani iwajengee waamini uwezo wa kusamehe na kuanza
mchakato wa upatanisho, kama anavyofafanua Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka
wake wa Kichungaji, Lumen Fidei, Mwanga wa Imani.
Waamini wawe ni vyombo vya
ujenzi wa misingi ya haki, amani na upendo, kwa kujitahidi kumwilisha ndani mwao,
ile Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani; wakitafuta, haki na amani na kwamba, nyanyaso
na madhulumu ya kidini kwa msingi wa kundi fulani kutaka kujijenga kisiasa au kijamii
ni jambo ambalo haliwezi kukubalika. Mwanga wa imani uwasaidie waamini na watu wenye
mapenzi mema kutembea katika upendo, unaowasukuma kutafuta mafao ya wengi, kwa kukazia
haki na amani.
Kurasa chungu za madhulumu na nyanyaso za utu na heshima ya
binadamu, iwe ni fursa ya kuomba na kutoa msamaha ili kujenga utamaduni wa Upatanisho,
Haki na Amani. Hii ndiyo changamoto inayoendelea kutolewa na Mama Kanisa wakati huu
ambayo bado kuna vita, kinzani na migogoro ya kijamii na kisiasa; kwani Mungu ni mwingi
wa huruma na mapendo na wala si mwepesi wa hasira. Kumbu kumbu hii iwe ni nafasi ya
kuendelea kuunga mkono juhudi za kuleta ukombozi kwa wale ambao bado wako kwenye kongwa
la talawa dhalimu sehemu mbali mbali za dunia.