2013-08-23 10:22:54

Biashara haramu ya binadamu ni kielelezo cha utumwa mamboleo!


Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 23 Agosti, inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya kupinga biashara haramu ya binadamu, iliyoanzishwa na UNESCO kunako mwaka 1994.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua madhara na changamoto zilizoko mbele ya Jumuiya ya Kimtaifa kuhusu biashara haramu ya binadamu, ameiagiza Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii itakayokutana mjini Roma kuanzia tarehe 2 hadi 3 Novemba, 2013 kuangalia njia za kisasa zinazoweza kutumika katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu.

Profesa Marcelo Sànchez Sorondo, Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii anasema kwamba, kuna kikosi kazi cha maandalizi ya mkutano wa taasisi hii utakaopembua kwa kina na mapana kuhusu madhara ya biashara haramu ya binadamu katika ulimwengu mamboleo pamoja na kubainisha mikakati ya kisayansi inayoweza kutumika katika mapambano haya. Hii ikiwa ni pamoja na kuhifadhi kwa njia za kisayansi kumbu kumbu za vinasaba vya binadamu ili kuzilinganisha na watu, watoto na wote wanaopotea katika mazingira ya kutatanisha.

Biashara haramu ya binadamu ni undhalilishaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu ni jambo ambalo ni kinyume kabisa cha maadili na utu wema. Biashara haramu ya binadamu inalifaidisha kundi la mafisadi na watu wanaotaka utajiri wa haraka haraka hata kama ni kwenda kinyume cha sheria na kanuni maadili. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu kwa nyakati mbali mbali, kwani ni jambo ambalo linapingwa si tu katika maisha ya kiroho, bali hata katika tamaduni za watu kwani ni jambo ambalo linagusa utu na heshima ya binadamu.

Mada hii ni muhimu sana katika mzunguko wa Sayansi Jamii, lakini pia inamezewa mate katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa mintarafu mikakati ya utandawazi. Biashara haramu ya binadamu inahataarisha usalama wa taifa husika sanjari na haki jamii za kimataifa.

Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa kwa Mwaka 2012 zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 20.9 wanaofanyishwa kazi za suluba kwa ujira kiduchu! Idadi hii inajumuisha kundi la wanawake na wasichana wanaotumbukizwa katika biashara ya ngono na wafanyakazi wa majumbani, jambo ambalo linaenea kwa kasi kubwa katika nchi za Ulaya na Marekani. Inakadiriwa kwamba, kila mwaka kuna jumla ya watu millioni 2 wanaotumbukizwa katika biashara ya ngono na kwamba, asilimia 60% ya idadi hii ya watu ni wasichana.

Biashara haramu ya viungo vya binadamu inachukua asilimia 1% ya idadi ya waathirika wa biashara hii inayowahusisha wafanyakazi katika sekta ya afya ambao walikuwa kiapo cha kulinda na kutetea zawadi ya uhai, lakini wanakiuka viapo vyao kwa kuelemewa mno na malimwengu. Hili ni tatizo kubwa ambao linaonesha jinsi uhalifu wa kimataifa unavyovuruga utu na heshima ya binadamu kwa misingi ya fedha.

Baadhi ya wachunguzi wa mambo wanasema, bado kitambo kidogo tu, biashara haramu ya binadamu itaweza kuvuka kiwango cha biashara haramu ya dawa za kulevya na silaha; biashara ambayo iko katika kiwango cha hali ya juu kimataifa. Biashara ya ngono inaonekana kuwa na soko kubwa katika Nchi Tajiri zaidi duniani na kwamba, waathirika wanatoka katika nchi maskini zaidi duniani.

Hawa ni wanawake, wasichana na watoto kutokana na umaskini na matumaini ya kupata maisha bora zaidi wanajikuta wametumbukizwa katika biashara ya ngono kimataifa. Bara la Asia na Amerika ya Kusini ni kati ya waathirika wakubwa zaidi, lakini Bara la Afrika limeaanza kunyemelewa na watu wenye uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka! Hili ni tatizo la kimaadili na kiutu linalopaswa kupewa uzito wa pekee.

Professa Marcelo Sànchez Sorondo anasema kwamba, biashara haramu ya binadamu ni mfumo mpya wa utumwa mamboleo. Ndiyo maana Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii itatumia mkutano wake wa Mwezi Novemba ili kuwashirikisha wadau mbali mbali kutoka katika sekta ya tiba ya binadamu kuangalia changamoto hii inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu.

Itakumbukwa kwamba, Kanisa tangu mwanzo limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara utumwa kwa kuwataka Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kuwaonjesha watumwa upendo na mshikamano wa Kikristo. Ni mwaliko kama huu uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kuziataka nchi tajiri kutekeleza sheria na kanuni zinazosimamia utu na heshima ya binadamu kwa kupinga biashara haramu ya binadamu kwa vitendo.

Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii inamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuliona tatizo hili na kuanza kulitafutia ufumbuzi kwa njia ya kisayansi, kwani hata hawa wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; ni ndugu zake Kristo. Ni biashara chafu inayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.