2013-08-22 09:32:01

Utamu wa Neno la Mungu!


Mfungeni, mkamtupe gizani..

Tafakari ya Agosti 22,

Miaka ya 1978 - 82 hapa Jijini Dar Es Salaam kampuni ya mabasi jijini ilikuwa na aina ya basi iitwayo "Icarus". Mabasi haya yalikuwa mawili kwa moja. Wengi waliyaita kwa jina la "Ikarusi kumba kumba". Yaani, basi hili likifika kituoni lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria wote - yaani, lilimkumba ye yote aliyetaka kupanda na kwenda safari yake.

Leo katika Injili yetu (Mt 22:1-14) tunakutana na mfano wa mbinguni uliofananishwa na karamu aliyoiandaa baba kwa ajili ya mwanawe. Baada ya watu walioalikwa kushindwa kuhudhuria, mwenye harusi anakumba aliyepo na asiyealikwa. Lakini, ufalme wa Mungu hata kama umetukumba kumba yabidi tuoneshe jitihada fulani. Ni sawa na waswahili wasemavyo - ukibebwa jishikilie, au ukilala katika shuka fupi basi fanya jitihada ya kukunja miguu !

Wapendwa katika Kristo, Bwana Yesu anataka kusema hili kwetu sisi leo,

1. Kwa njia ya Ubatizo na kuwa wana Kanisa tumealikwa tayari kuzaliwa
mara ya pili (Yoh 3:3). Hatua hii ni ya ufunguzi tu wa njia ndefu ya kumfuasa Kristo. Yaani, licha kuitwa kwa jina la Kikristo Mungu anataka aone mfanano wa jina letu la Kikristo na Maisha yetu. Na ndio maana Yesu licha ya kufanya miujiza na mahubiri katika miji pembetatu ya Kibiblia (Korazini, Betsaida, na Kapernaumu) aliwaambia "ole wako Betsaida, ole wako Kapernaumu na ole wako Korazini maana miujiza hii ingefanyika Tiro na Sidoni, wangetubu kwa kuvaa magunia (Mt 11:21).

Mwaliko wetu wa imani umetupa mazingira ya Sakramenti mbili muhimu - Ekaristi na kitubio. Lakini ni wangapi ambao wanashindwa kuzitumia sakramenti hizi kwa visingizio mbali mbali. Wengine ni kisingizio cha utu na ubinadamu wa Padre tu. Ubinadamu wa mwadhimishi wa Sakramenti hii unazuia macho ya mtu asipenye kumuona Kristo mwenyewe. Imani ni kitu cha ajabu sana.

Pale mmoja anapotia shaka ndipo penye wokovu na uponyaji wenyewe. Jemedari Naamani alipoambiwa na Elisha kajichovye mara saba mtoni Yordani alisita. Ila alipopewa moyo alijitosa na kupona (2 Wafalme 5:10). Thamani ya uwepo wa Padre katika msamaha na uponyaji ni mara elfu moja ya uponyaji wa mto Yordani. Padre anapokea Roho mtakatifu kwa huduma tunayoitilia mashaka wakati mwingine (Yoh 20:22) "pokeeni Roho Mtakatifu.."

2. Kanisa letu limekuwa na huruma ya kubatiza wakati mwingine watoto wengi waliozaliwa nje ya ndoa maparokiani. Mapadre wamekuwa wanafumba jicho moja kwa kuwapokea watoto hawa. Lakini bahati mbaya mara baada ya ubatizo huu wana familia wengi wamekuwa wanaendelea na kuishi pamoja - hata wengine kufikia kifo cha ghafla bila ya Sakramenti ya ndoa. Katika injili yetu leo tunaambiwa kuwa maisha ya mbinguni sio kumba kumba kwa majina ya ubatizo, kutoa michango jumuiyani au kuenda kanisani tu. kristu atakagua vazi letu - yaani roho zetu zilizoakisiwa na maisha yetu ya duniani.

Nguo hii nyeupe hutukumbusha jukumu tulilopewa siku ya ibada ya sakramenti ya ubatizo padre alipomwambia mbatizwa "mwanangu umekuwa kiumbe kipya jwa kumvaa Kristu. Nguo hii nyeupe iwe ishara ya cheo chako. Nawe ukisaidiwa kwa maneno na mifano ya jirani zako ukaifikishe safi katika uzima wa milele mbinguni."

3. Mungu wetu ni mwenye haki. Wale waliofanya matendo mema huzawadiwa, "njooni ninyi mlioandikiwa na baba yangu .."(Mt 25:34). Lakini haki ya Mungu huwageukua watenda mabaya kwa adhabu "Gehena ya moto" kwa kuwatupa nje kwenye giza ambapo kuna kilio na kusaga meno (Mt 21:13).


Tusali kwa ajili ya roho ya uongofu kwetu sisi sote. Tuwaombee ambao wanaishi pamoa ila wamekwama kwa kutofunga ndoa waamue mara ili ushiriki wa maisha ya masakramenti na waweze kuosha roho zao, nguo watakayoinesha kwa Mungu baba.

Fadre Benno Michale Kikudo,
Jimbo kuu la Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.