2013-08-22 08:31:06

Kristo ni nuru ya uzima wa milele!


Baada ya kuwa tumemtambua Kristo Nuru ya uzima, na kwamba haitoshi kuwepo tu duniani bali tunapaswa kuandamana naye ili tuwe na uzima, napenda leo tuone tofauti ya ufahamu wa kibinadamu na ufahamu ndani ya Kristo. RealAudioMP3
Bila shaka unang’aa jicho ukijiuliza kwa nini mada hii ya leo. Jibu lipo, karibu tuambae pamoja ndani ya viunga vya Radio Vatican katika makala hii ya vijana.
Kwa karne kadhaa sasa binadamu amekuwa na tabia ya kujiamini zaidi akili yake na uwezo wake wa kuvumbua, kufahamu na kutenda. Mwanafalsafa Nitsche alikuwa akimshauri dada yake Elisabeth kuwa jasiri na kujitafutia njia binafsi kwa kutegemea akili zake ili kufahamu mambo, kwani ndiyo namna nzuri ya kuwa mfuasi bora wa ukweli.
Sishangai yawezekana hata wewe leo ndivyo unavyodhani. Unaona unaweza kufahamu ukweli juu ya ulimwengu, maisha, mafanikio kwa kutegemea akili na uwezo wako. Kwa hivi unaona imani kwa Mungu ni kama ulemavu wa fikra au uzembe wa kutafuta mafanikio. Kama na wewe unadhani hivyo basi umebugi rafiki yangu. Ngoja nikupe mistari ya kweli kuhusu ufahamu na mafanikio.
Tumesema Kristo ni Nuru ya ulimwengu, yeye ni Muumba. Kumbe ina maanisha yeye aliyeumba vitu vyote ndiye anayefahamu ukweli kuhusu hivyo vitu. Kama formula ya Coca Cola vile, watu wanahangaika kuitafuta, lakini ni siri ya wachache waliovumbua na waliochanganya. Hata hivyo Mungu anajua yote hayo. Ukitaka kufahamu ukweli halisi wa vitu na mambo, mwamini na andamana na Kristu.
Kwa akili yako unaweza kufahamu fahamu vijimambo, au kwa uwezo wako unaweza kujipatia vimafanikio vya hapa na pale ukajiona basi na wewe babu kubwa, ukajiona pedeshee fulani. Ukweli ni kwamba ufahamu wako ni hafifu, sio kamili na mafanikio ni ya muda au hata ni halamu. Namaanisha wale mnaotumia njia zisizo halali kujipatia mafanikio.
Hii ni kwa sababu peke yako, kwa nguvu za kibinadamu huwezi kupata mafanikio au ufahamu unaoridhisha. Hapo unakuwa unaishi gizani, unahitaji Nuru ya kweli, ambayo ndiyo ninayokuzungumzia hapa, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Hai. Unafanya mchezo nini wewe.
Tutazame wale tunaishi katika imani ndani ya Kristu, tunafahamu mambo kibao, tunaridhika, tuna furaha na tuna amani. Unaelewa tofauti ipo wapi, ngoja nikutonye kidogo.
Baba Mtakatifu Francisko anasema pale ufahamu na uwezo wa binadamu unapofika kikomo, Nuru ya Kristo inahitajika kuangaza undani wa mambo na kumtia nguvu mwanadamu (Rej. Lumen Fidei, 3). Na hii ametukumbusha kule Rio de Janiero, Brasil wakati wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, bila Nuru ya Kristo huwezi kutambua na kutofautisha kwa usahihi kati ya wema na uovu. Kwa hiyo ni rahisi kwa kijana kufakamia mambo ya ajabu, starehe zilizo hatarishi, ulevi, matumizi haramu ya dawa za kulevya na kadhalika. Tuliza nafsi, mwamini Kristo, utaepuka uovu, utakuwa mwema, utapata mafanikio, utaridhika na kile ulicho nacho, utakuwa na amani na furaha.
Mpaka hapo umeionaje mistari yangu kuhusu Nuru hii, Kristo Mwenyewe. Unanichezea sauti ya kinabii wewe, ntakunasa, na utaongoka tu. Basi kwa leo sina la ziada, tuonane tena makala ijayo. Kutoka Studio za Radio Vatican, ni Padre Celestine Nyanda.








All the contents on this site are copyrighted ©.