2013-08-22 10:18:56

Jengeni maisha na wito wenu katika: Sala, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa!


Askofu Evarist Marcus Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha na wito wa Mapadre wanaotumwa kwenda kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kuwatakatifuza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Wanashiriki utume wa Mama Kanisa katika utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya tafakari ya kina ya Neno la Mungu na Mafundisho ya Kanisa. Mapadre ni viongozi wa Familia ya Mungu katika maeneo yao ya huduma.

Askofu Chengula katika Maadhimisho ya Sakramenti ya Daraja Takatifu kwa nyakati mbali mbali Jimboni Mbeya, amekazia umuhimu kwa Mapadre kuhakikisha kwamba, wanayasimika maisha yao katika nguzo ya sala kama njia ya kuzungumza pamoja na kuimarisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu. Bila maisha ya sala ya kina, Mapadre wanaweza kukaukiwa na hatimaye, kukata tamaa katika maisha na wito wao wa Kipadre.

Ni changamoto kwa Mapadre kujikita katika Tafakari ya kina ya Neno la Mungu, kwa kutambua kwamba, hiki ndicho chakula kinachoboresha maisha yao ya kiroho, ili hatimaye, waweze kuwamegea waamini Neno la Uzima wa Milele. Mapadre wajenge utamaduni na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, hapa ni mahali ambapo Padre, Mtawa au mwamini anapata fursa ya kumsikiliza Yesu anayezungumza naye kutoka katika undani wa dhamiri yake nyofu. Jambo la msingi ni mwamini kumwachia Yesu nafasi ili aweze kuzungumza naye.

Askofu Chengula anawaambia Mapadre kwamba, haitoshi kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kama njia ya kuwatakatifuza Watu wa Mungu, lakini hata wao pia wawe ni wa kwanza kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Mapadre wawe na ratiba ya maisha ya kiroho, ili wasifanye mambo kwa bahati nasibu!

Mapadre wahakikishe kwamba, wanatenga muda kwa ajili ya kutembelea na kusali kwenye Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo kwani hapa ni shule ya Sala, Maandiko Matakatifu na Maisha ya Kisakramenti. Hapa ni mahali ambapo waamini wanajifunza kujenga Familia ya Mungu inayowajibika kwa kumwilisha imani katika matendo, changamoto katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na hapo baadaye. Katika Jumuiya ya Ndogo ndogo za Kikristo, Mapadre wanashiriki kwa ukamilifu majiundo endelevu wakipokea na kuwagawia ndugu zao katika Kristo imani, matumaini na mapendo yaliyomo moyoni mwao!

Askofu Chengula pia anawataka Mapadre na viongozi wote wa Kanisa kuwa makini na matumizi ya mali ya Kanisa kwa kutambua kwamba, mali yote ya Kanisa waliyokabidhiwa ni kwa ajili ya azma ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hii ni changamoto ya kuacha tabia ya ubinafsi na uchu wa mali kwani mambo haya yanaweza kuwapotosha Makleri katika maisha na wito wao wa Kipadre. Watu wanataka kuwaona na kukutana na Mapadre wanaoonesha utakatifu na heshima ya maisha ya Kipadre.

Askofu Chengula anawataka Mapadre na Waamini katika ujumla wao kuanzia katika Familia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, Vigango na Parokia za Jimbo Katoliki Mbeya, kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kikanisa, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu, Jimboni Mbeya na Tanzania katika ujumla wake.

Askofu Chengula amekemea tabia ya baadhi ya waamini wa dini mbali mbali nchini Tanzania kutumia dini kama miamvuli ya kuanzisha na kuchochea vurugu kuacha mara moja kwani wanaweza kulitumbukiza Taifa katika maafa makubwa. Watanzania wajenge na kuimarisha: amani, utulivu, upendo na mshikamano wa kitaifa, urithi mkubwa walioachiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Misingi hii isipozingatiwa, watanzania watajikuta wakitumbukizwa katika machafuko ya udini na siasa tenge zinazowagawa wananchi na hivyo kuwa ni chanzo cha vurugu na kinzani.







All the contents on this site are copyrighted ©.