Dumisheni udugu, amani na mshikamano na maskini kama kielelezo cha imani tendaji!
Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya kipapa anasema kwamba, Baba Mtakatifu
Francisko inaonekana ni mtu mwenye maneno machache, lakini mengi anayaonesha kwa njia
ya vitendo na ushuhuda wa maisha yake mwenyewe.
Kati ya mambo mengi ambayo
kamwe hayataweza kufutika akilini mwa maelfu ya waamini na watu wenye mapenzi mema
waliokuwa wanafuatilia tukio la kutangazwa kwake hadharani kwa njia ya vyombo vya
mawasiliano ya jamii, ni pale alipoinamisha kichwa, akawaomba waamini na wote waliokuwa
wamemiminika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kusali kwa ajili yake
katika ukimya!
Kufumba na kufumbua, Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro,
ukawa kimyaaaaa kwa kitambo! Waamini wakawa wa kwanza kumbariki Baba Mtakatifu Francisko,
kabla hata ya Yeye mwenyewe kutoa baraka zake za kitume. Hili ni tukio ambalo kwa
hakika lilikuwa linatoka katika undani wa maisha yake, kielelezo makini cha utume
wake kama mchungaji mwenye uzoefu na mang’amuzi ya kina!
Padre Cantalamessa
anasema, si haba kwamba, ameamua kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi mtu
aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Mtakatifu Francisko ni mtu aliyeshuhudia vita na kinzani za kijamii
na kidini, akageuka na kuwa ni chombo cha amani, urithi ambao Baba Mtakatifu Francisko
anapenda kuurithisha kwa Kanisa na Jamii inayokabiliana na kinzani, migogoro na vita
vinavyoendelea kupelekea taabu, mahangaiko na mateso ya watu wasiokuwa na hatia.
Mtakatifu
Francisko alipenda na kuthamini mazingira, ambayo kimsingi ni haki ya uumbaji ambayo
Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu.
Lakini, dira na mikakati yote hii anasema
Padre Raniero Cantalamessa inaweza kufanikiwa tu, ikiwa kama Waamini na Jumuiya ya
binadamu katika ujumla wake, itashikamana katika umoja na udugu, kwa kutambua kwamba,
wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu wanapaswa kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana.
Kwa maneno machache anasema Padre Cantalamessa, Baba Mtakatifu Francisko anataka
kukazia: udugu, amani, mshikamano wa dhati na maskini kama kielelezo cha imani tendaji,
changamoto kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.