Watu wengi bado wana majeraha ya vita, chuki na kinzani za kijamii!
Askofu Alexis Touably wa Jimbo Katoliki Agboville, nchini Pwani ya Pembe ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Tume ya Majadiliano, Ukweli na Upatanisho nchini humo anasema, kuna
haja kwa Serikali kuongeza muda wa kazi kwa tume hii ili iweze kukamilisha vyema zaidi
dhamana iliyokuwa imepewa katika mchakato wa kutafuta haki, amani na upatanisho miongoni
mwa wananchi wa Pwani ya Pembe ambao wanaendelea bado kuponya makovu ya vita, kinzani
na migogoro ya kijamii.
Si rahisi kwa Tume hii kuweza kukamilisha dhamana
hii nyeti kwa kipindi cha mwaka mmoja, ukizingatia kwamba, vita na kinzani za kijamii
zimeleta athari kubwa kwa wananchi wengi. Kwa haraka haraka watu wanaweza kuona kwamba,
katika kipindi cha Mwaka mmoja, tume imeshindwa kukamilisha lengo na wajibu iliyokuwa
imekabidhiwa kwao, lakini wanasahau kwamba, wananchi wengi bado wanaendelea kuponya
majeraha kiasi kwamba, walishindwa kuonesha utashi wa ushirikiano na tume wakati wa
kutekeleza dhamana yake.
Mchakato wa uponyaji unazingatia pia uhuru wa mtu
binafsi anayeweza kujifungua kwa ajili ya kushirikiana na wengine katika kuleta mabadiliko,
au kukataa kabisa na kuendelea kubaki amejifunga katika undani wake. Baadhi ya watu
wamekataa kuonesha ushirikiano kwani wanasema wameathirika sana na kwamba, itawachukua
muda mrefu kurudi katika hali ya kawaida. Yote haya ni madhara ya vita, machafuko
ya kisiasa na chuki za kidini.
Askofu Touably anasema kwamba, bado Tume ya
Majadiliano, Ukweli na Upatanisho inahitajika ili kuponya madonda ya vita, chuki na
kinzani za kijamii nchini Pwani ya Pembe.