2013-08-21 09:56:52

Watawa wa Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Mombasa wanamwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani!


Askofu mkuu Boniface Lele wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, katika Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Watawa wa Shirika la Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Mombasa waliokuwa wanaweka nadhiri zao za daima, wengine wakiadhimisha Jubilee ya Miaka 50 na 25 ya maisha ya kitawa.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Lele amewahimiza watawa kuongeza upendo, furaha na ukarimu katika huduma wanazozifanya kwa ajili ya Watu wa Mungu wanaowazunguka, daima wakijifunza kutoka kwa Bikira Maria aliyejitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Familia Takatifu. Watawa waendelee kuwa kweli ni mwanga wa imani kwa kujikatalia mambo ya dunia ili kuambatana na Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Watawa wasimame kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wao kwa Kanisa na ulimwengu.

Hii ndiyo changamoto ambayo Mama Kanisa anaendelea kutoa kwa Watoto wake wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Mapendo na ukweli vinajidhihirisha pale ambapo imani inamwilishwa katika matendo na hivyo kuwa ni dira inayomwongoza mwamini kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha na huduma.

Hii ni changamoto ya kupenda kama Mwenyezi Mungu anavyopenda na kuthamini. Waamini wajitahidi kumwilisha ndani mwao, fadhila ya imani, matumaini na mapendo. Watambue kwamba, wanatakiwa kuitekeleza amri ya upendo kwa Mungu na jirani kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Askofu mkuu Boniface Lele anasema kwamba, maisha ya Sala, Sakramenti na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu yanaweza kumsaidia mwamini kukuza na kuimarisha uhusiano wake na Mwenyezi Mungu, kiasi hata cha kuweza kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani. Askofu mkuu Lele anawashukuru watawa kwa majitoleo na moyo wao wa sala kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu Jimboni Mombasa na sehemu mbali mbali za dunia wanakotekeleza utume wao.

Shirika la Watawa wa Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Mombasa lilianzishwa kunako mwaka 1941, ili kuwashirikisha waamini furaha ya ushuhuda wa Injili kwa Kristo na Kanisa lake kwa watu wanaoishi Jimbo kuu la Mombasa kwa njia ya huduma makini. Katika kipindi cha miaka 73, Watawa hawa wamekuwa wakitoa huduma katika maisha ya kiroho, kwenye sekta ya elimu, afya na mawasiliano nchini Kenya, Tanzania, Ulaya na Marekani.

Shirika la Watawa wa Mtakatifu Yosefu linaongozwa na roho ya Mtakatifu Benedikto, yaani Ora et Labora: Sala na Kazi; daima wakijitahidi kufuata na kuiga upole, imani na unyenyekevu wa Mtakatifu Yosefu mchumba wake Bikira Maria na Baba Mlishi wa Mtoto Yesu. Mtakatifu Yosefu ni dira na kielelezo cha maisha na utume wao ndani ya Kanisa.

Wafuatao wamefunga nadhiri zao za daima:
1. Sr. Rachel Wakene.
2. Sr. Catherine Furaha,
3. Sr. Josephine Mulunde,
4. Sr. Phylace Mokaya,
5. Sr. Mary Mutono pamoja na
6. Sr. Gladys Moraa.

Masista wafuatao wameadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya Maisha ya Kitawa
1. Sr. Hedwiga Mang'oli,
2. Sr. Blandina Matesha pamoja na
3. Sr. Auxilia Mkasumbuka.

Masista wafuatao wamemwimbia Mungu utenzi wa sifa kwa Jubilee ya Miaka 25
1. Sr. Jacinta Kivinya,
2. Sr. Gisela Wanyika,
3. Sr. Agnes Muthoni,
4. Sr. Rose Mbeneka pamoja na
5. Sr. Bernadette Mwelu.

Imeandaliwa na Sr. Bridgita Samba Mwawasi.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.