Someni alama za nyakati ili kuwahamasisha waamini kuchangia mchakato wa Uinjilishaji
mpya kwa hali na mali!
Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mkuu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji
wa watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya kazi za Kimissionari katika mahojiano na
Radio Vatican anasema, kwamba, Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa katika nchi mbali
mbali wanapaswa kusoma alama za nyakati kwa kuwaelimisha na kuwahamasisha waamini
na watu wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya
kwa hali na mali.
Mashirika
ya Kipapa ya kazi za kimissionari yatambue wajibu na dhamana ya kuendeleza kazi ya
Uinjilishaji mpya, kwa kuwahamasisha waamini ili waweze kujitoa kikamilifu ili kushiriki
katika utume huu. Mashirika haya yajiwekee mikakati ya uhamasishaji pamoja na kujijengea
nguvu ya rasilimali fedha. Wakurugenzi wa PSM wajitahidi kuwatambua waamini wao ili
kuweza kuwashirikisha kila mtu kadiri ya uwezo na nafasi yake.
Umefika wakati
wa kubadilisha mfumo wa uhamasishaji wa jumla na kuanza kuwalenga watu au makundi
ya watu kwa njia: mitandao ya kijamii, barua, matumizi sahihi na makini ya vyombo
vya upashanaji habari. Watu wahabarishwe kuhusu kazi na utume wa Mashirika ya Kipapa
ya Kazi za Kimissionari, ili waweze kujitoa kikweli kweli. Wakurugenzi hawa watambue
kwamba, fedha inayopatikana kama sehemu ya mchango wa waamini kwa ajili ya kazi za
kimissionari inapaswa kutumiwa kadiri ya lengo lake kwa kuzingatia misingi ya ukweli,
uwazi na uwajibikaji.
Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari yasome
alama za nyakati na kuanza kushiriki katika mchakato wa maboresho wa uhamasishaji,
ukusanyaji na matumizi ya rasilimali fedha.