2013-08-20 11:23:48

Mchakato wa kumtangaza Kardinali Otunga kwa ngazi ya Jimbo kukamilika hapo tarehe 27 Septemba 2013


Mheshimiwa Padre Celestino Bundi, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa na Kazi za Kimissionari nchini Kenya anasema, mchakato wa kumtangaza Kardinali Maurice Michael Otunga kuwa Mwenyeheri unatarajiwa kufikia ukomo wake kwa ngazi ya Kijimbo hapo tarehe 27 Septemba 2013.

Tukio hili linatarajiwa kutanguliwa na Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Kardinali Otunga pamoja na kuchangisha fedha ya kuanzisha Mfuko wa Kardinali Otunga hapo tarehe 6 Septemba 2013.

Kamati ya mchakato wa Kardinali Otunga inaendelea kukamilisha maandalizi, ikiwa ni pamoja na Kalenda za Mwaka 2014 zitakazosambazwa na Mabinti wa Mtakatifu Paul ambao wana mtandao mkubwa katika masuala ya maduka ya vitabu. Tarehe 6 Septemba 2013, Kamati itazindua mtandao utakaokuwa na taarifa na maelezo mbali mbali kuhusiana na maisha na utume wa Kardinali Otunga tangu alipozaliwa kunako mwaka 1923 hadi kufariki dunia kunako tarehe 6 Septemba 2003.

Kwa ufupi, Kardinali Otunga alizaliwa kunako tarehe 31 Januari 1923. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapadrishwa hapo tarehe 3 Oktoba 1950. Tarehe 25 Februari 1957 akawekwa wakfu kuwa Askofu na Askofu mkuu James Robert Knox.

Tarehe 15 Novemba 1969 akateuliwa kuwa Askofu mkuu na hapo tarehe 5 Machi 1973, Papa Paulo wa VI akamteuwa kuwa Kardinali. Baada ya huduma iliyotukuka kwa Familia ya Mungu nchini Kenya, akafariki dunia hapo tarehe 6 Septemba 2003, Jijini Nairobi.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Otunga alikuwa ni kati ya Mapadre wa kwanza kwanza nchini Kenya. Akabahatika kuteuliwa kuwa ni Askofu, Askofu mkuu na hatimaye Kardinali. Ilikuwa ni tarehe 11 Novemba 2011 Jimbo kuu la Nairobi lilipoanzisha mchakato wa kumtangaza Kardinali Otunga kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu. Mchakato huu kwa ngazi ya Kijimbo unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 27 Septemba 2013.







All the contents on this site are copyrighted ©.