Hali kuhusu mabadiliko ya tabianchi, njaa na utapiamlo!
Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa,
FAO kuhusu: uchafuzi wa mazingira kutokana na uwepo wa hewa ya ukaa, baa la njaa na
utapiamlo, zinaonesha jinsi ambavyo sekta ya kilimo inavyochangia katika masuala haya.
Hewa ya ukaa
inayozalishwa kutoka katika sekta ya kilimo imeongezeka kwa asilimia 1.6 kwa mwaka
katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, yaani kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2010.
Hali hii imesababisha ongezeko la hewa ya ukaa angani kwa asilimia kumi; jambo
linalochangiwa na kazi zabinadamu. Shughuli za ufugaji na matumizi ya mbolea za viwandani
ni kati ya mambo makubwa yanayoendelea kuchangia uchafuzi wa mazingira. Hapa hewa
chafu inayozalishwa angani kutokana na janga la uchomaji misitu na matumizi ya ardhi
haikuingizwa.
Takwimu za FAO kuhusu: mtaji na uwekezaji; mabadiliko ya tabianchi;
upatikanaji wa chakula; uzalishaji wa chakula na biashara; baa la njaa na utapiamlo;
athari zake katika hali ya nchi na uhusiano wake na maisha ya binadamu zimechambuliwa
kwa kina na mapana. FAO inasema kwamba, ukosefu wa chakula umekuwa pia ni chanzo cha
kinzani na migogoro ya kijamii. Kutokana na changamoto hizi kuna haja ya kuwa ni matumizi
mazuri ya rasilimali katika sekta ya kilimo, ili kuhakikisha kwamba, kilimo kinakuwa
ni endelevu na rafiki kwa mazingira.
Katika kipindi cha Mwaka 2010 hadi mwaka
2012 kulikuwa na watu millioni 870 waliokuwa wanapata lishe duni. Hii ni sawa na asilimia
12.5 ya idadi ya watu duniani, wengi wao ni wale wanaoishi katika Nchi changa. Kati
ya mwaka 2005 hadi mwaka 2011, nchi nyingi za Kiafrika zilisema kwamba, kuna watu
waliokuwa wanakabiliwa na lishe duni hali iliyopelekea watu kudumaa na wengine wengi
kuwa na uzito mdogo kuliko kiwango cha wastani. Barani Afrika idadi hii ni sawa na
asilimia 20% na kwamba, hali ni mbaya kwa wananchi wanaoishi katika nchi za Pwani
ya Pembe.
Takwimu za uzalishaji katika sekta ya kilimo zinaonesha kwamba,
uzalishaji umeongezeka maradufu na kwamba, uzalishaji wa mazao ya nafaka umeongezeka
zaidi kwani hiki ni chakula kinachotumiwa zaidi na watu wanaoishi katika nchi maskini
zaidi duniani. Uzalishaji huu umeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini China na India.
Nafaka ni chakula ambacho kwa sasa kinatumika pia kama nishati uoto! Hali ya uchumi
inabainisha kwamba, kumekuwepo na ongezeko la ununuzi wa chakula unaofanywa na Serikali,
hasa kutoka katika nchi zinazoendelea. Ongezeko la bei ya mazao ya nafaka imeongezeka
kwa asilimia 4% na hivyo sekta ya kilimo imechangia asilimia 1% ya Pato Ghafi la Dunia.