2013-08-19 09:45:11

Wahamiaji: mahujaji wa imani na matumaini


Baraza la Maaskofu Katoliki Australia kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 25 Agosti 2013 linaadhimisha Juma la Wakimbizi na Wahamiaji na kwa namna ya pekee Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuzingatia kanuni maadili badala ya kukwepa dhamana hii kwa kisingizio cha hali mbaya ya uchumi au usalama wa taifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linapenda kuendeleza kauli mbiu iliyokuwa imechaguliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa Maadhimisho ya Siku ya 99 ya Wakimbizi na Wahamiaji kwa Mwaka 2013, iliyoadhimishwa Kikanisa hapo tarehe 13 Januari 2013, yaani: Wahamiaji: mahujaji wa imani na matumaini.

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Juma hili wanasema, Jumuiya ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini Australia inapaswa kushiriki kikamilifu katika majadiliano kuhusu hali ya wakimbizi na wahamiaji nchini Australia kwa kuondokana na majadiliano ambayo mara nyingi yamekuwa yakilenga katika masuala ya uchumi na usalama wa taifa na kuanza sasa kujikita katika majadiliano yanayogusa kanuni maadili, mafao ya mtu pamoja na haki zake msingi. Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wala si kubezwa na kutwezwa kama inavyojidhihirisha katika nchi nyingi.

Huu ni wajibu msingi kwa kila mtu binafsi, Parokia pamoja na Taasisi zote za Kanisa Katoliki kuhakikisha kwamba, zinaanzisha mchakato wa kuhamasisha majadiliano yatakayobainisha wajibu na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji nchini Australia. Serikali nchini humo inawajibu wa kutoa majibu muafaka kuhusiana na hatima ya wakimbizi na wahamiaji katika ngazi mbali mbali.

Kanisa kwa upande wake, halina budi kutambua mchango wake katika maisha ya kiroho kwa wakimbizi na wahamiaji; na wote wanaoomba hifadhi ya kisiasa, kwani maisha ya kiroho na jambo muhimu kwa kila mwamini. Wakimbizi na wahamiaji wengi nchini Australia ni wale wanaotoka katika Jumuiya za Kikristo.

Ni watu waliokuwa wanachama wa vyama mbali mbali vya kitume na baadhi yao walikuwa hata wakishiriki nyadhifa za uongozi wa Kanisa, lakini kutokana na sababu mbali mbali wamelazimika kuyakimbia makazi na nchi zao na sasa wanajikuta wakiwa ugenini. Waamini hawa wanaweza kushirikisha mang’amuzi na utajiri wa imani yao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linasema, kuna sababu mbali mbali ambazo zinapelekea baadhi ya watu kuyakimbia makazi na nchi zao. Wengi wanakimbia vita, hali ngumu ya maisha na umaskini; ukosefu wa fursa za ajira; majanga na maafa asilia; magonjwa ya mlipuko; dhuluma na nyanyaso. Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linaonesha mikakati yake ya kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji ni kuhakikisha kwamba, viongozi kitaifa na kimataifa pamoja na mashirika ya kimataifa; yanashiriki kikamilifu katika kushughulikia hatima ya wakimbizi na wahamiaji kwa kujenga na kuimarisha mshikamano unaoongozwa na kanuni auni.

Kuwepo na ushirikiano na nchi asilia wanamotoka wakimbizi na wahamiaji hao pamoja na nchi zinazotoa hifadhi. Ushirikiano huu unawezekana pale tu heshima na utu wa wakimbizi na wahamiaji vinathaminiwa sanjari na kuenzi haki zao msingi kama mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa nchi wanamotoka na kwa zile nchi ambazo zinatoa hifadhi kwa watu hawa.

Wakimbizi na wahamiaji wanaohofia maisha yao, wasinyimwe hifadhi ya kisiasa na wala wasifungwe gerezani, kwani mwelekeo wa sasa ni kuwaweka vizuizini wakimbizi na wahamiaji kwa kisingizio cha usalama wa taifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujiuliza swali msingi, Je, wao kama mtu binafsi anaweza kufanya nini ili kuleta suluhu ya matatizo na changamoto zinazowakabili wahamiaji na wakimbizi, bila kupoteza matumini ya maisha. Waamini wanaalikwa kutafakari kwa kina kuhusu wahamiaji kama mahujaji wa imani na matumaini, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji nchini Australia kwa kuwaomba waamini kuendelea kusali ili kwamba imani na matumaini ziwe ni dira na mwongozo kwa Jumuiya za Kikristo ili kuishi kwa umoja, upendo na mshikamano wa dhati na Wakimbizi pamoja na wahamiaji wanaotafuta nafuu ya maisha nchini Australia.








All the contents on this site are copyrighted ©.