Tafuteni mambo ya msingi zaidi, gundueni njia na mbinu za Uinjilishaji mpya!
Mkutano wa 34 wa urafiki kati ya watu wa Mataifa kwa mwaka huu unaongozwa na kauli
mbiu "dharura kwa binadamu" na changamoto kubwa katika azma ya Uinjilishaji kwani
Kanisa linatambua kwamba, binadamu ndiye njia inayotumiwa na Mama Kanisa hata katika
ulimwengu wa utandawazi, kila mwamini anaalikwa kugundua utume wake na kujikita zaidi
katika mambo msingi, daima akitafuta njia na mbinu mpya za Uinjilishaji.
Hii
ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa mkutano wa urafiki
kati ya watu wa mataifa uliofunguliwa rasmi hapo tarehe 18 Agosti na unatarajiwa kuhitimishwa
hapo tarehe 24 Agosti 2013, ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Tracisio Bertone,
Katibu mkuu wa Vatican. Ujumbe huu umesomwa na Askofu mkuu Francesco Lambiasi wa Jimbo
Katoliki Rimini, Italia wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi wa
mkutano huu, Jumapili iliyopita.
Binadamu anaendelea kuwa ni fumbo la uhuru,
neema, ufukara na ukuu. Ni njia inayotumiwa na Mama Kanisa katika utekelezaji wa kazi
ya ukombozi iliyoanzishwa na Mwenyezi Mungu katika Agano la Kale; kwa namna ya pekee
utu na heshima ya binadamu vinajionesha kwenye Fumbo la Umwilisho, linalomwonesha
Kristo kuwa ni ukweli na njia ya maisha. Ni mlango uliofunguliwa kwa ajili ya wote.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, mwanadamu bado ni mdau mkubwa katika masuala ya kiuchumi,
kisiasa na kwa ajili ya njia za mawasiliano ya kisasa, ndiyo maana mwanadamu amekuwa
ni sawa na "kichwa cha mwendawazimu" kila mtu anataka kukifanyia majaribio ili kuharibu
uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu unaowafanya binadamu kuwa huru jambo ambalo ni
kikwazo kwa wale wasiowatakia mema binadamu.
Mkutano wa Rimini unapania kutoa
tafakari ya kina inayomrudishia mwanadamu utu na heshima yake, tangu pale anapotungwa
mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni mwaliko wa
kuheshimu na kuthamini utakatifu wa maisha ya mwanadamu, ili kila mtu aweze kutekeleza
kwa ukamilifu utume wa maisha yake. Kristo amelidhaminisha Kanisa: Injili, Sakramenti
na kwamba, Kanisa ni chemchemi msingi ya matumaini ya mwanadamu, changamoto kwa waamini
kuwaendea wote wenye kiu ya kutaka kukutana na kumfahamu Mwenyezi Mungu.
Waamini
wajitahidi kumuiga Yesu aliyejifanya mwanadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, ili
kuwa karibu na kila mtu na katika medani mbali mbali za maisha, ili wote waweze kuonja
upendo wa Mungu. Waamini wanachangamotishwa kuwa na ujasiri wa kutangaza Habari Njema
ya Wokovu bila woga wala makunyanzi; wakati ufaao na wakati usiofaa kwa kuzingatia
ukweli na heshima.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni wajibu wa kila
mwamini anayetumwa kumhudumia mwanadamu, akijitahidi kumwendea pembezoni mwa maisha
yake ya kijamii na kiroho alikojificha. Waamini wanapaswa kuwa ni waaminifu kwa Kristo
na Kanisa lake, ili kuweza kutekeleza utume wa Mama Kanisa kama Mama na Mwalimu; wakionesha
utii katika ukweli, ili watu waweze kumrudia Kristo na kujifunza kutoka kwake, kwani
Yeye ndiye njia, ukweli na uzima.
Ni mwaliko wa kuwaendea wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii hasa maskini wa hali na maisha ya kiroho. Hawa ni maskini wanaotindikiwa
upendo; wenye kiu ya ukweli na haki; watu wanaomtafuta Mwenyezi Mungu, ili waweze
kumpeleka kwa jirani zao.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba,
tafakari hii inaweza kuwa ni msaada mkubwa wakati huu wajumbe wa mkutano wa 34 wa
urafiki kati ya watu wanapokutanika mjini Rimini ili kufanya tafakari ya kina kuhusu
dharura ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia uwepo wake kwa njia ya
sala na sadaka yake takatifu.