Kongamano la IV la Kimissionari Kitaifa nchini Argentina
Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linaadhimisha Kongamano la IV la Kimissionari
Kitaifa kama fursa ya kuwatia moyo na kuwaimarisha waamini kutekeleza dhamana na wajibu
wao wa Kimissionari katika Majimbo na Kanisa kwa ujumla, mintarafu maelekezo ya Mkutano
wa nne wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kusini na Caraibi, uliofanyika
mjini Aparecida.
Maadhimisho ya Mwaka 2013 yanaongozwa na kauli mbiu Wamissionari
wa Argentina, shirikisheni imani yenu". Maadhimisho haya yanafanyika wakati huu Mama
Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani. Hii pia ni sehemu ya Maandalizi ya
Kongamano la IV la Amerika na lile la IX yatakayofanyika nchini Venezuela.
Kwa
sasa Maadhimisho haya yanawapatia waamini nafasi ya kutafakari changamoto zinazokwamisha
mchakato wa Utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu katika ulimwengu wa utandawazi na
maendeleo ya sayansi na teknolojia; Ulimwengu ambao umesheheni kila dalili za ukanimungu.
Maadhimisho
ya Kongamano hili yamefunguliwa kwa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko anayewapongeza
kwa ari na moyo wa kimissionari wanaouonesha na kwamba, umefika wakati wa kutoka katika
undani mwao ili kwenda kutangaza Injili ya Kristo pembezoni mwa maisha ya Jamii. Kongamano
hili la kitaifa liwe ni nafasi ya kukua na kukomaa katika utume wa kimissionari kwa
kutumia vyema na bila woga, karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu.
Baba
Mtakatifu anawaombea ili kwamba, Yesu mwenyewe aweze kuwaondoa kutoka katika kishawishi
cha kutaka kuponda raha mustarehe. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia uwepo wake
kwa njia ya Sala na Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.