2013-08-19 07:44:46

Kanisa linahamasisha utunzaji bora wa mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi


Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani ilikuwa ni fursa nyingine kwa vijana kuweza kujinoa kuhusu mada mbali mbali katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira, dhamana ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu. Kanisa linapenda kukazia kuhusu dhana ya utunzaji wa mazingira kadiri ya Mafundisho ya Kanisa. RealAudioMP3

Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1992 Jumuiya ya Kimataifa ilianzisha mchakato unaopania kudumisha maendeleo endelevu, uliofanyika huko Rio. Maendeleo endelevu ni dhana inayobainisha maendeleo yanayogusa mahitaji ya watu wa kizazi hiki bila kuhatarisha maisha ya kizazi kijacho.

Kunako mwaka 2012, Jumuiya ya Kimataifa ikakuyakutanisha Mataifa makubwa yaliyokuwa yanaibukia katika kasi kubwa ya maendeleo ili kutafuta mbinu mkakati wa utekelezaji wa mpango wa maendeleo endelevu, mkutano huo ukaitwa Rio+20. Kwa bahati mbaya, mkutano huu ukahitimishwa pasi na ufafanuzi makini wa utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu katika Jumuiya ya Kimataifa.

Ni mchango wa Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati alipokuwa anachangia kwenye kongamano la utunzaji bora wa mazingira wakati wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani huko Rio de Janeiro. Anasema, Mababa watakatifu wamekuwa wakikazia kwa namna ya pekee utunzaji bora wa mazingira kama msingi wa kuendeleza haki na amani duniani, kama alivyowahi kusema Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, Upendo katika Ukweli, “Caritas in Veritatis”, anaeleza kwamba, maendeleo endelevu ni changamoto inayomtaka kila mtu kuwajibika kadiri ya nafasi na dhamana yake, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Papa Francisko alipokuwa anazungumza na Waandishi wa habari siku chache tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, alibainisha kwamba, ameamua kuchagua jina la Francisko kwani ni Mtakatifu aliyesimama kidete kulinda na kutunza mazingira.

Hii ni changamoto kwa kila mtu kulinda mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi. Lakini, mwelekeo wa sasa ni watu kutaka kujinufaisha wenyewe, kiasi cha kuhatarisha amani, maendeleo na ustawi wa wengi. Mafundisho ya Kanisa kuhusu utunzaji bora wa mazingira yanapata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu, kama hali inayoonesha uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu kama sehemu ya mchakato wa kudumisha haki, amani na ustawi wa wengi.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake kwa Siku ya kuombea amani duniani kwa mwaka 2010 alisema ukitaka kuvuna amani, linda mazingira, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutunza mazingira kama kielelezo makini cha amani.

Kardinali Turkson anasema kwamba, Biblia ni kitabu ambacho kinatoa dira na mwongozo wa utunzaji bora wa mazingira kwa mtu binafsi, familia na Jamii husika, kwa kuzingatia maadili, tasaufi, haki na wajibu wa kijamii. Lengo ni kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea kutishia amani na usalama kwa Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linawajibu na dhamana ya kuendelea kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira kama kikolezo cha amani duniani.

Vijana wanapaswa kurithishwa utamaduni wa kupenda, kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao yao kwa sasa na kwa ajili ya kizazi kijacho. Vijana wanakumbushwa kwamba, wamepewa dhamana ya kutunza mazingira na maisha yao kwa ujumla. Ni mwaliko wa kuachana na utamaduni unaokumbatia kifo, mambo yanayoharibu ekolojia ya maisha ya mwanadamu kutoka katika undani wake. Jamii inahamasishwa kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi. Mazingira pia ni kielelezo cha zawadi ya Mungu kwa binadamu, kama yalivyo maisha.

Ni matumaini ya Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani kwamba, vijana wataendelea kuwahamasisha vijana wenzao kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi.

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.