Imani inawajibisha na wala si kama urembo uliopambwa kwenye keki!
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 18 Agosti
2013 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewataka waamini
kuwa na subira katika majaribu na kuendelea kumtumainia Yesu Kristo, chanzo na kilele
cha imani yao.
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, waamini kwa namna ya
pekee kabisa wanaalikwa kumtaza Yesu Kristo ili kujenga na kuimarisha uhusiano na
Mwenyezi Mungu. Yesu ni daraja muhimu sana kati ya binadamu na Mwenyezi Mungu, kwani
Yesu ni Mwana Mpendwa wa Mungu na waamini ni ndugu zake Kristo.
Baba Mtakatifu
Francisko anakiri kwamba, Liturujia ya Neno la Mungu kwa Jumapili ya Ishirini ya Kipindi
cha Mwaka C wa Kanisa inachangamoto kubwa ambayo inapaswa kuangaliwa kwa makini kutokana
na ugumu wake. Yesu anawauliza wafuasi wake, Je, mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta
amani duniani? Moto unaozungumzwa na Yesu anasema Baba Mtakatifu ni imani ambayo imeletwa
na Yesu hapa duniani, inayomtaka mwamini kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza
katika maisha yake, kwa kutambua kwamba, Mungu ni upendo.
Kwa njia ya Yesu,
waamini wanapata fursa ya kuweza kumtambua Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa huruma
na upendo; mkweli na mwaminifu na kwamba, ni chemchemi ya maisha kwa ajili ya wote.
Kutokana na mantiki hii, Yesu anasema amekuja kuleta mgawanyiko kati ya watu, kwa
kutambua kwamba, Yesu mwenyewe ndiye kiini cha amani na upatanisho wa kweli.
Amani
inayoletwa na Yesu inamtaka mwamini kumkana Shetani na mambo yake yote; kuachana na
ubinafsi, ili hatimaye, kuchagua jema, ukweli na haki hata pale ambapo mambo haya
yanahitaji sadaka kubwa pamoja na kujitosa kimasomaso. Mambo haya yanaweza kuwagawa
watu, lakini, Yesu ni daraja linalowaunganisha watu na wala si kinyume chake.
Yesu
anawapatia wafuasi wake vigezo msingi vya kufanya maamuzi yao katika maisha: kuishi
katika ubinafsi au kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza; kutumikiwa au kutumikia
wengine; kutii ubinafsi au kumtii Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo maana halisi ya mfarakano
ambao Yesu anazungumzia katika Injili.
Baba Mtakatifu anasema, Yesu kamwe hakutoa
ruhusa ya matumizi ya nguvu kama njia ya kueneza Imani, bali nguvu ya Wakristo inajikita
katika ukweli na upendo unaopinga matumizi ya nguvu kwani imani na vita ni mambo mawili
yanayosigana kimsingi; lakini imani na nguvu ni sawa na chanda na pete kwani ni mambo
yanayofumbata upole ambayo ni nguvu ya upendo.
Baba Mtakatifu Francisko anasema,
hata kwa baadhi ya ndugu na jamaa ya Yesu walisigana kuhusu maisha na utume wake kama
ambavyo yanasimulia Maandiko Matakatifu. Lakini Bikira Maria alimwelewa, akaukazia
macho Moyo Mtakatifu wa Mwana wa Aliye Juu na utume wake. Ni kutokana na imani thabiti
iliyoshuhudiwa na Bikira Maria, hata ndugu zake wakajikuta wakiwa ni kati ya wafuasi
wa kwanza wa Yesu waliounda Jumuiya za kwanza kwanza za Wakristo.
Baba Mtakatifu
anawaalika waamini kumkazia macho na hatimaye kumfuasa Yesu Kristo hata pale ambapo
kuna gharama kubwa, kwa kutambua kwamba, kumfuasa Yesu kunahitaji kujitosa kikamilifu
kwani imani ni nguvu ya moyo na kamwe si kama urembo unaowekwa kwenye keki!
Mara
baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbuka wahanga wa
ajali ya Meli iliyotokea nchini Manila na hivyo kusababisha watu wengi kupoteza maisha
yao. Hadi kufikia Jumapili mchana, miili ya watu 31 ilikuwa imekwishapatikana na watu
wengine 170 hawajulikani waliko.
Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii pia kuwaalika
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Misri.
Ametambua uwepo wa makundi mbali mbali ya waamini na mahujaji kutoka sehemu mbali
mbali za dunia waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
mjini Vatican.