Asiyekuwepo
na lake halipo. Baada ya kifo cha Yoshua kunatengenezwa ombwe la utawala na uongozi.
Waisraeli hawana tena kiongozi. Na taifa linakosa mwelekeo "there is no sense of direction".
Watu wanaanza kujichanganya na malimwengu. Wanaanza hata kuabudu Mungu wa Mabaali.
Wanamsahau Mungu aliyewakomboa na kuwapatia nchi ya ahadi.
Mungu anawaahidi
kupata Waamuzi watakaokuwa majemedari wa vita katika sehemu mbali mbali mtawanyiko
katika nchi zima ya Israeli kama vile Gideon, Samson, Debora na wengine.
Fundisho
moja kwetu sisi, tujifunze kuwa hata katika nafasi za kukosa kiongozi wa kiroho kwa
Misa takatifu au ibada kwa muda fulani, sisi tubaki na tabia ya kuwasiliana na Mwenyezi
Mungu daima. Tuwe na sala zetu za rohoni pamoja na tafakari ya kina ya Rozari takatifu,
Muhtasari makini wa Injili; Mawaridi ya sala au sala ye yote ya tafakari na Neno la
Mungu. Tusiingize kisingizio cho chote cha kumuacha Mungu.
Katika somo la Injili
: Mt 19:16-22, Yesu anamwambia kijana mmoja -
"nenda ukauze vitu vyote, uwape
maskini na utakuwa na hazina mbinguni kisha njoo unifuate.." Tunaambiwa katika Injili
kuwa kijana aliondoka kwa huzuni nyingi sana.
Leo Aug 19 tunaambiwa na Kristu
mambo haya :
Katika maisha ya binadamu muda wetu ni mali sana. Jumapili iliyopita
nilikuwa kwa Semina ya viongozi wa Halmashauri wa walei parokia ya Chang'ombe. Kilio
cha wana semina wengi kilikuwa juu ya mahudhurio hafifu ya wana jumuiya katika vikao
hasa akina baba. Kila mmoja anaweza kujisifu nina ndoa, natoa zaka, nasaidia Kanisa
kwa michango.
Lakini Kristo anakuomba leo, uza muda wako ukawape maskini katika
jumuiya yako. Hakuna zawadi kubwa katika maisha ya jumuiya inayowanyanyua wana jumuiya
wote zaidi ya kuwa nao na kukaa nao. Zawadi ya "To be there, and to be with them"
Jumuiya zetu zina watoto, maskini, walala hoi waliokata tamaa ya maisha. Uwepo wetu
ni uwepo komboi "saving presence" kama nabii Isaya asemavyo "Roho wa Bwana yu juu
yangu, amenipaka mafuta ili niwahubirie maskini habari njema.."(Isaya 61:1-3). Sisi
tupo hivi na tunakuwa hivi kwa sababu ya jumuiya zetu (John Mbiti).
2. Tuweke
mkakati na mpango wa kuuza vipaji vya akili na maarifa Parokiani. Panga programu za
kufundisha hesabu, Fizikis, Kemia, au uongozi na utawala bure. Katika dunia inayotegemea
kulipwa kwa vipindi vya "tuition", sisi tufanye tofauti kidogo. Tuuze na kuwapa watoto
ambao wazazi wao hawawezi kutoa cho chote. Najua wengi tutanuna tukiombwa kufundisha
bure kwa vile elimu ni yetu ni mali na tumeipata kwa shida. Sote tutaondoka kwa huzuni
na kuwaacha watoto wakifeli na kutupa lawama zote kwa NECTA.
3. Jitihada ya
kuuza utajiri wetu ni kujinyenyekeza na kujifananisha na watu wengine. Ni kujibandua
na dhana kuwa utu wa mtu unatokana na kujirundikia kichuguu cha vitu vya dunia (materialism).
Utu, kwa maana sahihi na pana ni tokeo la roho iliyoshiba na kutajirishwa na Mungu
mwenyewe. Heri kwetu kama tu "maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.."
(Mt 5:3).
4. Kuuza vyote katika maanazizi (radical view) ni kupoteza kwa muda
kiasi kidogo, ila kurudishiwa mara mia kwa baraka na neema za Mungu - "tafuteni kwanza
ufalme wa mbingu, mengine yote mtapewa kwa ziada.." (Mt 6:33). Kutafuta ni kukana
ya kidunia, na kupewa ni kumiminiwa mibaraka kutoka mbingini.
Tusali leo kwa
ajili ya mioyo yetu isitengeneze ombwe la kutokuwa na Mungu. Mungu ajaze kila sehemu
ya maisha yetu. Na tuombe kuonja uchungu wa kuuza kizuri tulichonacho ili kuwainua
wengine wanaotuzunguka ambao wanaokandamizwa na umaskini na ulala hoi.