2013-08-19 09:53:57

Changieni kwa hali na mali ili kufanikisha mkutano mkuu wa AMECEA 2014


Askofu mkuu Tarcisius Ziyaye, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi na Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitokeza kwa ajili ya kuchangia kwa hali na mali ili kufanikisha Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa AMECEA unaotarajiwa kufanyika mjini Lilongwe kuanzia tarehe 16 Juni hadi tarehe 26 Juni 2014. Mkutano huu utaongozwa na kauli mbiu "Uinjilishaji Mpya kwa njia ya wongofu wa ndani na ushuhuda wa imani ya Kikristo".

Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa AMECEA kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, linasema, hapo tarehe 6 Septemba 2013 kutafanyika tamasha la muziki wa kukata na shoka utakaovishirikisha vikundu maarufu kutoka Malawi kwa ajili ya kuchangisha fedha za kugharimia mkutano mkuu wa AMECEA ambao kwa mara ya tatu utafanyika nchini Malawi tangu AMECEA ilipoanzishwa kunako mwaka 1961, zaidi ya miaka 50 iliyopita.

Kwa mara ya kwanza Kanisa Katoliki nchini Malawi lilikuwa ni mwenyeji wa Mkutano wa AMECEA kunako Mwaka 1979, mkutano ambao ulifanyika mjini Zomba. Maaskofu wa AMECEA wakarudi tena nchini Malawi kunako Mwaka 1995, mkutano ambao ulifanyika mjini Mangochi.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi ambaye pia Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ndiye Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA.








All the contents on this site are copyrighted ©.