2013-08-19 09:34:13

Amani duniani katika haki!


Baraza la Maaskofu Katoliki India, Jumapili iliyopita limeadhimisha Siku ya 30 kwa ajili ya kuombea amani nchini India. Kauli mbiu ya Maadhimisho haya kwa mwaka huu ni “Amani duniani katika haki”. Mada hii imechaguliwa kwa makusudi kama sehemu ya mwendelezo wa Maadhimisho ya Waraka wa Kichungaji ulioandikwa na Papa Yohane wa XXIII, “Pacem In Terris”, Amani Duniani na kutiwa mkwaju hapo tarehe 11 Aprili 1963.

Baraza la Maaskofu Katoliki limewakumbusha waamini na watu wenye mapenzi mema nchini India umuhimu wa Mafundisho ya Waraka huu katika mchakato wa kukuza, kudumisha na kuendeleza misingi ya haki, amani na mshikamano miongoni mwa Jamii.

Dunia mpya inasimikwa katika misingi ya ukweli, upendo na uhuru. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Yohane wa XXIII alivyobainisha katika Waraka wake wa Amani Duniani na kwamba, amani inapatikana pale tu: haki msingi, mahusiano, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu vinatambuliwa na kuthaminiwa. Waraka huu unafafanua kwa kina maana ya haki msingi za binadamu kuwa ni mambo yote yanayofumbatwa katika haki msingi za binadamu.

Ili amani na utulivu viweze kutawala miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa na Kitaifa, kuna haja ya kukuza na kudumisha msingi wa majadiliano na kwamba, vita na kinzani ni mambo ambayo yamepitwa na wakati kwa sasa kama njia ya kuleta suluhu ya matatizo ya kijamii. Haki inapaswa kueleweka kuwa ni utambuzi wa kweli wa utu wa mwanadamu unaohitaji kulindwa dhidi ya mashindano ya utengenezaji wa silaha za mahangamizi.

Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusitisha utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za mahangamizi ambazo zinaweza kuleta maafa makubwa kwa binadamu. Ujumbe huu ni muhimu kwa India ambayo ni mnunuzi mkubwa wa silaha kutoka nje na kwamba, India hivi karibuni ilijitoa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa silaha za mahangamizi.

Baraza la Maaskofu Katoliki India linasema, yamekuwa ni Mapokeo ya Kanisa Katoliki nchini India kuadhimisha Jumapili ya kuombea haki, kila jumapili inayofuatia baada ya Maadhimisho ya Uhuru wa India. Baraza la Maaskofu Katoliki India kunako mwaka 1983 katika mkutano wao uliofanyika mjini Bombay uliamua kwamba, Kanisa nchini India liadhimishe Jumapili ya Kuombea Haki, kama sehemu ya mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kutambua changamoto zinazoikabilia haki nchini India.

Mwaliko huu unakwenda sanjari na Sheria za Kanisa zinazomtaka kila mwamini kuhakikisha kwamba, anakuza na kuendeleza haki jamii mahali anapoishi; shughuli hii itekelezwe na viongozi wa Kanisa mintarafu kweli na moyo wa Kiinjili kuhusiana na masuala ya hakijamii.








All the contents on this site are copyrighted ©.