2013-08-17 09:27:59

Mikakati ya Caritas DRC katika maboresho ya maisha ya watu wasiokuwa na makazi maalum!


Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini DRC limekuwa ni kielelezo cha upendo wa mshikamano unaoongozwa na kanuni auni pamoja na upendo kwa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum, ili kupata uhakika wa usalama wa maisha, chakula na makazi.

Caritas nchini DRC hivi karibuni imeanza kutekeleza mkakati unaopania kuwajengea watu wasiokuwa na makazi maalum wapatao 22,000 uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku. Katika mikakati yake, Caritas imeanza kuwapatia wananchi uwezo wa kujenga nyumba bora na imara zaidi; inaendelea kuimarisha uwezo ili kujitosheleza kwa chakula kwa kuwapatia pembejeo za kilimo pamoja na mafunzo ya kilimo bora na chenye tija. Wananchi wakiweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa ajili yao na familia zao, mambo mengine yanaweza kuboreka.

Mradi huu mkubwa unaendeshwa kati ya Caritas DRC na Caritas Ubelgiji na kwamba, walengwa wakuu ni wananchi wanaoishi katika Maeneo ya Dongo, Songo na Sabasaba yaliyoko Jimboni Budjala na eneo la Bobito Jimboni Molegbe. Itakumbukwa kwamba, watu wasiokuwa na makazi ya kudumu nchini DRC ni wengi sana kutokana na vita na kinzani za kijamii zinazoendelea nchini humo. Vita imeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kilimo na uzalishaji, jambo ambalo linatishia usalama na uhakika wa chakula hata kwa siku za usoni.







All the contents on this site are copyrighted ©.