Mazoea yakizidi sana huleta dharau.
Waisraeli wameanza kumzoea Joshua na watumishi wa Mungu wana wa Haruni. Wamezoea sadaka
zao na sanduku la Agano. Katika utulivu wa nchi ya ahadi hakuna jipya tena. Wanaanza
kuvutika na miungu mwingine. Wanataka kuuacha mbacha kwa msala upitao. Yoshua anawaambia
chagueni ninyi wenyewe nani wa kumtumikia. ".. Lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia
Bwana" (Yoshua 24:14-29).
Leo Agosti 17, 2013: - Mungu kwa kinywa cha Yoshua
anataka kusema,
1. Mungu daima kwetu sisi lazima kila siku awe mpya. Tusidhani
kuwa kwa kusoma masomo Kanisani, kwa kuimba kwaya au kuwa kiongozi parokiani tumekwishamjua
Mungu. Hata kama tukilala na kuamkia Kanisani tumche Mungu kwa uzito wote na kutetemeka
kana kwamba tumemjua Leo. Njia za Mungu daima huwa hazichunguziki.
2. Kumtumikia
Mungu kunahitaji familia zima ihusike. Baba ahakikishe watoto wanafuata utaratibu
na nidhamu ya nyumbani ikiwemo kusali. Na ndio maana ”Shema Israel” (Kumb 6:4) ilimtaka
baba wa familia awafundishe watoto wake kumpenda Mungu. Baba anamtumikia Mungu na
watoto wake anaposali nao kabla ya kulala, anapokwenda nao Kanisani na kushiriki shughuli
nyingine za kikanisa. Baba akienda, watoto wote watafuata.
3. Kuna familia
zetu ambazo zina wasichana wa kazi nyumbani ambao ni Wakristo na tena Wakatoliki,
lakini Jumapili wanazuiwa kufika Kanisani. Siku za jumapili ndio wanatoa nguo zote
za kufua na kumpatia ”house girl”. Au kwa familia nyingine wasichana wengine huwa
hawajapata Komunio ya kwanza au Kipaimara. Ni jukumu la wenye familia kuhakikisha
kuwa wasichana hawa wanafuata mafundisho na kupata huduma ya Sakramenti pindi wakiwa
katika kazi. Hii ni kuhakikisha nyumba yote inamtumikia Bwana. Na pia kutimiza vizuri
amri ya kushika kitakatifu siku ya Bwana ambapo hata mjakazi hakutakiwa kufanya kazi
(Kutoka 20:10)
Somo letu leo la Injili - Mt 19:13-15, Kristo anaonesha na
kukumbusha wajibu wa wazazi kwa watoto. Kuna wazazi ambao hawali chakula na watoto
wao, hawaongei nao, hawakagui na kukagua daftari zao. Watoto wanakua na hisia za kuachwa,
kukataliwa na kutopendwa. Watoto daima huwa wanaguswa sana na hisia za mguso "sense
of touch". Mguso wa baba au mama huwaachia hisia za usalama, upendo na kujaliwa. Na
ndio maana Kristo, huku akiwashika na kuwabariki watoto akasema - "waacheni watoto
wadogo waje kwangu.." au kwa lugha ya Kimakonde - "Valeke vadyoko vidikidiki vaide
kwangu.."
Bwana Yesu anataka kusema na familia zetu yafuatayo :
1. Dini
ya kwanza ya watoto ni kupendwa, kutunzwa na kujaliwa na wazazi wao nyumbani. Hii
ni katekesi ya kwanza ya msingi kwao. Tunapomfundisha mtoto kuwa Mungu atupenda, ni
lazima mtoto awe ameonja kwa nafasi ya kwanza kutoka upendo wa wazazi wake. Daima
tunalaumu watoto wa siku hizi hawajui dini. Kumbe, tatizo ni kuwa sisi kama wazazi
tulishindwa kuwaonjesha dini ya kwanza kwao - kuwapenda na kuwakumbatia kama alivyofanya
Yesu.
2. Wajibu wa wazazi ni kuwapa watoto viashiria vingine vya upendo -
yaani, kuwalisha chakula vizuri, kuhakikisha wanalala mahali pazuri, wanavaa nguo
nzuri na mahitaji mengine. Kufanya hivi kunahitaji wazazi kujinyima. Mtoto hawezi
kula matunda au mboga nzuri kama baba ataendekeza bia na nyama choma katika viti virefu
baa. Kuwalisha watoto vizuri ni sadaka kubwa kwa familia ye yote. Hivyo, unapoongeza
bia ya nne au ya tano ujue wazi unaacha kuwakumbatia watoto wako.
3. Mtoto
akipendwa vizuri ni rahisi naye kuwapenda na kuwaheshimu wazazi. Mtoto atatimiza
amri ya nne ya Mungu kiurahisi kwa vile atakuwa ameonja utamu wa utii toka kwa wazazi.
Na mwisho tuwaonye watoto wetu kwa upole. Hasira na vipigo vya kupitiliza huwaharibu
kabisa watoto wetu.
Tusali kwa ajili ya watoto ambao wapo katika familia zenye
matatizo. Wazazi hawaishi kugombana kila siku, mzazi mmoja ni mlevi pindukia, wazazi
wao wamefariki na shida nyingine. Bwana wakumbatie watoto hawa kwa upendo wako na
uwabariki wapate riziki ya kutosha na fukuto la Upendo kutoka kwako.
Fadre
Benno Michael Kikudo, Jimbo kuu la Dar es Salaam.