Utoto Mtakatifu nchini Madagascar wafanya kongamano la kwanza
Kwa mara ya kwanza Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar limehitimisha Kongamano
la Utoto Mtakatifu kitaifa, tukio ambalo limehudhuriwa na watoto 2,000 wenye umri
kati ya miaka 6 hadi 14 kutoka katika Majimbo 20 yanayounda Baraza la Maaskofu Katoliki
Madagascar.
Kongamano hili la kitaifa sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani
uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, limeongozwa
na kauli mbiu "Watoto wanaomwamini Yesu Kristo na kushirikiana kati yao ni vitalu
vya Kanisa". Tukio hili liliandaliwa na Tume ya Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki
Madagscar. Kwa siku nne mfululizo, wanachama wa Utoto Mtakatifu wamebahatika kupata
katekesi ya kina kuhusu: watoto na imani; mtoto na mabadiliko katika ulimwengu wa
utandawazi; haki msingi za mtoto mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Hizi
ni Katekesi zilizokuwa zinatolewa na Maaskofu kutoka Madagascar kwa ajili ya majiundo
makini ya watoto hawa ambao ni tumaini la Kanisa na Jamii kwa sasa na kwa siku za
usoni. Imekuwa ni nafasi kwa watoto hao pia kushiriki michezo na masuala mbali mbali
ya kijamii kadiri ya umri na nafasi yao.
Katika Ibada ya Misa Takatifu ya
kufunga Kongamano la Kwanza la Utoto Mtakatifu nchini Madagascar iliyoongozwa na Askofu
mkuu Jean Claude Randrianarisoa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar alisema
kwamba, shule ya kwanza yenye wajibu wa kurithisha tunu msingi za maisha ya kiimani,
kimadili na utu wema ni familia. Wazazi na walezi wanaendelea kuhamasishwa ili kuhakikisha
kwamba, wanashiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto wao katika: upendo,
msamaha na upatanisho.
Hizi ni mada msingi zinazoendelea kufanyiwa kazi na
Familia ya Mungu Barani Afrika, kama sehemu ya utekelezaji wa Maagizo ya Mababa wa
Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika. Baada ya Misa Takatifu, watoto wa Utoto
Mtakatifu nchini Madagascar wametumwa kuwainjilisha watoto wenzao kwa njia ya ushuhuda
wa mifano bora ya maisha, kwa maneno na matendo adili.