2013-08-16 10:15:58

Jitajirishe na Katekesi ya kina kuhusu Fumbo la Bikira Maria kupalizwa mbinguni!


Kanisa Katoliki popote duniani huadhimisha Sherehe ya kupalizwa Bikira Maria Mbinguni na kuwekwa kwake Malkia wa mbingu; Wamisionari wa Damu Azizi, huadhimisha siku ya kuanzishwa kwa Shirika lao; tukio lililofanyika katika Abasia ya Mt. Felix, kijijini Giano, mkoani Umbria, nchini Italia. Gaspari Del Bufalo ndiye mwanzilishi, ambaye aliliweka Shirika chini ya ulinzi wa Bikira Maria Mama na Malkia wa Damu Azizi. Na hatimaye, waamini wa Parokia ya Bikira Maria wa Damu Azizi inayojumuiisha maeneo la Kisasa na Nzuguni iliyoko katika Jimbo Katoliki Dodoma, huadhimisha siku ya somo wao.

Kupalizwa mbinguni kwa Bikira Maria ni fundisho pekee muhimu katika Kanisa?
Kanisa lafundisha na kuishi mafundisho kadha wa kadha ya kiimani. Saba kati ya hayo, ni mafundisho muhimu kiasi cha kusema "asiye yaamini na kuyaishi, sio mkatoliki wa kweli. Mafundisho au mafumbo hayo ni kama ifuatavyo:

· Utatu Mtakatifu: Kwamba Mungu wetu ni mmoja katika nafsi tatu; yaani; Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Hili ni fumbo msingi na ni fumbo mama la mafumbo mengine yote.
· Umwilisho: Kwamba Kristo Mungu aliyetwaa mwili wa kibinadamu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na kwa njia ya Bikira Maria, hivyo kuwa Mungu-kweli na Mtu-kweli.
· Ukombozi: Kwamba kwa mateso, kifo na ufufuko wake, Yesu Kristo ndiye Mkombozi pekee wa ulimwengu.
· Ekaristi Takatifu: Kwa mageuzi katika adhimisho la Misa Takatifu, lile Kristo aliloliadhimisha jioni ya Alhamisi Kuu, linatendeka tena; yaani, mkate na divai, hugeuka kuwa Mwili na Damu ya Kristo.
· Bikira Maria Kukingiwa dhambi ya asili: yaani, ili Yesu azaliwe, Mungu Baba aliandaa mazingiza kwa kumkinga Bikira Maria toka doa lolote la dhambi tangu tumboni mwa mamaye Anna.
· Bikira Maria Kupalizwa mbinguni:- yaani, Mungu, alimchukua mbinguni Bikira Maria mwili na roho.
· Bikira Maria Mama wa Mungu:- kwamba Maria ni Mama wa Yesu, Yesu ni Mtu-Mungu, hivyo, Maria aliye mama wa Yesu-Mtu pia ni mama wa Mungu.

4. Kuna mbinu iwezayo kutumika kuyakumbuka mafumbo hayo saba?
·Utatu - Umwilisho – Ukombozi- Ekaristi – Kukingiwa- Kupalizwa Mbinguni - Mama wa Mungu.
5. Juu ya Kupalizwa mbinguni Bikira Maria kuna angalisho la pekee?
· kwa kuwa Kupalizwa mbinguni ni moja ya mafundisho yenye hadhi ya kuitwa fumbo; yafaa, tutafakari na kuelewa vyema nini kinachoadhimishwa.

6. Je, nini maana ya Kupalizwa mbinguni?
·Kanisa Katoliki linaamini, linafundisha na kuhimiza kuwa: Bikira Maria baada ya kumaliza maisha yake hapa duniani, alipalizwa mbinguni, mwili na roho.
·Hii ni sherehe kubwa kuliko zote zinazoadhimishwa na Kanisa kwa heshima ya Bikira Maria.

·Na wasio Wakatoliki husema na kuuliza: kwa nini Wakatoliki mnamheshimu Maria kiasi hicho; ni kama kusema, eti tunamheshimu kupita kiasi au kuliko inavyostahili.
·Ukweli ni kwamba, kwa kumchagua Maria, kati ya vizazi au watu wote kuwa mama wa Mwanae wa pekee Kristo, Mungu alimheshimu Maria kuliko alivyowaheshimu wanadamu wengine wote na kuliko sisi tunavyoweza kumheshimu Bikira Maria.

·Ikiwa Mungu kamheshimu Maria kiasi hicho, cha kuwa Mama wa Mwanaye wa pekee, cha kuwa Mpalizwa mbinguni- mwili na roho, kwa nini sisi tusimheshimu kwa namna tufanyavyo na hata zaidi ya hivyo?

· Tujiulize: kwa nini tusimpende mama yetu? Je, mtu akimdharau mama yako mpendwa, huyo atakuwa bado rafiki yako?

· Maria ni mama wa Bwana wetu: alimzaa, alimtunza, hadi kufikia utu uzima, na akabaki chini ya msalaba siku ile Yesu alipoinuliwa, yaani, kusulibiwa na kufa msalabani. Anastahili sio tu heshima (reverence) bali heshima kubwa (veneration) pasipo kuvuka mipaka ya kumpa heshima ya kumwabudu (adoration).

· Na tunapomwendea, tukiomba msaada wa maombezi yake, Maria hufikisha maombi na sala zetu kwa Mwanae, na kama arusini Kana, Mwanae Kristo hutujalia ili mradi ombi liendane na matakwa ya Baba wa mbinguni ya kumkomboa mwanadamu.
· Basi tuzidi kumpenda na kumsifu Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni kwa kuimba Zab. 45:9.

7. Nini asili au msingi wa fundisho juu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni? (Au fundisho fundisho hilo lilitujia vipi?)
· Kwa hakika:- fundisho halikubuniwa au kuzushwa na viongozi wa Kanisa Katoliki kama baadhi ya wazushi na wapinzani wanavyofikiri. Msingi wake ni wa kweli kama ifuatavyo:

· Maandiko Matakatifu: sambamba na nia ya Mungu ya kumkomboa mwanadamu toka dhambi na mauti, Maria alikuwa katika mpango na wazo la Mungu tangu milele na kutabiriwa katika Agano la Kale kama isomekavyo katika Mw. 3:15 na Is. 7:14. Maria aliheshimiwa na Mungu kiasi cha kuteuliwa kuwa Mama wa Mkombozi, kama isomekavyo katika Gal. 4:4-5. Maria alishirikishwa ipasavyo na kikamilifu katika mpango huo wa Ukombozi, naye Kwa hiari pasipo shuruti, alikubali na alitekeleza; hivyo, ilimpendeza Mungu kuwa Maria atawale mbinguni pamoja na Mwanae Mkombozi Yesu Kristo.

· Mkingiwa Dhambi ya Asili: hivi ni nani baada ya kujijengea nyumba nzuri apate kukaa ndani yake atamruhusu adui yake kutangulia kuingia na kukaa humo? Ni swali awekalo mbele yetu Mt. Sirillo wa Alexandria; kwamba Mungu alimwumba Maria, akamchagua tangu milele awe mama wa Mkombozi; ingekuwa ajabu kama angemruhusu shetani akae rohoni mwa Bikira Maria; ndio maana, Mungu alimkinga dhidi ya dhambi ya asilli; hivyo yeye aliyezaliwa bila dhambi ya asili, hakustahili mwili wake uoze kaburini.

· Maria ni mshiriki katika kazi ya ukombozi:- Alipo Yesu yuko Bikira Maria; mama Maria aliambatana na Yesu akashiriki taabu na raha. Maria alichukua mimba na kumzaa Yesu; Maria na Yosefu walilazimika kumtwaa mtoto Yesu na kukimbilia Misri kumwepusha mtoto na mauaji ya Herode; alikuwa naye arusini Kana; aliambatana naye katika njia ya mateso kuelekea Kalvari; alibaki chini ya msalaba baada ya kusulibiwa Yesu; alipokea maiti ya mwanae na kumzika; Maria aliyeshiriki nyakati za ukombozi; Maria aliyeambatana na Yesu katika nyakati za Mungu kudhihirisha pendo la ukombozi; alistahili kushiriki utukufu wa Mwanae.

8. Fundisho au tamko rasmi juu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni linasemaje?
· Kutokana na sababu hizo za msingi na baada ya kupata ridhaa ya maaskofu Katoliki duniani kote; ilimpendeza Mungu, Kanisa na wote wenye mapenzi mema, kuwa tamko rasmi litolewe.
· Hivyo, saa 3 asubuhi, jumatano ya tarehe mosi Novemba, mwaka 1950; mbele ya maaskofu 700 na waamini takribani laki 6 hivi, askofu wa Roma, khalifa wa Kristo, mchungaji mkuu wa duniani wa Kanisa Katoliki, Baba Mtakatifu Pio XII, alitoa tamko rasmi juu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho.

· Papa Pio XII katika tukio hilo, alisema: "kwa sababu hii, baada ya kumtolea Mungu sala na maombi ya kudumu, na baada ya kuomba mwanga wa Roho wa kweli, tunataarifu, tunadhihirisha, tunaeleza wazi kabisa na kutangaza kuwa; ni ufunuo wa imani, kwamba, Mama safi wa Mungu, Maria Bikira daima, baada ya maisha yake hapa duniani, alipalizwa mbinguni mwili na roho katika utukufu wa mbinguni.

9. Kuna tofauti gani kati ya kupaa na kupalizwa?

·Ni muhimu kutofautisha hayo mawili. Yesu kwa kuwa yeye ni Mungu na hivyo alikuwa na nguvu yake mwenyewe kurudi kwa Baba, alipaa mbinguni; bali, Bikira Maria (japo kuwa alijitahidi kuishi katika neema) kama wanadamu wengine, hakuwa na uwezo wa kuelekea mbinguni- hivyo alifika huko kwa kuwezeshwa na Mwanae Kristo; na huko ndiko kupalizwa mbinguni.
· Kuhitimisha tafakari hii mambo mawili tunaalikwa kuyafanya: kufahamu faida za tukio la Bikira Maria kupalizwa mbinguni na kubainisha sala ifaayo kumtolea Bikira Maria.

10. Sherehe ya kupalizwa Bikira Maria inatufundisha nini:
· kwanza, mwanadamu akishirikiana na neema ya Mungu, anaweza kuishinda dhambi; anaweza kuyashinda mauti;
· pili: ni ishara ya matumaini kwetu- wanadamu tumeahidiwa kushiriki furaha na utukufu wa Kristo mfufuka; siku moja tutashiriki utukufu wa Kristo; lakini, baada ya kustahimili kwa imani, dhiki, mateso, madhulumu ya hapa duniani.
· Tatu: Maria ni mwombezi na mgawaji wa neema- kwani Maria ni mama wa msaada na huruma, na kazi yake ni kutuombea ili stahili za Kristo zitufikie; dhambi zetu zisamehewe; na hatimaye tupate uzima wa milele.
· Nne Bikira Maria, kama mama yeyote mwema, yuko tayari kumsaidia yeyote anayemkimbilia katika mahangaiko yake- kama tunavyosali katika sala ya memorare: "kumbuka ee Bikira mpole sana, haijasikilika bado hata mara moja, kwamba ulimwacha mtu aliyeukimbilia ulinzi wako, aliyeomba msaada wa maombezi yako”; je, tunamtumia kweli mwombezi huyu mkuu?
· Tuzidi kumwomba Bikira Maria mpalizwa mbinguni- ili tuweze kupata neema ya ukombozi toka kwa Mwanae Kristo.


11. Kuna uhusiano gani kati ya Maria Mpalizwa mbinguni na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu?
· Wamisionari wa Damu Azizi:- Ni Shirika la mapadre na mabruda, lililoanzishwa na Padre wa Jimbo la Roma, Gaspari del Bufalo, na alilianzisha rasmi katika tarehe 15 Agosti 1815 hivyo siku ya sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni.
· Licha ya maisha yao kusimama juu ya nguzo au mihimili mitatu, yaani, Tasaufi ya Damu, Maisha ya Jumuiya na utume;
· Kutokana na uhusiano wa Damu ya Yesu na Maria, wanamtambua Bikira Maria Mama wa Damu Azizi kuwa msimamizi mkuu wa Shirika;
· Na kutokana na mwanzilishi wao kuvutiwa na uinjilishaji wa Mt. Fransis Ksaveri, basi wanamtambua Mt. Francisko Ksaveri kama msimamizi wa utume wao.

12. Tasaufi na ibada kwa Damu Azizi ina maana gani?
· Katika Kanisa, kuna ibada nyingi, nzuri na takatifu. Kati ya hizo kuna moja ya pekee inayompendeza Mungu, ndio ibada kwa damu ya Kristo.
· Sisi tunaomfahamu na kumwadhimisha Bikira Maria, Malkia wa mbingu, tunapaswa kumpenda na kuendeleza ibada hii ya thamani na muhimu kwa wokovu wa roho zetu.
· Tena kwetu, hili sio tu jambo jema, na wajibu wetu kumtambua Kristo, ambaye kwa Damu yake iliyomwagika katuonesha pendo la pekee la Baba wa mbinguni kwa mwanadamu.
· Kwa sabau hiyo, ni kosa la aina gani tutakuwa tumefanya kumsherehekea Maria pasipo kuikumbuka ibada kwa damu Azizi ya Yesu. Damu ile ilitotoka kwa Maria, kwa mapendo ya kimama alimshibisha Yesu alipokuwa tumboni mwa mamaye.

13. Ni kipi kielelezo cha uhusika wa Maria kwa Damu ya ukombozi?
· Sala ya Wamisionari wa Damu Azizi kwa Maria Mama wa Damu Azizi ni kielelezo cha kutosha; nayo inasema:

Tunakuheshimu Maria kwa kuwa Mungu amekuteua kati ya wanawake wote kuwa Mama wa Mwanawe. Kwake yeye, wewe ni kalisi safi na takatifu, kwa kuwa kwa njia yako ameiepusha dhambi ya asili, na pamoja nawe ameanzisha uumbaji mpya.

Unang’aa na kuangaza kwa usafi wa moyo wako. Wewe ni tunda la kwanza la ukombozi, ulioustahili kwa Damu ya Mwanao, hata kabla ya Yesu kuwa mtu ndani yako. Mungu amekutajirisha kwa njia ya pekee, ili uweze kutekeleza mpango wake bila kikwazo. Hivyo ulimkubalia kuwa Mama wa Mkombozi.

Bila kuweka masharti ulifuata hatua kwa hatua mapenzi ya Mungu kwa imani isiyotikisika. Ilikuwa njia ya majaribu, ya matukio yasiyotazamiwa, mwendo wa imani; hivyo ukajikuta mwenyewe juu mlima Kalvari, mbele ya Mwanao aliyetapakaa Damu, baada ya kufuatana naye maishani, na katika njia yake ya kuelekea msalaba.
Tunakupenda, ewe Mama chini ya msalaba, Mama wa Damu Azizi, kwa sababu mlimani Kalvari ulikuwa Mama yetu sote. Damu ya Yesu, iliyotoka kwako ulipompa mwili wa kibinadamu, ni damu ya ukombozi inayotiririka kutoka msalabani; hivyo wewe, Mama wa mwili wa Kristo, pia ni Mama wa Kanisa.

Tunatamani kukupenda wewe na Mwanao, na kukuheshimu kama Mwanao alivyofanya katika maisha yake, alipokuwa mtoto na mtu mzima. Pamoja naye tunapenda kushiriki maumivu yako na pia furaha zako. Mama, tuonyeshe namna tutakavyokupenda zaidi na hata kujisikia wanao na kukamilika ndani mwako zaidi.

Kwa kuwa Yesu alimwaga damu yake kwa ajili ya wote, hata moyo wako uko wazi kwa wenye matumaini, kwa waliotengwa, waliokata tamaa na wasiopendwa.

Tunataka kujiunga nawe Mama mwenye huruma kwa wote. Pamoja nawe twataka kutuliza na kusaidia binadamu, kwa kuwa wewe uko karibu hata na wale wasiokufahamu au kukuelewa.

Kaa karibu nasi, Mama wa Damu Azizi, ili tuwe karibu na hao unaowapenda sana. Tupatie imani yako, tukubali kuongozwa na Roho Mtakatifu, kama ulivyofanya wewe.
Utupatie unyenyekevu wako, ili tuwatumikie wale ambao Yesu alikufa kwa ajili yao. Tujalie msalaba wako, ili tuweze kuwa na huruma kama yako kwa wale wanaoishi bila neema.

Maria, Mama yetu, utusaidie kuchukua nafasi yako katika dunia hii, ili Yesu zaidi na zaidi apate kuishi kati ya watu na ufalme wake ukue. Utusaidie kufuata mfano wako ili tujitoe wenyewe pamoja na Damu ya Kristo, kwa utukufu wa Mungu Baba na kwa wokovu wa ulimwengu mzima. Amina.


14. Ulimwengu wa sanaa unawahusianisha vipi Bikira Maria, Yesu na Mt. Gaspari Del Bufalo?
14.1. Mama Maria na Damu ya Ukombozi:

·Wachoraji mbali mbali wameonesha katika picha zao namna wote wawili, yaani, Yesu na Maria wanavyochangia katika kikombe cha ukombozi.
· Huko Bersanzone Italia, wanaiheshimu picha ambamo Maria anapokea katika chombo kichanya cha zabibu; na huko Geneva- nchini bado Italia, wanaiheshimu picha inayomwonesha Maria akimkabidhi Yesu zabibu.
· Vielelezo hivi viwili, ni msaada mwingine kulielewa na kulieleza fundisho juu ya Maria Mama wa Damu Azizi.

· Picha ile ya pili, yaani, Maria kumkabidhi Yesu zabibu, inamkumbusha Yesu, jinsi mama yake alivyofanya matone ya damu yatiririke. Matone hayo yatakusanywa katika kalisi;
· Na katika picha ya kwanza, Yesu anapomkabidhi mamaye zabibu, ishara ya kumwahidi Maria kuiweka Ekaristi inayofichika katika maumbo ya divai.

14.2. Mama Maria na Gaspari Del Bufalo:
·Huko Rimini, mji ulioko Italia, katika Madhabahu ya Malkia wa Huruma, katika kikanisa kidogo cha Mt. Gaspari, kuna kielelezo kingine bayana. Maria anaoneshwa akimkabidhi kalisi padre Gaspari, ili kumtia moyo aeneze ibada kwa Damu Azizi ya mwanae Yesu; naye Gaspari, akijidhatiti katika utume huo, kiasi cha kuhitimisha maisha yake katika miaka 51 tu, kwa kujituma katika kazi, akitolea uwezo na karama zake zote za kipadre kwa Kristo na wale aliokabidhiwa na Kristo, hasa wanyonge na wagonjwa; Gaspari alitoa maisha yake kama ishara ya kuungana na sadaka ya mwana wa Maria, sadaka ya Kristo msalabani.

· Gaspari alipenda watu wote wamfuate Kristo; akithibitisha kwa kwa kubeba katika safari za kuhubiri picha ya Mama aliyembeba mtoto mwenye kushika kalisi na kwa kuamini kwa dhati kuwa damu ya Kristo ni silaha imara ya kuyashinda mauti na nguvu zote za giza au kishetani; na katika hili alipata uthibitisho.

15. Damu ya Kristo ina nguvu gani katika maisha ya watu?
·Licha ya miujiza mingi aliyoitenda Mungu kupitia Gaspari Del Bufalo alipoomba kwa jina la Damu ya Kristo, mwaka 1836, yaani mwaka mmoja kabla ya kufa kwake Gaspari Del Bufalo, mtawa mmoja wa kike, wa monasteri ya Priverno ya huko Italia- alisumbuliwa na sauti zilizosikika daima katika makazi yake. Gaspari alipokwenda kuhubiri katika mji huo, mtawa huyo alimwomba Gaspari anyamazishe sauti hizo zinazomsumbua.

Naye Gaspari alimshauri aandike juu ya mlango wake maneno yafuatayo: "Viva il divin Sangue", yaani: idumu au isifiwe Damu Azizi; ndio maneno yaliyoonekana hata katika bendera aliyoibeba Gaspari alipokwenda kuhubiri. Baada ya mtawa huyo kutekeleza alivyoelekezwa na Gaspari, kelele sumbufu hazikusikika tena.

· Ni maneno hayo hayo, kwa amri ya Gaspari, kama zinavyoelekeza kanuni za Wamisionari wa Damu Azizi, maneno hayo lazima yaandikwe juu ya milango ya nyumba waishimo wamisionari wake; na yaandikwe juu ya milango ya wote wanaoiheshimu Damu ya Kristo kama Damu ya ukombozi.

· Gaspari aliye mtume wa Damu, na kielelezo cha heshima kwa Bikira Mpalizwa mbinguni, atuwashe kwa mapendo yale yaliyousukuma moyo wake kuwaelekea Yesu na Maria,; yaliyomsukuma kuanzisha shirika la Wamisionari, watakaohamasisha na kusambaza ibada kwa Damu Azizi.

16. Kwa nini Parokia ya Kisasa-Medeli-Nzguguni ishangilie kwa namna ya pekee sikuu ya kupalizwa mbinguni?
· Japokuwa parokia tajwa inajumuisha vigango vinne kwa sasa, yaani; cha Mt. Anna (Medeli), cha Mt. Maria De Mathias (Nyumba 300), cha Mt. Paulo wa Msalaba (Nzuguni Maweni) na cha Mt. Yohane Mbatizaji (Nzuguni Sokoine); Kigango cha Mt. Anna (Medeli) kinabeba historia iliyopelekea maeneo ya Kisasa na Nzuguni kuteuliwa na kutangazwa Parokia tena parokia yenye jina la Bikira Maria Mama wa Damu Azizi.

· Kigango cha Mt. Maria De Mathias kimezaliwa wakati huduma za kichungaji eneo hilo zikitolewa tayari na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu mnamo 2010; vigango vya Mt. Anna, Mt. Paolo wa Msalaba na Mt. Yohane Mbatizaji vilihudumiwa kwa miaka mingi na Parokia ya Kanisa Kuu, kisha Parokia ya Kiwanja cha Ndege, na hatimaye Parokia ya Makole.

· Mwaka 2002, Wamisionari wa Damu Azizi walianzisha jumuiya yao Kisasa ili kuhudumia Radio Mwangaza, Kijiji cha Matumaini na sehemu mbili zingine zilizotarajiwa kujengwa, yaani, nyumba ya Makao yao Makuu Tanzania na kituo cha kiroho, kilichobadilishwa baadaye kuwa kumbi za Mkutano na Hoteli ya Mt. Gaspari.

· Tangu wakati huo (2002) Wamisionari wa Damu Azizi walioishi na kufanya kazi kisasa, wakitambua wajibu wao msingi ni uchungaji wa roho, waliomba kibali toka parokia ya Makole kuhudimia kigango cha Medeli, huduma iliyoendelea hadi 2007, mwaka ambao eneo lililoombwa kuhudumiwa likajumuisha Nzuguni Maweni na Sokoine.

· Ujenzi wa nyumba 300 kwa ajili ya viongozi wa serikali pamoja na uwepo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kulipelekea uwepo wa Waamini wanafunzi na walimu wa chuo pia wafanyakazi wengine; ambao walianza kusali katika chapel ya Kijiji cha Matumaini, kisha ibada za Jumapili kufanyika nje ya nyumba zao kwa zamu na hatimaye kujenga Kanisa la kigango lililoanza kutumika mwaka 2011.

· Ikumbukwe kuwa, mwaka 2008, Askofu Ruwaichi aliwaomba Wamisionari wa Damu Azizi kusimamia uchungaji wa maeneo ya Kisasa-Medeli akitaja sababu za msingi za ombi hilo ikiwemo- wamisionari hao wana nyumba Kisasa, kwamba Jimbo la Dodoma ndilo lililowapokea walipokuja Tanzania mara ya kwanza hapo mwaka 1966 na kwamba hawakuwa na Parokia Dodoma.

· Ombi hilo la mhashamu Askofu lilijibiwa kwa ujumla mwaka huo 2008 na kwa namna ya pekee, mwaka 2010 wakipendekeza jina la parokia kumheshimu Maria, kwa namna anavyoheshimika katika shirika lao, yaani, Maria Mama wa Damu Azizi.
· Sambamba na Mhashamu Askofu Ruwaichi kufurahia ukubali wa wamisionari hao, aliridhia Parokia hiyo kuwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa Damu Azizi.

· Parokia ya Bikira Maria Mtakatifu wa Damu Azizi (The Blessed Virgin Mary- Our Lady of the Precious Blood) ilizaliwa rasmi hapo 2 Januari 2011, kwa mujibu wa Hati ya uzinduzi ya tarehe 1 Januari 2011 ya Mhashamu Askofu Jude Thaddeus S. Ruwaichi OFMCap, Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Dodoma; alitoa tamko hilo kwa kuzingatia Mkusanyo wa Sheria za Kanisa na. 515:1&3

Sambamba na tamko hilo, Mhashamu Askofu Ruwaichi alisema, mosi; Parokia hiyo ya Kisasa-Medeli, itajumuisha maeneo yafuatavyo, ambayo yote yanamegwa kutoka Parokia ya Makole, nayo ni: Kisasa, Medeli, Nzuguni Maweni na Nzuguni Sokoine; pili; Parokia ya Kisasa ni sehemu ya Dekania ya Mt. Paulo wa Msalaba; na tatu; aliwaagiza wanaparokia wa Kisasa kuzingatia: mosi, kuliheshimu agizo la Kristo la kupendana na kukuza umoja wa watoto wa Mungu.

Pili, kujituma kwa kufanya juhudi za dhati zenye lengo la kurithisha, kulea, kulinda na kuimarisha imani; tatu, kujitahidi kuela dhamiri na kujenga maadili bora miongoni mwa waamini wa marika yote; nne, kushikamana na kujituma katika juhudi za kuijenga parokia na kulitegemeza kanisa na utume wake mtakatifu; tano, kushirikiana na wadau wote wa uinjilishaji, wakiwemo wenye daraja, watawa na walei; pia, kukuza ushirikiano na ngazi nyingine za Kanisa kama vile Dekania, Vikarieti, Jimbo, nk; sita, kukuza na kudumisha sauti ya unabii na ushuhuda unaowapasa kila mmoja binafsi na wote kwa pamoja.

Makala hii imetayarishwa kutoka Radio Mwangaza FM
Dodoma, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.