2013-08-16 07:29:11

Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Malaria inatoa matumaini, lakini vuteni subira!


Shirika la Afya Duniani, WHO limepokea kwa mikono miwili taarifa iliyotolewa hivi karibuni na watafiti wa ugonjwa wa Malaria kutoka Marekani kwamba, wamefanikiwa kupata chanjo dhidi ya wadudu wa Malaria. Hii ni habari inayotia matumaini kwa mamillioni ya watu wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na ugonjwa wa Malaria hasa Barani Afrika. RealAudioMP3
Chanjo hii ambayo kwa sasa imepewa jina Pfspz imefanyiwa utafiti na majaribio huko Maryland, Marekani na kuonesha mafanikio makubwa, lakini watu waliofanyiwa majaribio ya chanjo hii walikuwa ni wachache, ndiyo maana Shirika la Afya Duniani linawataka watu kuvuta subira wakati ambapo juhudi zinaendelea kubainisha juu ya ufanisi wa chanjo hii.
Shirika la Afya Duniani linasema kwamba, hadi sasa kuna chanjo 20 ambazo zimefanyiwa utafiti katika hatua mbali mbali kabla ya kuthibitisha kwamba, zinafaa kwa ajili ya matumizi ya chanjo dhidi ya Malaria kwa umma mkubwa zaidi.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani kwa Mwaka 2010 zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 660,000 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Malaria. Waathirika wakubwa wa ugonjwa wa Malaria Barani Afrika ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano.








All the contents on this site are copyrighted ©.