Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Tanzania, Jaji Joseph Warioba amewataka
watu wenye ulemavu kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya katiba ili kuiwezesha Tume yake
kujua mahitaji yao na kuyafanyia kazi. Akizungumza katika siku ya kwanza ya mkutano
wa Baraza Maalum la Katiba kwa ajili ya watu wenye ulemavu mjini Dodoma Alhamisi,
Agosti 15, 2013), Jaji Warioba amesema Tume yake inatarajia kupata maoni mazuri yanayohusu
watu wenye ulemavu kutoka katika baraza hilo.
“Mtusaidie kupata maoni kuhusu
maeneo yote ya rasimu ya katiba yanayohusu watu wenye ulemavu,” alisema na kuongeza
kuwa hilo lisiwazuie kutoa maoni kuhusu maeneo mengine ya rasimu ya katiba.
“Nyie
pia ni sehemu watanzania na hata mkiwa viongozi mtakuwa viongozi wa watanzania wote...
kwa hiyo ipitieni rasimu yote na mtoe maoni katika maeneo yote pia,” alisisitiza Jaji
Warioba na kuongeza kuwa Tume yake pia iliandaa Baraza Maalum kama hilo Zanzibar kwa
kushirikiana na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ).
Akiongea katika
mkutano huo, Mkurugenzi wa Shirikisho la Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Bw. Novatus
Rukwago aliishukuru Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwezesha kufanyika kwa baraza
hilo na kusema kuwa mkutano huo umeshirikisha vyama vyote kumi vya watu wenye ulemavu.
Alivitaja
vyama hivyo kuwa ni Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo (CHAWATA), Chama cha Wasiiona
(TLB), Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Afya ya Akili (TUSPO) na Chama cha Watu Wenye
Ulemavu Walioumia Uti wa Mgongo Kilimanjaro (KASI).
Vyama vingine vinavyohudhuria
mkutano huo ni Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa
Mabaka ya Ngozi (PSORATA), Chama cha Albino Tanzania (CAT), Chama cha Watu Wenye Ulemavu
wa Akili (TAMH), Chama cha Viziwi Wasioona (TASODEB) na Chama cha Watu Wenye Ulemavu
wa Vichwa Vikubwa na Mgongo Wazi (ASBAHT).
Kuhusu Gharama za Muungano
Katika
hatua nyingine, Jaji Warioba amefafanua kuhusu gharama za uendeshaji wa muungano wa
shirikisho la Serikali tatu ambao umependekezwa na Tume yake katika rasimu ya katiba
iliyozinduliwa Juni 3, 2013. Akijibu swali la mjumbe mmoja wa Baraza hilo aliyeomba
ufafanuzi kuhusu gharama za uendeshaji wa Serikali ya Muungano ndani ya shirikisho,
Jaji Warioba amesema Tume yake imependekeza Serikali ya Muungano iendeshwe na mapato
yatakayotokana na ushuru wa bidhaa ambao unakua kila mwaka.
“Tumependekeza
chanzo hiki kikubwa cha ushuru wa bidhaa baada ya kupokea maoni ya wataalam na kujiridhisha,”
alisema na kufafanua kuwa mapato yanayotokana na ushuru wa bidhaa yanatosha kuendesha
shughuli za Serikali ya Muungano inayopendekezwa. Akiongea kuhusu suala hilo katika
mkutano huo, Mjumbe mwingine wa Tume hiyo Bw. Ally Saleh amesema kwa sasa mapato ya
ushuru wa bidhaa ni zaidi shilingi trilioni moja na kuwa maoni ya wataalam ambayo
Tume yake imeyapokea yanaonyesha kuwa kwa kiasi kikubwa mapato hayo yanakua kila mwaka.
“Kwa hiyo mapato haya ya ushuru wa bidhaa yanatosha kuifanya Serikali
ya Muungano ijisimamie na mapato mengine waachiwe washirika wa Muungano,” amesema.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea na mikutano ya Mabaraza ya Katiba ili kupokea
maoni kuhusu rasimu ya katiba. Mikutano hiyo inatarajia kumalizika Septemba 2 mwaka
huu.