2013-08-15 12:12:11

Waamini wa Parokia ya Castel Gandolfo wanasema wameguswa na maisha na utume wa Papa Francisko!


Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho ni kielelezo cha faraja na matumaini kwa waamini wanaosafiri katika mwanga wa imani. Ni maneno ya Padre Pietro Diletti, Paroko wa Parokia ya Castel Gandolfo, wakati alipokuwa anamkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa waamini na mahujaji waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Libertà.

Anasema, wamekuwa wakifuatlia matukio mbali mbali ya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa dhati na kwamba, wameguswa na mfano wa maisha, maneno na matendo yake, ambayo yanaendelea kuleta mwamko na ari mpya zaidi ya upendo kwa Kristo na Kanisa lake. Wamegundua msisitizo kwa Kanisa kuendelea kuwa kijana na umuhimu wa vijana kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa.

Mapadre wametakiwa kuwa karibu na waamini wao, ili waweze kuwasindikiza katika hija ya maisha yao ya kiroho, kwa kuwaonjesha furaha na matumaini ya watu wa Familia ya Mungu inayofanya hija ya pamoja na wala si katika upweke! Waamini wanaendelea kuguswa na unyenyekevu, uvumilivu na bidii inayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika kuwatafuta na kuwaganga wale waliopotea katika muda, wanaoogelea katika ulimwengu wa kufikirika; watu wanaokumbana na umaskini pamoja na hali ngumu ya maisha, ili wote hawa waweze kuonja mwanga wa matumaini mapya.

Padre Pietro Dilletti anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa maisha na utume wa Kanisa kwa vijana, kwani hili ni kundi ambalo linakabiliwa na changamoto mbali mbali za maisha, kiasi kwamba, linaanza kupoteza matumaini. Kama Parokia wanaendelea kuwekeza katika utume kwa vijana ili waweze kuwa na maisha, furaha na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Parokia pamoja na changamoto mbali mbali inaendelea kutweka hadi kilindini ili kufurahia matunda ya ushuhuda wa imani. Wamemhakikishia Baba Mtakatifu sala na sadaka yao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.







All the contents on this site are copyrighted ©.