2013-08-15 08:41:59

Vijana jitahidini kuwa na uzima wa Kimungu ndani yenu!


Karibu sana ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika makala hii ya vijana. Baada ya Baba Mtakatifu Francisko kutoa barua ya kitume Lumen Fidei, Mwanga wa Imani, kama kawaida yetu vijana tunaichangamkia maana ndani yake kuna mafundisho kabambe, yametulia kama maji ya mtungini, na utaona umuhimu wake pale tu unapoyatumia, kwani yanakata kiu yote ulionayo kuhusu Mwanga wa Imani yetu. RealAudioMP3
Katika Injili Kristo mwenyewe anasema “mimi ni Nuru ya Ulimwengu, aniaminiye hatabaki gizani bali atakuwa na nuru ya uzima” (Yohana 12,46). Kwanza hebu angalia maneno yanayokuvutia kwenye sentensi hiyo ya Kristo: kwanza mimi, yaani Kristu mwenyewe, halafu Nuru, Giza, kisha Uzima. Unajua kijana una hulka ya kuvutiwa na vitu, sasa mimi napenda kukufumbua macho namna ya kuchambua vinavyokufaa kati ya vile vinavyokuvutia, mambo ya ving’amuzi kama ujuavyo tena.
Kristo ni mwana wa Mungu aliye hai, Nafsi ya pili ya Mungu sawa na Baba. Vitu vyote vimeumbwa naye. Injili ya Yohana inatufundisha kuwa vitu vyote vimefanyika kupitia yeye (Rej. Yohana 1, 1-4). Kumbe, yeye Mungu, ni Muumba wako.
Nuru ni tofauti kidogo na mwanga. Mwanga ni miale inayoangaza ambayo athari yake yaweza kuwa chanya au hasi. Mfano mwanga wa jua una athari hasi machoni, una athari hasi kwa baadhi ya mimea. Wakati nuru ni miale ambayo athari yake ni chanya. Nuru inaondoa giza na kuleta muonekano wa vitu vile vinavyopaswa kuwa. Nuru haichomi, haiunguzi.
Kristo anaondoa giza katika ulimwengu huu, anatufunulia vile maisha yetu yanavyopaswa kuwa na kutuonesha njia ya imani inayotufaa. Nuru hii ya Kristu inatuletea sasa uzima.
Uzima ni uhai unaodumu, yaani maisha. Kuna wale wenye uhai, wanapumua lakini hawaishi. Yaani wapo wapo tu. Kristo anakupa uzima, yaani maisha. Ndani ya Kristo, imani thabiti kwake inakuelekeza namna ya kuishi vema na kufurahia maisha. Na maisha au uzima huu haukomi baada ya kifo, bali unakufanya udumu katika uzima wa milele.
Nakuona unavyokodoa jicho tu, najua unajiuliza kama na wewe unaishi kweli au upo upo tu, na unajiuliza kama utaishi milele hata baada ya kifo. Kila mtu anapenda uzima. Na hilo linawezekana iwapo unamwamini Kristo, na unamkabidhi maisha yako, yeye aliye nuru ya ulimwengu, yeye mleta uzima, na yeye ndiye nuru ya Imani yako.
Kwa leo tunaishia hapo, kwa niaba ya watangazaji wote wa Radio Vatican, nakutakia kila la kheri na maisha ya furaha ndani ya Kristo Mwanga wa Mataifa, mimi ni sauti ya kinabii, Padre Celestin Nyanda.








All the contents on this site are copyrighted ©.