2013-08-15 11:15:32

Fanyeni hija ya imani, mkitambua kwamba ninyi ni Wamissionari mnaotumwa kutangaza Injili ya Kristo!


Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe waamini wa Jimbo Katoliki la Concepciòn, lililoko nchini Argentina katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Jimbo hili lilipoanzishwa. Baba Mtakatifu anamwambia Askofu Armando Josè Rossi kwamba, anasikitika kuona waamini wanaojitafuta na kujifungia katika ubinafsi wao.

Hii ni changamoto kwa Kanisa kuendelea kupandikiza mbegu ya miito mitakatifu, kama ilivyokuwa kwa miaka kadhaa Jimboni humo, kwani hapa ilikuwa ni chemchemi ya miito ya Kipadre na kitawa. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, anaendelea kukazia mambo makuu matatu: hija, utume pamoja na kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Waamini wanapaswa kuonesha ari na mwamko katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Waoneshe hali ya unyenyekevu ili kuweza kujifunza zaidi kutoka kwa Roho Mtakatifu kwani kuna hatari kwa baadhi ya waamini kudhani kwamba, wao wanafahamu ukweli mkamilifu, hali inayoweza kuwapotosha katika maisha ya kiimani na hatimaye kujikuta wanajitafuta wenyewe na kumwacha Kristo ambaye ni Mkombozi wa dunia.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujitahidi kukutana na Kristo katika hija ya maisha yao kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti, ili hatimaye, kuonja ile furaha ya Habari Njema ya Wokovu inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Waamini wajitahidi kumfahamu, kumpenda na kumwabudu Kristo kwa kutambua kwamba, wao kama wafuasi wake wanatumwa kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao ambayo yanapaswa kuwaletea watu mabadiliko ya ndani. Hii ni changamoto kwa waamini kujitosa kutangaza Injili ya Kristo kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Jimbo Katoliki la Concepciòn, Argentina kwa kuwaweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, aliyebahatika kumfahamu, kumsikiliza na kumwabudu na kumshuhudia Mwana wa Mungu, mwaliko kwa waamini kumfahamu na kumpenda Kristo kama alivyofanya Bikira Maria.







All the contents on this site are copyrighted ©.