2013-08-15 12:06:56

Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni ni kielelezo cha mapambano, ufufuko na matumaini ya Familia ya Mungu


Hata Bikira Maria aliomba kwa sala zake paji la Roho Mtakatifu ambaye alimfunika tayari kama kivuli siku ya kutangazwa kwake. Mwishowe, Bikira Maria asiye na doa, aliyekingiwa na kila doa la dhambi ya asili, baada ya kuhitimisha mwendo wa maisha yake hapa duniani, aliinuliwa katika utukufu wa mbinguni: mwili na roho, akatukuzwa na Mwenyezi Mungu kama Malkia wa ulimwengu, ili aweze kufananishwa kikamilifu zaidi na Mwanaye Yesu Kristo, aliye Bwana wa mabwana.

Bikira Maria aliyetukuzwa mbinguni mwili na roho, ni sura na mwanzo wa Kanisa ambalo litapata utimilifu wake katika ulimwengu ujao. Kadhalika anang'aa duniani kama alama ya hakika ya matumaini na ya faraja kwa Taifa la Mungu lililosafarini, mpaka siku ya Bwana itakapokuja. Huu ni utajiri wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika hati yake ya kichungaji kuhusu Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, akiwa mjini Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma, amesema kwamba, Liturujia ya Neno la Mungu katika Sherehe hii ina utajiri mkubwa unaoonesha mapambano, ufufuko na matumaini ya Familia ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema Kanisa liko kwenye mapambano, limekwishapata ushindi lakini mapambano baado yanaendelea kutokana na uwepo wa Shetani anayepingana na Mungu. Waamini wanapaswa kusimama kidete katika mapambano haya wakitambua kwamba, wanasindikizwa na Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni na sasa anafurahia utukufu wa Mwanaye Mpendwa.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujivika silaha ya sala na kwa namna ya pekee Tafakari ya Rozari Takatifu, ambayo kimsingi ni muhtasari wa Injili, silaha madhubuti katika mapambano dhidi ya Shetani na wafuasi wake.

Baba Mtakatifu Francisko anawambia waamini kwamba, imani yao inapata chimbuko lake kutokana na mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Hili ni tukio la imani, kama lilivyo tukio la Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho mintarafu mpango wa Kristo. Ubinadamu wa Bikira Maria umeinuliwa kwa njia ya kifo cha Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo aliyeingia kwenye maisha ya uzima wa milele mwili na roho.

Hata Bikira Maria amefuata nyayo za Mwanaye katika maisha ya uzima wa milele. Bikira Maria alionja mateso ya Msalaba wa Kristo, akaungana naye hadi dakika ya mwisho na hatimaye, akafufuliwa kutoka katika wafu na kupalizwa mbinguni.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Injili inaonesha matumaini baada ya mapambano kati ya maisha na kifo; wema na ubaya; Kristo mfufuka anaonesha ushindi wa upendo na kwamba, Utenzi wa Bikira Maria ni wimbo wa matumaini ya watu wa Mungu wanaofanya hija ya maisha katika historia; watu ambao wamewaonjesha jirani zao matumaini pale walipokuwa wamekata tamaa.

Hata leo hii Mama Kanisa anaendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa matumaini hasa katika maeneo ambayo Wakristo wanadhulumiwa na kuteswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Bikira maria daima yuko karibu na wote wanaoteseka, anafanya hija pamoja nao; anateseka na kuimba nao utenzi wa matumaini.







All the contents on this site are copyrighted ©.