Siku kuu ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho!
Mpendwa mwana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa
mbinguni mwili na roho. Ni zawadi kwa Mama Bikira Maria anayokabidhiwa mwishoni mwa
maisha yake hapa duniani. Sherehe hii huja kila tarehe 15 ya mwezi wa nane kadiri
ya kalenda ya kiliturujia ya Kanisa Katoliki. Tunaposherehekea
kupalizwa mbinguni kwa Mama Bikira Maria tunashangilia, lakini pia tunataka kukua
katika imani katoliki ambapo tunakumbuka kuwa mama kanisa mnamo Novemba 1, 1950 katika
mamlaka aliyokabidhiwa na Kristo, Baba Mtakatifu Pio XII katika ile hati iitwayo Munificentissimus
Deus, ambayo tunaweza kuitafsiri kama “Mungu Mkarimu” alifundisha wazi na kwa milele
kuwa Mama Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili ili amzae Mwana wa Mungu, aliyempa
Yesu Kristo damu yake ya kibinadamu, akaambatana naye mpaka chini ya msalaba, amepalizwa
mbinguni mwili na roho. Amepalizwa mbinguni mwili na roho ikiwa ni tuzo toka kwa Bwana
wetu Yesu Kristo.
Fundisho hili la kupalizwa mbinguni mwili na roho, limefundishwa
baada ya tafakari kina, kanisa likinyanyua maombi yake kwa Mungu, kwa njia ya Roho
Mtakatifu wa ukweli, katika unyenyekevu na udumifu na hivi ikafunuliwa wazi na Mungu
mwenyewe kuwa Bikira Maria amepalizwa mbinguni. Mpendwa msikilizaji, ni zawadi
kwa kanisa, ni zawadi kwa kila mmoja wetu na hivi kinachofuata baada ya kupokea zawadi
hii ya imani, ni heri na vigelegele kwa kwa kanisa takatifu mbele ya Mama Bikira Maria
mtukuka aliye pia Mama wa Kanisa.
Mpendwa mwana wa Mungu, kwa sherehe hii
tunafurahia kushirikishwa kwa Mama Bikira Maria katika utukufu wa mwanae Yesu Kristo
Mkombozi pekee wa ulimwengu. Utukufu ambao mama huyu ameushiriki tangu mwanzo kwa
fumbo la umwilisho, yaani Yesu Kristo kutwaa mwili wa kibinadamu kwa njia yake. Si
hilo tu bali kupalizwa mbinguni kunaambatana na Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo
na ufufuko wa Kristo na hivi Bikira Maria anamsindikiza Mwanaye mpaka chini ya Msalaba
akishuhudia mates na kifo chake.
Kwa namna hiyo basi, Mwana asingeweza kumwacha
Mamaye aoze kaburini, lazima amtuze zawadi hiyo ya kupalizwa mbinguni. Kumbe Kanisa
linapiga vigelegele kwa sababu ya kutukuzwa kwa Mama wa Mungu lililo tunda la ufufuko.
Katika
kusherehekea kupalizwa mbinguni kwa mama Bikira Maria yafaa kutambua na kujifunza
kidogo upi ni mzizi wa Bikira Maria kupalizwa mbinguni. Ndiyo kusema tangu mwanzo
Mungu aliweka jambo hili katika mpango mathubuti. Tunaona katika kitabu cha Mwanzo,
lile anguko la wazazi wa kwanza yaani Adamu na Eva, ambao kwa njia yao kifo kinaingia
duniani, na mara moja tangazo la upendo toka kwa Mungu linatolewa kwa mwanadamu, likiwa
ni kandamizo kwa shetani kama tusomavyo “nitaweka uadui kati yako wewe na huyo mwanamke”
Mw 3:15 yaani nyoka aliyeleta anguko kwa wazazi wa kwanza anaambiwa atawekewa uadui
mkali na uadui huu utakuja kwa njia ya mwanamke.
Kwa vyovyote vile mwanamke
huyu asingeweza kuwa Eva kwa maana Eva na nyoka walifanya urafiki. Ni lazima awe mwanamke
mpya kabisa. Mwanamke huyu kadiri ya mafundisho ya mababu na walimu wa Kanisa ni Mama
Bikira Maria, ni Eva mpya, ni yule ambaye wokovu utaingia duniani kwa njia ya utii
wake wake kwa Mungu. Kumbuka maneno yake kwa Malaika Gabrieli akisema, “nitendewe
kama ulivyonena” Na zaidi ya hilo uzao wake haiwezekani ukawa ni Adamu bali ni Adamu
mpya, na hivi Yesu Kristo Masiha atakayetangaza uadui dhidi ya dhambi na kifo yaani
dhidi ya utawala wa shetani.
Kristo mshindi wa kifo, aliye Adamu mpya haachi
kumshirikisha mama kwa karibu katika vita dhidi ya kifo na kwa namna hiyo basi Yesu
na Maria wako pamoja katika uadui dhidi ya nyoka kielelezo cha mwovu shetani. Bikira
Maria ni mkombozi mwenza na hivi kwa sababu Mkombozi Yesu Kristo anapokufa mara moja
kifo chake kinafuatwa na ufufuko, vivyohivyo mkombozi mwenza Mama Bikira Maria anapokufa
lazima kifo chake kifuatwe mapema iwezekanavyo na ufufuko kabla ya ufufuko wa wote
na hapa ndipo kuna kupalizwa mbinguni. Mantiki hii inakuzwa na mababu na walimu wa
Kanisa wakianzia pale katika Proto – Evangelium kitabu cha Mwanzo sura ya 3 : 15,
Kama tulivyokwisha sema hapo mwanzoni.
Katika Agano Jipya, Bikira Maria anapokea
salaam ya pekee toka kwa malaika Gabriel akimwambia “salaam Maria ewe uliyebarikiwa
na Mungu! Bwana yuko nawe” Lk 1:28. Salaam hii ni amkio la juu kabisa lenye kuonesha
kuwa tangu mwanzo wa maisha yake na hata mwisho hana doa la dhambi. Na hivi hayuko
chini ya utawala wa kifo kilicho tabia ya dhambi.
Ni mkingiwa dhambi ya asili
na hivi kwa namna yoyote angepalizwa mbinguni mwili na roho. Anaambiwa umebarikiwa
kuliko na kati ya wanawake wote, kumbe baraka yake haichangamani na baraka za wengine.
Baraka hii haiji tu bali anapewa kwa sababu amejaa neema tangu kuumbwa kwake na kwa
sababu hiyo uwepo wa Bwana ni mkamilifu katika yeye. Baraka aliyonayo mama Bikira
Maria ni kinyume na laana ya kale ya kurudi mavumbini kwa wazazi wetu wa kwanza. Mw.
3:19. Ndiyo kusema kama Kristu ni mshindi dhidi ya kifo kilicholetwa na Adamu, basi
Maria ni mshindi dhidi ya kifo kilicholetwa na Eva.
Kwa ushindi huu lazima
Bikira huyu atuzwe zawadi ya kushiriki utukufu wa Mwanae kabla ya wanadamu wengine
wote, ndiyo kupalizwa mbinguni.
Kupalizwa Mbinguni ni kuendeleza ushindi na
ni mlango wa kumfuasa Kristu kuingia mbinguni kwetu sisi tuliokabidhiwa kwake pale
chini ya msalaba. “mama tazama huyu ndiye mwanao”! Kamwe mama hatatuacha katika uvuli
wa machozi, lazima atatoa chozi la upendo kwa mwanae na tutapata ondolea na msamaha
wa dhambi. Nani kama mama?
Mpendwa unayenisikiliza, kwa kupalizwa kwa Mama
Bikira Maria mbinguni tunaona ujio wa shime kwa akina mama wote, na hivi tunashangilia
nafasi kubwa katika maisha ya akina mama wanayozawadiwa kwa ushindi wa Maria mama
mtukuka, tunda la kwanza la ukombozi.ni ushindi wa akina mama wote, ni ushindi wa
familia zote.
Mpendwa mwana Kanisa tunapoadhimisha sherehe hii tunawaombea
watawa wote wa mashirika mbalimbali waliojiweka chini ya ulinzi wa Bikira Maria mpalizwa
mbinguni. Washike imani katoliki, wampende mama Maria kwa heshima na uchaji wa juu
na zaidi wakue katika fumbo na fundisho hili la kupalizwa Mbinguni mama Bikira Maria.
Kwa namna ya pekee tunaalikwa pia kuwaombea Wamisionari wa Damu Takatifu ya
Yesu ambao tarehe 15 Agosti 1815 Shirika lao lilianzishwa na Mtakatifu Gaspari na
kuwekwa chini ya ulinzi wa Bikira Maria wa Damu Takatifu. Wamisionari hawa wanafanya
kazi katika mabara ya Amerika, Ulaya, Asia na zaidi sana Afrika katika nchi ya Tanzania
na Guinea Bissau. Wajibu na karama ni kutangaza upendo wa Damu Takatifu ya Kristu
iliyotolewa msalabani kwa ukombozi wa ulimwengu.
Ninakusindikizeni kwa tafakari
hii nikikuombea baraka tele za Bwana katika maisha yako zinazomwagika na kububujika
kwa njia ya Bikira Maria mpalizwa Mbinguni, mama mtukuka juu ya wanawake wote, malkia
wa mbinguni.
Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii Imeletwa Kwako na Padre Richard
Tiganya, C.PP.S.