2013-08-14 08:08:26

Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe Padre na Shahidi wa Mwanga wa Imani


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Agosti, anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Maximiliani Maria Kolbe, Padre na Mfia dini. Ni Padre aliyependa kwa dhati, akalimwilisha pendo hili kwa matendo na katika ukweli kama Padre na shahidi wa mwanga angavu wa imani inayomwilishwa katika matendo.

Ni shahidi aliyeongozwa na Mwanga wa Kristo Mfufuka, kiasi cha kuyatoa maisha yake kwa ajili ya Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kichungaji Lumen Fidei, Mwanga wa Imani anasema, huu ni mwanga wenye nguvu na uwezo wa kumwangazia mwanadamu katika maisha yake yote, kwani ni Mwanga unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, aliye hai, Mungu ambaye ni upendo mkalimifu, unaomchangamotisha mwamini kujenga maisha thabiti.

Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe katika Mwaka wa Imani, ambao waamini wanaalikwa kuishuhudia imani yao katika matendo, kwa kujiaminisha kwa Kristo aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kama kielelezo cha juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu.

Kutokana na ukweli huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha Imani kwani unafumbata upendo wa Mungu, ushuhuda na tafakari ya kina, ili kila mtu anayemwangalia Yesu pale Msalabani aweze kuamini na kuokoka.

Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe alizaliwa kunako mwaka 1894, akajiunga na Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko kama mtawa. Akakuza na kuimarisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, kiasi hata cha kuanzisha "Jeshi la Bikira Maria".

Ni Padre aliyetekeleza utume wake kwa njia ya mahubiri ya kina yaliyokuwa yanabubujika kutoka katika Neno la Mungu. Alikuwa ni mwandishi mahiri aliyetumia taaluma yake kuendeza Habari Njema ya Wokovu na Kweli za Kiinjili. Alionesha ari na mwamko mkubwa wa shughuli za kimissionari Barani Ulaya na Asia.

Wakati wa madhulumu ya Kinazi, alitupwa kizuizini na kuonja mateso na madhulumu ya utawala wa kinazi kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Akiwa gerezani akaamua kutoa sadaka ya maisha yake kama Padre ili kuokoa maisha ya Baba wa familia, aliyekuwa mwenza pale gerezani, ushuhuda wa hali ya juu wa imani inayomwilishwa katika matendo. Akafariki dunia kwa njaa hapo tarehe 14 Agosti 1945.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili wakati akielezea sifa za Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe alisema kwamba, ni msimamizi wa hali tete katika karne hii. Mama Kanisa anapofanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe sanjari na Mwaka wa Imani anapenda kuweka mbele ya macho ya waamini matatizo na changamoto zinazoendelea kumwandama mwanadamu katika nyakati hizi za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Licha ya maendeleo makubwa katika sayansi na teknolojia, lakini kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na matatizo pamoja na mahangaiko ya wengine, kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko, kuna mamillioni ya watu wanaoteseka kutokana na balaa la njaa na utapiamlo duniani. Uchu wa mali na madaraka ni kati ya mambo ambayo yameendelea kusababisha vita na madhulumu kwa watu wasiokuwa na hatia, changamoto ya kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli unaojikita katika toba na wongofu wa ndani.

Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe kwa ushuhuda wa maisha yake ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuthamini tunu ya uhai ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, waamini wajitahidi kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na Fumbo la Kifo kwa: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma. Katika mwaka wa Imani, hii ndiyo imani katika matendo inayoongozwa na Mwanga wa Kristo Mfufuka.

Tafakari hii imeandaliwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.